Majeruhi waitesa Barcelona

Muktasari:

Kuumia kwa beki Thomas Vermaelen kumemuongezea hofu kocha wa Barcelona, Ernesto Valverde ambaye amebakiwa na mabeki wawili pekee wa kati Gerard Pique na Clement Lenglet huku timu hiyo ikikabiliwa na mechi muhimu za Ligi Kuu Hispania na Ligi ya Mabingwa Ulaya, hivyo kusali mabeki waliopo wasiumie katika mechi zinazowakabili kuanzia ile ya wikiendi hii.

Barcelona, Hispania. Ongezeko la majeruhi katika safu ya ulinzi ya Barcelona limeanza kumpa hofu kuu kocha Ernesto Valverde, katika kampeni ya kutetea taji la Ligi Kuu Hispania na Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Kuumia kwa Thomas Vermaelen wakati akiitumikia timu yake ya Taifa ya Ubelgiji kumemfanya aungane na Samuel Umtiti aliye majeruhi.

Madaktari wametoa ripoti inayoonyesha kuwa Vermaelen anatakiwa kuwa nje ya uwanja kwa wiki kadhaa jambo linalomaanisha Barcelona imebakiwa na walinzi wawili pekee wa kati Gerard Pique na Clement Lenglet.

Hii inaiweka timu hiyo katika presha kubwa hasa ikizingatiwa kuwa inakabiliwa na mechi tatu ngumu dhidi ya mahasimu wao wa mji wa Catalunya, Sevilla, Inter Milan ya Italia katika ligi ya mabingwa na Real Madrid katika ligi kuu.

Ingawa mechi hizo zote zitapigwa katika uwanja wao wa nyumbani wa Nou Camp lakini kutokana na kubakiwa na walinzi hao wawili pekee kocha amekumbwa na mashaka.

“Kuumia kwa Vermaelen ambaye ndiyo kwanza anarejea dimbani baada ya kuwa nje kwa muda mrefu kutokana na kuwa majeruhi ni pigo kwetu msimu huu ameanza mechi mbili tu za La Liga,” alisema Valverde.

Majeruhi wameifanya timu hiyo kubadili mfumo wake wa uchezaji badala ya kushambulia inacheza zaidi kujilinda jambo lililoipunguzia nafasi ya ushindi.

Barcelona iliyolazimishwa sare dhidi ya Athletic Blibao, Girona na Valencia, na kufungwa na timu isiyo na umaarufu ya Leganesn timu ya tatu kutokana mkiani mwa ligi hiyo.

Timu hiyo imeshuka hadi nafasi ya pili katika msimamo ikiwa na pointi 15 moja nyuma ya vinara Sevilla kila timu ikiwa imecheza mechi nane.