Majeraha yamuondoa Dube Zimbabwe

Muktasari:

Hii sio mara ya kwanza kwa Dube kucheza katika timu ya Taifa, kabla ya kutua Azam alikuwa anaichezea timu hiyo akiwa anacheza katika Ligi ya kwao.

STRAIKA Prince Dube wa Azam FC, ameshindwa kujiunga na kikosi cha timu ya Taifa Zimbabwe baada ya kuumia nyama za paja katika mchezo wao dhidi ya Kagera Sugar uliopigwa Jumapili Oktoba 4 usiku katika uwanja wa Azam Complex.

Dube ambaye ndio kinara wa mabao katika Ligi Kuu Bara akifunga matano, alitakiwa kujiunga na timu hiyo jana Jumanne, lakini kutokana na majeraha hayo imemlazimu kusalia nchini.

Kupitia katika akaunti ya Ofisa Habari wa timu hiyo, Thabit Zakaria aliandika kwamba mchezaji huyo hajaumia sana na amepewa muda wa mapumziko.

"Amepewa mapumziko ya wiki moja baada ya hapo ataanza mazoezi ya polepole kisha atarejea katika hali yake".

Zimbabwe wanajiandaa kucheza mchezo wa kurafiki katika kalenda ya Fifa dhidi ya Malawi, Oktoba 11.