Majeshi haya yameibeba Simba kinoma

Muktasari:

  • Mwanaspoti limekuorodheshea majeshi ambayo yamepambana kwa namna moja ama nyingine kuhakikisha Simba inaandika rekodi.

SIMBA imetinga hatua ya robo fainali kwa mara ya tatu baada ya kufanya hivyo mara ya mwisho mwaka 2003, wakati timu hiyo ilipofika hatua ya makundi. Kipindi hicho robo fainali ilikuwa kwenye hatua ya makundi.

Katika kufanikisha hilo, Simba ina jeshi lake lililopambana kufanikisha suala hilo kwa jasho na damu kiasi cha kukata kiu ya mashabiki ndani ya Uwanja wa Taifa.

Matoke ya 2-1 dhidi ya AS Vita yaliifanya timu hiyo kusonga mbele baada ya kufikisha pointi tisa na kujihakikishia kuandika rekodi nyingine katika soka la Tanzania.

Mwanaspoti limekuorodheshea majeshi ambayo yamepambana kwa namna moja ama nyingine kuhakikisha Simba inaandika rekodi.

AISH MANULA

Ni miongoni mwa wachezaji waliochangia kwa kasi kikubwa mafanikio ya Simba katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Licha ya kufungwa mabao 12 katika mechi tatu za ligi hiyo, uwezo wake wa kupanga mabeki na kuifanya Simba kuwa imara umeiwezesha kufika hatua ya robo fainali.

Hata hivyo, Manula ni kipa ambaye amecheza mechi nyingi kuliko mwingine yeyote wa Simba hivyo anatakiwa kupatiwa msaidizi wa kumpa changamoto ambaye atakuwa mbadala sahihi katika kikosi.

COULIBALY/ KAPOMBE

Zana Coulibaly alianza kwa kusuasua katika kikosi cha Simba lakini Kocha Patrick Aussems alimpa nafasi ya kucheza katika kikosi chake licha ya mashabiki kuonyesha kutoukubali uwezo wake.

Kadiri siku zilivyosonga ndivo alivyokomaa hasa katika kupiga krosi, Kocha Aussems amekuwa akimpa majukumu ya kupiga krosi nyingi upande wake.

Mchezaji huyu amechangia katika kuhakikisha Simba inasogea ikiwa katika Ligi Kuu na Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kuiimarisha nafasi ya beki wa kulia.

Kapombe tangu amesajiliwa misimu miwili iliyopita, akitokea Azam FC amekuwa katika kiwango bora katika kutengeneza nafasi.

Uwezo wake wa kupanda na kushuka uliisaidia Simba katika Ligi ya Mabingwa Afrika lakini baadaye alipata majeraha na nafasi yake ilichukuliwa na Nicholas Gyan.

Gyan alikuwa na uwezo mzuri wa kupiga krosi kuliko kukaba, kiasi cha kuwafanya viongozi wa klabu hiyo kuingia sokoni na kumsajili Coulibaly.

MOHAMMED HUSSEIN/E KWASI

Wawili hawa wote kwa kila mmoja wao ametoa mchango katika kikosi cha Simba kwenye michezo waliyocheza.

Mohammed Hussein ambaye maarufu kama Tshabalala ameweza kuwa muhimili katika upande wa kushoto Simba, kiasi cha kumfanya awe miongoni mwa wachezaji waliocheza mechi nyingi katika kikosi hicho.

Kwasi ameshindwa kuendana na kasi ya Simba na kumfanya Tshabalala kucheza mechi nyingi, lakini katika mechi ambazo amepewa nafasi ameonyesha uwezo licha ya kutokuwa chaguo la Kocha Aussems.

PASCAL WAWA

Wakati anatua wengi walimuita babu, lakini amegeuka kuwa muhimu katika safu ya ulinzi ya kikosi cha Simba.

Katika mchezo wa mwisho wa hatua ya makundi alimdhibiti straika wa AS Vita, Mundele Makusu kiasic cha kushindwa kufanya lolote na Kocha wa AS Vita, Frolent Ibenge alimtoa.

Wawa alituliza mashambulizi akisaidiana na beki mwenzake Erasto Nyoni, lakini kazi kubwa ilikuwa ikifanywa na yeye kutokana na Nyoni kutoka katika majeraha.

ERASTO NYONI

Takribani miezi mitatu alikaa nje ya uwanja baada ya kupata majeraha ya goti katika Kombe la Mapinduzi.

Mchezo wa mwisho dhidi ya AS Vita ulikuwa ndio mchezo wake wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika tangu arejee lakini aliweza kutulia na kucheza vizuri katika mchezo huo.

Nyoni na Wawa walipeana majukumu kuhakikisha kila jambo linaenda sawa na walifanikiwa katika hilo.

JAMES KOTEI

Sio mtu ambaye anatajwa sana katika kikosi cha Simba ‘invisible’ lakini anachafua dili nyingi za upinzani katika eneo la kiungo. Kotei ni injini ya Simba katika eneo hilo.

Kila kiungo ambaye anacheza naye anakuwa huru kucheza kutokana na yeye kukaba na kuwafanya wapinzani washindwe kabisa kutamba.

Katika mchezo dhidi ya AS Vita alielewana vizuri na kiungo mwenzake, Mzamiru Yassin kiasi cha kukaba kwa pamoja na kupiga pasi za mwisho ambazo ziliweza kuwapoteza wapinzani.

CLATOUS CHAMA

Anaitwa Mwamba wa Zambia kutokana na uwezo wake wa kumiliki mpira na kupiga chenga zake za maudhi.

Dhidi ya AS Vita hakuwa na madhara makubwa ndani ya dakika 88 alizocheza lakini aliweza kuwanyanyua mashabiki wa Simba katika dakika 89 baada ya kufunga bao la ushindi.

Chama amekuwa bora katika uwanja wa nyumbani kwani ameweza kuivusha Simba mara mbili baada ya kufanya hivyo katika wa kufuzu hatua ya makundi dhidi ya Nkana Red Devils ya Zambia.

MKUDE/ MZAMIRU

Mkude amekuwa akielewana na James Kotei katika eneo la kiungo na michezo mingi walikuwa wakicheza pamoja na kulifanya eneo hilo kuwa bora muda wote.

Katika mchezo wa mwisho dhidi ya AS Vita, Mkude hakucheza kutokana na kuwa kadi mbili za njano, hata hivyo nafasi yake ilizibwa vizuri na Mzamiru Yassin.

Ndani ya dakika 10 za mwanzo Mzamiru alipotea lakini alitulia na alipoelewana tu na Kotei waliweza kutawala eneo la kiungo na kucheza pasi nyingi na kushambulia.

EMMANUEL OKWI

Hakuwamo katika kikosi kilichocheza dhidi ya JS Saoura wiki iliyopita kutokana na kuwa na majeruhi. Pengo lake katika nafasi ya ushambuliaji lilionekana baada ya kuzoeleka akicheza sambamba na John Bocco na Meddy Kagere katika eneo hilo.

Katika mchezo dhidi ya Vita alirejea na alikuwa na faida baada ya kusimama na washambuliaji wenzake hao na kumfanya Bocco kuzunguka zaidi kuwasumbua mabeki wa Vita.

John Bocco

Ameutendea haki unahodha wake baada ya kuibeba Simba mabegani kwa kutoa pasi ya mwisho kwa Chama na kuweka mpira wavuni katika bao ambalo liliivusha Simba katika hatua ya robo fainali.

Bocco alikuwa akihaha uwanja mazima kuchukua mipira kutoka katikati na kuisogeza juu hali ambayo ilikuwa ikiwafanya Kagere na Okwi wasihangaike szaidi ya kusubiri mipira ikitokea chini.

Meddie Kagere

Mpaka sasa ana mabao matano katika Ligi ya Mabingwa Afrika na kuhusika katika kuibeba Simba kuelekea katika hatua ya robo fainali.

Spidi yake imekuwa kubwa katika ufumaniaji wa nyavu kwani hata katika Ligi Kuu yeye ndiye mchezaji wa Simba mwenye mabao mengi baada ya kufunga 12 hadi sasa.

WENGINEO

Katika mchezo wa juzi Jumamosi, Kocha Asseums aliwaingiza Hassan Dilunga, Haruna Niyonzima na Rashid Juma badala ya Okwi, Mzamiru na Kotei.

Asseums alifanya hivyo ili kuongeza mashambulizi baada ya kuona hakuwa na kitu cha kupoteza, hasa baada ya kubaini matokeo kuwa 1-1 hayakuwa na faida.

Alifanya hivyo ili kuweza kushambulia zaidi na kuwatoa wachezaji ambao walikuwa wakikaba zaidi (Kotei na Mzamiru). Kitu ambacho kilisaidia kuongeza mashambulizi na kupata bao la ushindi.

AUSSEMS USIPIME

Mbeligiji huyo alionyesha kuwa ni mtu mwenye kuweza kuusoma mchezo kwa haraka na kutafuta suluhisho.

Akiwa na msaidizi wake, Deniss Kitambi katika mchezo wa juzi dhidi ya AS Vita ulipokuwa ukisomeka 1-1 hadi mapumziko waliweza kubadilisha kabisa mchezo wote.

Mabadiliko waliyoyafanya yaliibeba Simba kwani Vita walionekana kukata pumzi dakika za mwisho, hivyo mabadiliko yao yalisaidia kuongeza mashambulizi ya haraka.