Majina ya mastaa hawa yatatikisa kinoma usajili ujao

Muktasari:

Hata hivyo, hiyo ni moja ya dili nyingi za wachezaji ambao wanadaiwa kwamba watatingisha sana wakati dirisha la usajili litakafunguliwa kwa sababu watagombewa kila kona. Hii hapa orodha ya masupastaa wa soka watakaotikisa dirisha lijalo la usajili kutokana na timu kibao kuhitaji huduma zao.

London,England. MANCHESTER United wameripotiwa kuwa na mpango wa kupeleka ofa yao ya pili huko Real Madrid kumnasa Gareth Bale baada ya kudaiwa dili la kubadilishana na Alexis Sanchez kushindwa kutiki.

Jambo hilo haliwashangazi watu kwanini limekwama kwa sababu Los Blancos wasingekubali kumkukubali Sanchez baada ya kiwango chake kuwa cha chini tangu alipojiunga na Man United akitokea Arsenal kwenye dirisha la Januari mwaka jana.

Hata hivyo, hiyo ni moja ya dili nyingi za wachezaji ambao wanadaiwa kwamba watatingisha sana wakati dirisha la usajili litakafunguliwa kwa sababu watagombewa kila kona. Hii hapa orodha ya masupastaa wa soka watakaotikisa dirisha lijalo la usajili kutokana na timu kibao kuhitaji huduma zao.

Eden Hazard – (Chelsea)

Likitajwa jina la Eden Hazard kwa sasa basi moja kwa moja linahusishwa na klabu ya Real Madrid baada ya staa huyo wa Kibelgiji kugoma kusaini mkataba mpya huko kwennye klabu yake anayocheza kwa sasa, Chelsea. Kwa muda sasa, Los Blancos wametajwa kuwa na mpango wa kumchukua staa huyo wa zamani wa Lille na hasa baada ya kocha Zinedine Zidane kurudi Bernabeu. Hata hivyo, saini yake haitapatikana kirahisi, hivyo ni mchezaji atakayetikisa kwenye dirisha linalokuja la usajili.

Christian Eriksen – (Tottenham)

Tottenham Hotspur inajaribu kuweka ugumu kwa kiungo wao Eriksen ili asipatikane mnunuzi wa haraka baada ya kutaja bei kwamba staa huyo wa Denmark anauzwa Pauni 200 milioni. Staa huyo mkataba wake unaelekea ukingoni na amegoma kusaini dili jipya licha ya kupewa ofa mara tatu tofauti na uongozi wa Spurs. Kiungo huyo anawindwa na Real Madrid, lakini Barcelona nao inamtaka sambamba na Manchester United jambo litakaloibua ushindani mkali mwishoni mwa msimu huu wakati Spurs itakapoamua yaishe kwa kumpiga bei.

Raheem Sterling – (Man City)

Mwingereza, Raheem Sterling anacheza soka la ubora wake kwa sasa huko Manchester City kutokana na kile anachompatia kocha Pep Guardiola. Hivi karibuni kuliibuka taarifa za kwamba kocha Zinedine Zidane anamtaka staa huyo kitu ambacho hakika kitaleta vurugu kubwa kwenye dirisha lijalo la usajili kama kikosi cha Los Blancos kitaamua kuwa siriazi kwenye kuitaka saini yake hasa ikizingatiwa kwamba hata Man City wenyewe hawatakubali kirahisi kumwaachia aondoke. Sterling anaonekana kuwa kwenye mipango ya Guardiola, hivyo Zidane kumpata itabidi apambane sana na hilo ndilo litakalofanya uhamisho wake kutikisa kama utatokea.

Paul Pogba – (Man United)

Hivi karibuni, kiungo Paul Pogba amewaaminisha Manchester United kwamba hana mpango wa kuihama timu hiyo yenye maskani yake huko Old Trafford. Miezi michache iliyopita, Pogba alikuwa akihusishwa na mpango wa kurudi kwenye klabu yake ya zamani ya Juventus baada ya kuwa kwenye malumbano yasiyokwisha na kocha Jose Mourinho. Lakini, tangu Ole Gunnar Solskjaer alipotua Old Trafford maisha ya Pogba yamebadilika na kuonyesha soka la kiwango cha juu na kuwafanya mashabiki wa timu hiyo wasitamani Mfaransa wao huyo aondoke. Kumeibuka pia habari za Real Madrid kumweka kwenye orodha Pogba. Lakini, suala la Pogba kubaki au kuondoka litategemea na Man United itakavyomaliza msimu, kama ikiwa nje ya Top Four, basi kutakuwa na vita kali ya kuhusu Pogba.

N’Golo Kante – (Chelsea)

Kiungo wa kubaka, N’Golo Kante hakuna ubishi kwamba kwa sasa hafurahii sana soka lake analocheza huko kwenye kikosi cha Chelsea. Hilo linasababishwa na namna anavyotumiwa na kocha Maurizio Sarri, akimpanga kwenye kiungo ya juu wakati kwenye eneo lenye uhodari wa wake ni kwenye kiungo ya chini, kukaba. Wachambuzi wengi wamekuwa wakimshangaa kocha Sarri kwa jinsi anavyomtumia staa huyo wa Ufaransa.

Taarifa sasa zinadai kwamba Juventus inaliona hilo na wanahitaji saini yake ili akakipige kwenye kikosi chao ambako watampanga kwenye eneo lake analopenda kucheza. Lakini, saini ya Kante haitakiwa na Juve tu, Real Madrid na Paris Saint-Germain nao inamhitaji kiungo huyo huku ni wazi kabisa ikifahamika kwamba Chelsea hawatakubali kufanya biashara. Kutokana na hilo, Kante ni staa mwingine atakayetikisa dirisha lijalo la usajili kama mwenyewe ataamua kufungua milango ya kutimkia kwingineko, kikosi kikishindwa kupata nafasi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.

David De Gea – (Man United)

Kama kuna kitu ambacho Manchester United hawakipendi kwa sasa basi ni kurejea kwa Zinedine Zidane kwenye benchi la Real Madrid. Kocha huyo Mfaransa baada ya kurudi kwenye timu hiyo tu ameamua kumweka benchi kipa Thibaut Courtois waliyemsajili mwaka jana na kumrudisha golini Keylor Navas, huku ripoti zikielezwa kwamba Zidane bado anataka tena kuvamia Old Trafford kwenda kunasa huduma ya kipa De Gea. Huko nyuma, Los Blancos ilifanya mara kadhaa jitihada za kutaka kumsajili kipa huyo Mhispaniola, lakini dili zilikwama na sasa huenda wakarudi tena kwenye dirisha lijalo huku Man United wakihangaika usiku na mchana kumsainisha dili jipya. De Gea bado anawagomea Man United juu ya mpango wa kusajili mkataba mpya akitaka alipwe pesa ndefu kwa wiki na hapo ndipo panapokuja suala la kwamba huenda kwenye dirisha lijalo akahusika kwenye usajili.

Kylian Mbappe – (PSG)

Mshambuliaji kinda wa Kifaransa, Kylian Mbappe ameondoka AS Monaco kwenda kujiunga na Paris Saint-Germain akiwa na sababu nyingi ikiwamo ya kubeba taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya. Lakini, kwenye kikosi hicho mambo hayakwenda tofauti, PSG wameendelea kufanya hivyo kwenye michuano hiyo ya Ulaya jambo linalomfanya Mfaransa huyo huenda akaingiwa na ushawishi wa kwenda kujiunga na timu itakayompa fursa ya kubeba taji hilo. Kwa muda mrefu sana Real Madrid imekuwa wakihusishwa na mpango wa kunasa huduma yake, lakini kuna vigogo wengine kama vile Manchester City na Barcelona zimekuwa zikitajwa kwamba zinahitaji saini ya mchezaji huyo kitu kinacholeta imani kubwa ya kuwapo na vita kali kwenye dirisha lijalo la usajili kama PSG watakuwa tayari kufungua milango ya kusikiliza ofa za kuwapiga bei mastaa wao ili kupunguza bili yao ya mishahara kwenye timu.

Antoine Griezmann – (Atletico Madrid)

Mwaka jana tu hapo, Antoine Griezmann alisaini dili jipya la kuendelea kukipiga kwenye kikosi cha Atletico Madrid kwa miaka mingi zaidi. Uamuzi wa kusaini mkataba hapo ulikuja baada ya jina lake kuhusishwa sana na mpango wa kwenda kujiunga na Barcelona ambao walionekana wazi wangemnasa staa huyo.

Lakini, si Barcelona tu, Griezmann aliwahi kuhusishwa pia na Manchester United na mambo yalivyokuwa yakionekana kwamba fowadi huyo wa Ufaransa alikuwa anakwenda kutua Old Trafford. Atletico mambo yao kwa siku za karibuni hayapo vizuri na Barcelona wameripotiwa kuwa na mpango wa kurudi Atletico kwenda kufanya mchakato wa kumsajili mshambuliaji huyo akambadili Luis Suarez huko Nou Camp. Griezmann anawindwa na timu kibao pia ikiwamo PSG na jambo hilo ndilo linaloongeza hisia za kwamba wakati dirisha la usajili litakapofunguliwa, basi Griezmann atakuwa mmoja wa mastaa ambao majina yao yatatikisa kwenye kipindi hicho.

Gareth Bale – (Real Madrid)

Huku kwenye Ligi Kuu England kumedaiwa kuwapo kwa vita ya chini baina ya Chelsea, Manchester United na Tottenham Hotspur juu ya mchezaji Gareth Bale. Kocha wa Man United, Ole Gunnar Solskjaer ameweka wazi kwamba mipango yao kwa sasa ni kusajili mastaa wenye viwango vikubwa na kwenye hilo Bale anahusika pia. Lakini, mwenyekiti wa Spurs, Daniel Levy amekiri kufanya jitihada za kutaka kumrudisha kwenye kikosi cha staa wao huyo wa zamani. Chelsea pia wanatajwa kwa sababu Bale anaweza kutumiwa na Real Madrid katika kufanya dili la kubadilishana wachezaji ili wao wamchukua Eden Hazard. Lakini, yote kwa yote ni kwamba Bale kwenye dirisha lijalo la usajili litakapofunguliwa, jina lake litakuwa miongoni mwa yatakayotikisa katika kipindi hicho cha usajili wa wachezaji huko Ulaya.

Neymar – (PSG)

Yanasemwa mengi kuhusu hatima ya Mbrazili Neymar huko kwenye kikosi cha Paris Saint-Germain. Kuna taarifa zinazodai kwamba staa huyo huenda akarudi zake Barcelona alikotoka miaka mitatu iliyopita. Lakini, kuna habari nyingine zinazomhusisha mchezaji huyo kuwa kwenye mipango ya kwenda kufanya mapinduzi kwenye kikosi cha Real Madrid. Mengi yanazungumza, lakini Neymar amekuwa kwenye minong’ono mingi ikiwamo ya kuhusishwa pia na Manchester United. Mambo hayo na mengine mengi ndio yanayofanya jina la mchezaji huyo kuhisiwa kwamba litakuwa gumzo sana wakati dirisha lijalo la usajili litakapofungwa hasa ukizingatia kwamba kuna timu nyingi vigogo zitaingia sokoni kusajili wachezaji wenye majina makubwa na viwango vya dunia kama Mbrazili huyo.