Makame naye ajifariji, Metacha freshi

Thursday March 26 2020

 

By OLIPA ASSA

KIUNGO fundi wa mpira ambaye amekuwa akisugua benchi kwa sasa ndani ya Yanga, Abdulaziz Makame amekiri mambo ni magumu, lakini atapambana kurejea kikosi cha kwanza, huku kipa Metacha Mnata akieleza namna alivyofanikiwa kutimiza ndoto zake.

Tuanze na Makame, enzi za Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera kiungo huyo alikuwa ana nafasi kikosi cha kwanza ila chini ya Luc Eymael amekuwa akisugua benchi.

Hata hivyo, kiungo huyo kutoka Zanzibar, alisema jambo hilo linamkwaza, lakini anaamini bado ana nafasi ya kujituma na ipo siku atakuwa tegemeo katika kikosi cha Eymael.

“Kila jambo lina wakati wake, mdogo mdogo nitatimiza malengo yangu kwani sijioni kama nimefika na siku zote mwenye njaa ndiye anayetafuta sana,” alisema Makame.

Lakini kwa upande wa kipa Metacha amekiri mpaka sasa amepiga hatua kubwa tangu ajiunge na Yanga msimu huu akitokea Mbao FC.

Metacha alisema moja ya mafanikio kuwa ni kuitwa timu ya taifa ambako amekwenda kupata mbinu tofauti zinazomsaidia kufanya vyema akiwa na Yanga.

Advertisement

“Kabla ya Juma Kaseja hajaumia tulipoitwa pamoja timu ya taifa, nilikuwa najifunza mengi kwani ni kati ya makipa bora nchi hii, baadhi ya mbinu nazitumia kuisaidia timu yangu,” alisema.

Mbali na kuitumikia Taifa Stars, alisema Yanga imemtangaza kwa wadau wa soka nchini na amekuwa akipita sehemu imekuwa rahisi kutatuliwa shida zake.

Advertisement