Makambo atua, atangaza kiama

Muktasari:

  • Akizungumzia taarifa za kudaiwa kutoroka, mshambuliaji huyo ameshangaa akisema kuondoka kwake kulikuwa baraka za uongozi.

ZILE stori zilizoenezwa mtandaoni kwamba straika Heritier Makambo eti katoroka, zimezimwa kibabe, baada ya straika huyo tegemeo wa Yanga kutua alfajiri ya jana Jumatano na kushusha presha Jangwani, lakini akatangaza vita nzito ya ufungaji.

Makambo ambaye aliripotiwa na gazeti hili kwenda kwao kwa matatizo ya kifamilia na kuelezwa angerejea kati ya juzi na jana amerejea huku akifichua kuwa, amerejea ili kuendelea na moto wake wa kutupia kambani na kuwaonya wapinzani wake.

Akizungumza na Mwanaspoti Makambo alisema amerejea kuendelea na kazi yake na kwa sasa yuko imara zaidi kuendeleza kazi ya kufunga mabao na kudai wapinzani wake wajiandae kuteseka kwake katika duru la pili.

Makambo mwenye mabao 11 alisemaa kwa sasa anajiona yuko sawa baada ya kumaliza matatizo yake binafsi yaliyomrudisha kwao na akili yake inawaza kufunga zaidi.

Alisema kwa sasa anazijua timu zote pinzani na aina ya mabeki wao na ingawa anatambua kwamba ushindani utakuwa mkali lakini atakabiliana nao kuweza kuipaisha timu yake.

“Niko sawa sasa, nimemaliza matatizo yote yaliyokuwa yananisumbua nimerudi kazini kuendelea na kazi yangu kama awali,” alisema Makambo.

“Nataka kufunga zaidi najua ligi ni ngumu lakini sasa nazijua timu zote siwezi kukata tamaa nimejiandaa kufunga zaidi katika nafasi nyingi nitakazotumia.

Akizungumzia taarifa za kudaiwa kutoroka, mshambuliaji huyo ameshangaa akisema kuondoka kwake kulikuwa baraka za uongozi.

Alisema viongozi wake wote wa klabu na hata kocha wake, Mwinyi Zahera alikuwa na taarifa juu ya kuondoka kwake.

“Nilipofika Kinshasa nikasikia huku kuna habari eti nimetoroka nilishangaa sana, haikuwa kweli sijajua ni nani amesema hivyo, kabla ya kuondoka niliomba ruhusa kwa uongozi na hata kocha aliniruhusu,” alisema Makambo.