Maka atupiwa virago Ihefu SC, ila bado kuna tatizo

WAJUKUU wa Mbogo Maji, Ihefu SC tayari wameanza kuyaona machungu ya Ligi Kuu, wanaanza kushikana uchawi huko na mwisho wa siku Kocha Maka Mwalwisi akafungashiwa virago.

Unapozungumzia moja ya timu zenye uchumi mzuri kwenye Ligi Kuu Bara, huwezi ukaacha kuitaja Ihefu SC kutoka Mbarali mkoani Mbeya kwani imejitosheleza vilivyo.

Huu ni msimu wa kwanza wa Ihefu kwenye Ligi Kuu, lakini imeizizidi hata timu kongwe. Timu hiyo ina uwanja, hosteli pamoja na usafiri wa kisasa. Tatizo kubwa la timu hiyo ni mwenendo wake katia ligi tangu ilipopanda ambao umekuwa wa kusuasua. Licha ya kucheza kandanda safi, lakini haipati matokeo mazuri jambo ambalo limeanza kutiliwa shaka.

Hakuna wachezaji wapambanaji na hata kocha atakayekuja inabidi ajivike mabomu kwa kikosi hicho. Kwa hapa Maka anapaswa kulaumiwa kwani ndiye aliyehusika na usajili akiwa na viongozi wa timu.

TATIZO LIKO HAPA

Ihefu SC inacheza soka la kuvutia na hata walioshuhudia mchezo wa kwanza dhidi ya Simba, Uwanja wa Sokoine, Mbeya, licha ya kufungwa mabao 2-1, lakini wengi walifurahishwa na soka walilotandaza.

Ihefu ilijitahidi kuishika Simba na kuwapa matumaini watu wa Mbeya kuwa wamepata ‘kitu’ kutokana na mwenendo wa Mbeya City kuwa mbovu, huku Tanzania Prisons ikihamia Nelson Mandela, Sumbawanga.

Habari za ndani ni kwamba, baada ya timu hiyo kupanda Ligi Kuu kulijitokeza makundi ambayo hayakuweka taswira nzuri kwa wakazi wa Mbarali katika kuisapoti timu yao. Inaelezwa wakati timu ikiwasili kutoka Mwanza kucheza na Mbao FC na kupanda Ligi Kuu, wadau waliandaa mapokezi, lakini sherehe hizo hazikufanyika.

MAKA ABEBESHWA ZIGO

Siku zote timu inapofanya vizuri mara nyingi wanaopongezwa ni wachezaji, lakini ikiboronga mtu wa kwanza ni kocha na ndicho kilichotokea kwa Maka Mwalwisi.

Wiki iliyopita uongozi wa Ihefu ulitangaza kuachana na kocha huyo aliyeisaidia kupanda Ligi Kuu akiipokea timu ikiwa nusu msimu Daraja la Kwanza.

Katika taarifa iliyotolewa Oktoba 6 ilieleza kuwa imeamua kusitisha mkataba na kocha huyo na kumtakia heri kokote aendako.

Maka alijiunga na timu hiyo akipokea mikoba ya Salhina Mjengwa aliyetimuliwa baada ya kupoteza michezo kadhaa na kuifanya timu hiyo kupoteza mwelekeo Daraja la Kwanza baada ya kuongoza kundi kwa muda mrefu kisha kupitwa na Dodoma Jiji FC.

Maka alikuwa kocha msaidizi wa Mbeya City ilipopanda Ligi Kuu msimu wa 2013/14, huku Juma Mwambusi akiwa kocha mkuu. Baada ya hapo alitimkia Panone, Mlale FC na Mbeya Kwanza - zote zikiwa za Daraja la Kwanza.

SIO SHWARI

Katika michezo mitano ya ligi iliyocheza Ligi Kuu timu hiyo imeshinda mchezo mmoja dhidi ya Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Sokoine kutokana na bao la Enock Jiah katika dakika ya saba ya mchezo uliopigwa Septemba 13.

Ihefu imepoteza michezo minne, ikiruhusu mabao saba huku ikifunga mabao mawili na sasa inashika nafasi 19 ikiwa na alama tatu huku mkiani ikiwapo Mbeya City yenye alama moja.

Ihefu ilichapwa mabao 2-1 na Simba, 1-0 na Mtibwa Sugar, 2-0 na Mwadui FC kisha ikalala 2-0 mbele ya Gwambina FC. Inatakiwa kujipanga zaidi maana msimu ujao zitashuka timu nne moja kwa moja huku zinazokamata nafasi ya 13 na 14 zikicheza mtoano.

Kibarua kikubwa mchezo unaofuata itakapokuwa ugenini kukipiga na Biashara United ambayo haijapoteza mchezo hata mmoja wa ligi msimu huu, kisha itacheza na Azam ambayo ipo kileleni na haijapoteza mchezo ikiwa imeruhusu mabao mawili kwenye michezo mitano.

TETESI ZA MAKOCHA

Hadi sasa timu ipo chini ya James Wanyato huku taarifa za chini zikieleza makocha kadhaa tayari wameomba kazi ya kuifundisha akiwemo Samuel Moja.

Moja aliwahi kuifundisha Lipuli FC na kuisaidia kutinga fainali ya Azam Sports Federation (ASFC) mwaka juzi na kupoteza kwa bao 1-0 mbele ya Azam FC katika mchezo uliofanyika Uwanja wa Ilulu, Lindi.