Majeraha yaliyomstaafisha soka Kocha Amunike

Friday November 9 2018

 

By Dk.Shita Samwel

KWA wale wahenga wa miaka ya tisini ambao walibahatika kulitazama kombe la dunia la mwaka 1994 lililofanyika nchini Marekani moja ya Timu bora iliyoishangaza dunia ilikuwa ni kikosi cha Nigeria.
Katika kikosi hicho cha kizazi cha dhahabu alikuwamo kocha wa sasa wa timu ya taifa ya Tanzania Emanuel Amunike ambaye alikuwa winga akishirikiana vyema na mshmbuliaji wa kati Rashidi Yekini.
Amunike aliweza kupiga magoli 9 katika timu ya taifa akiwa na mastaa wakubwa ambao karibia wote walitua klabu za ulaya ikiwamo Jay-Jay Okocha, Sunday Oliseli, Daniel Amokachi na Nwankwo Kanu.
Wengine ni pamoja na Victor Ikpeba na Nwankwo Kanu, Celestine Babayaro, Uche Okechukwu, Taribo west na Tijan Babangida, Garba lawali, Mobi Oparaku, Emmanuel Babayaro na Wilson Oruma.
Amunike aliwahi kuichezea klabu ya Zamalek ya misri na Sporting CP ya Ureno na kuziwezesha kutwaa ubingwa wa ndani, mwaka 1996 alitua Barcelona na kuungana na “Mr Phonemeno” Ronaldo De Lima.
Amunike ambaye alikuwa mchezaji bora wa Afrika hakuweza kufanya vizuri katika kikosi Catalans kutokana na majeraha ya Goti ambayo yalikuwa yakimrudia mara kwa mara.
Inaelezwa kuwa majeraha ya Goti yalikuwa yanamweka nje muda mrefu kutokana na kupona na kujirudia tena kiasi cha Barcelona kuamua kuumpeleka klabu ya Albacete ya daraja la pili mwaka 2000.
Nguli huyu wa soka alikuwamo pia katika kikosi cha dhahabu kilichonyakua kombe la Afika Mwaka 1994 aliamua kustaafu rasmi kucheza soka mwaka 2004 akiwa na umri wa miaka 33.
Historia ya majeraha ya Kocha huyu ambaye alikuwamo katika kikosi cha “dream team” kilichotwaa medali ya dhahabu katika Olimpiki ya mwaka 1996 leo amenifanya nilete ufahamu juu ya majeraha ya goti.
Takribani kila mwaka zaidi ya watu milioni tano duniani wanafika katika vituo vya madaktari wa upasuaji wa mifupa kwa ajili matibabu ya majeraha ya magoti na matatizo mengine ya magoti.
Goti ndiyo ungio kubwa kuliko yote mwilini na limeumbwa kwa ufanisi wa hali ya juu.
Ungio hili lina mfupa wa paja, wa ugoko na wa nyuma ya ugoko na kifupa duara cha goti inayounganishwa na nyuzi za ligamenti na tendoni.
Tendoni huunganisha misuli kwenye mifupa, tendoni ya misuli minne ya mbele ya paja huunganisha sehemu ya mbele ya paja na kifupa duara cha goti (Patella)
Ukiacha majeraha ya kuteguka na kuvunjika kwa mifupa inayounda goti tishu laini ikiwamo nyuzi za ligamenti na Tendoni hupata majeraha mabaya.
Majeraha makubwa ya goti yanahusisha kupasuka au nyufa katika mfupa plastiki wa goti na kuchanika au kukwanyuka kwa nyuzi ngumu zinazounga mfupa na mfupa (ligaments).
Zipo nyuzi kuu nne za ligaments katika goti ikiwamo mbili zenye umbile kama herufi X moja upande wa nyuma inayojulikana kama Posterior Cruciate Ligament (PCL) na iliyopo katikati ya goti upande wa mbele inayojulikana kama Anterior Cruciate Ligaments (ACL).
Vile vile ziko mbili za pembeni kwa kila goti kulia na kushoto, kuna iliyopo pembeni inayotazama nje ya mwili inajulikana kama Lateral Collateral Ligaments (LCL) na pembeni inayotazama ndani ya mwili inayojulikana kama Medial Collateral Ligaments (MCL).
Aina ya majeraha ya goti ambayo ndiyo mabaya ni yale ambayo yanahusisha majeraha yanayohusisha Ligamenti ya ACL eneo la mbele ya goti, nyuzi hii ndiyo inayobeba shinikizo kubwa la mwili.
Ligamenti za MCL na LCL hupata majeraha ya wastani  na majeraha ya hizi yanaweza kutibiwa na kupona na huwa na matokeo mazuri.
Ligamenti ya nyuma ya goti PCL inaweza kujeruhiwa na kuwa tatizo katika kupona kama ilivyo ligamenti ya ACL.
Nyuzi zinazoshikilia mifupa hiyo zikipata majeraha makubwa yanaweza yasipone kwa wakati.
Kuna uwezekano mkubwa jeraha alilopata kocha Amunike lilikuwa nikukatika kwa nyuzi kubwa moja wapo inayoshikilia goti pamoja na tishu za jirani na goti, ambazo huchukua muda kupona.
Nyuzi ya mbele (ACL) iliyo na umbile kama herufi “X” ndiyo ambayo inakumbwa na majeraha makubwa kwa wachezaji wa soka, jeraha kama hili ndilo linalomweka nje Oxlade-Chamberlain wa Liverpool.
Ukubwa wa majeraha haya yanaweza kuanishwa katika makundi matatu, yapo majeraha ya kawaida, yapo ya kati na makubwa.
Nyuzi hizo zinazoshikilia zinaweza kujeruhiwa na kuvutika kupita kiwango, kuchanika kidogo, kuchanika na  kuachana pande mbili au kukwanyuka toka katika mfupa uliojipachika.
Pale inapokatika pande mbili au kukwanyuka na kutoka katika mfupa uliojipachika, mejeraha ya aina hii ndiyo makubwa kwa goti na huchukua muda mrefu kupona.
Ni kawaida maumivu yakaisha kabisa kumbe kwa ndani bado nyuzi hizo au tishu laini za jirani hazijaunga vizuri kuweza kustahimili mikikimiki ya soka.
Ndiyo maana wanasoka wengi wanaopata majeraha ya goti huwa yanajirudia rudia baadaye huwa jeraha sugu na hatimaye wanasoka hulazimika kuachana na soka.
Kwa mwanasoka goti lipo katika hatari ya kujeruhiwa zaidi kuliko maungio mengine hii ni kutokana na kubebea shinikizo kubwa la uzito wa mwili na mchezo wa soka ukihitaji kulitumia vyema ungio hili.
Goti ni aina ya ungio bawawa lenye mijongeo mikuu mitatu ikiwamo kunyooka, kujikunja na kujizungusha.
Hivyo ikitokea umechezewa faulo na kulazimishwa kwenda uelekeo ambao sio wake hapo inamaana unaweza ukapata majeraha ya nyuzi za ligamenti.
Kukaa nje ya uwanja kwa miezi 3-6 ni muda mzuri wa kutosha kupumzika na ni nafasi nzuri kwa mchezaji kupona endapo tu bainisho la jeraha lake(diognosis) na matibabu yalikuwa sahihi.
Vile vile kama mchezaji alikuwa anashikamana na matibabu na ushauri anaopewa ni jambo la msingi kupona kwa wakati.
Kupona hutegemeana na kinga ya mwili, lishe, ukubwa na aina ya jeraha, eneo lilipo jeraha, umri wa mchezaji, mwili kuoana na matibabu, matumizi ya dawa za maumivu kiholela na uzito wa mwili.
Vile vile kama mchezaji atakuwa na mwenendo mbaya kimaisha ikiwamo ulevi, uvutaji wa sigara, matumizi ya vilevi vingine, kutopata mapumziko na msongo wa mawazo.
Haya ndiyo majeraha ya goti yasiyotabirika kupona ambayo yalikata ndoto za kocha wetu wa timu ya Taifa toka nchini Nigeria.


 


Advertisement