Majeshi Zenji kufyekelewa mbali

Muktasari:

ZFA imesema ili kuwatambua wachezaji wote wanaocheza soka nje ya visiwa hivyo wameanza mchakato wa kuomba kufunguliwa mfumo mpya wa kuwasajili wachezaji na kuwaombea uhamisho kwa njia ya mtandao kama wanavyofanya TFF (Shirikisho la Soka Tanzania).

CHAMA cha Soka Zanzibar (ZFA) kimesema hakina rekodi ya wachezaji wote wanaocheza Ligi Kuu Bara, lakini wakafichua mpango wa kufyeka timu za majeshi ili zibaki chache kama ilivyo Bara.

ZFA imesema ili kuwatambua wachezaji wote wanaocheza soka nje ya visiwa hivyo wameanza mchakato wa kuomba kufunguliwa mfumo mpya wa kuwasajili wachezaji na kuwaombea uhamisho kwa njia ya mtandao kama wanavyofanya TFF (Shirikisho la Soka Tanzania).

Ligi Kuu Zanzibar ina timu sita za majeshi ambazo ni KMKM, Polisi, JKU, Zimamoto, Mafunzo na KVZ na mpango ujao ni kubakiza timu chache ili timu za uraiani na zenye uwazo mkubwa zipewe nafasi ya kucheza ligi.

Katibu Mkuu wa ZFA, Mohamed Ali aliliambia Mwanaspoti mpango wa usajili kwa njia ya mtandao utaanza rasmi mwakani ikiwemo kupunguza timu za Ligi Kuu kutoka 19 hadi 12.

“Kwa sasa ligi haina mdhamini wala mfadhili, watu wanaogopa kuwekeza pesa zao kutokana na uwingi wa timu, hivyo ni lazima timu zipunguzwe na zile zitakazoshiriki ligi ni zile tu zenye uwezo mkubwa maana sasa kuna timu nyingine hazina hata uwezo na sifa za ushirikishwaji kwenye ligi.”