Makampuni yajitosa mechi ya Stars

Muktasari:

Stars imefuzu hatua ya pili ya mashindano ya kufuzu Chan baada ya kuitupa nje Kenya kwenye raundi iliyopita

WAKATI siku mbili zikibaki kabla ya mechi ya kuwania kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wanaocheza ligi za ndani (Chan), baina ya Tanzania 'Taifa Stars' na Sudan, kampuni kadhaa zimejitolea kugawa tiketi za bure kwa mashabiki ili kutazama pambano hilo.
Mechi hiyo itachezwa Jumapili, saa 1.00 usiku kwenye Uwanja wa Taifa jijini huku bei ya chini ya tiketi ikiwa ni Shilingi 1000.
Tiketi hizo za bure zilizotolewa na kampuni hizo ambazo mashabiki watagawiwa, watapatiwa kupitia kamati ya hamasa ya hiari ya waandishi wa habari kwa timu za taifa pamoja na kamati ndogo ya hamasa ya Taifa Stars.
Kampuni hizo ambazo zimeamua kutoa tiketi za bure ni GF Trucks & Equipments ambayo itatoa tiketi 500 na Asas itakayotoa tiketi 1000.
"Kwa upande wetu wanahabari tunawaomba Watanzania wajitokeze kwa wingi kwenye Uwanja wa Taifa siku ya Jumapili na pia waendelee kuonyesha uzalendo kwa timu zetu na nchi kiujumla.
Tumefurahi kuona tumepata kampuni ambazo zimeunga mkono harakati zetu waandishi wa habari na mfano ni GF Trucks & Equipments ambayo imetoa tiketi 500 ambazo tutazigawa kwa makundi mbalimbali kama vile watoto yatima, wanafunzi na mashabiki wa soka," alisema mwakilishi wa kamati ya hiari ya hamasa kwa waandishi, Pascal Kabombe.
Kwa upande wake mwenyekiti wa kamati ndogo ya hamasa ya Taifa Stars, Haji Manara alisema kuwa kampuni ya Asas nayo imeamua kugawa tiketi za bure kwa mashabiki.
"Sifa yetu kubwa Watanzania ni kujaza uwanja na sina shaka na hilo kwenye mechi yetu dhidi ya Sudan, Jumapili kwamba tutaujaza uwanja na vitochi vyetu kwa ajili ya kuhanikiza na mimi nitakuja na taa ya chemli kabisa.