Majembe mapya Ligi Kuu England

Saturday September 12 2020

 

Pazia la Ligi Kuu England (EPL) linafunguliwa rasmi leo ambapo kutakuwa na mechi nne zitakazohusisha timu nane, huku ikiendelea kesho kwa uwepo wa mechi mbili.

Katika mechi za leo, Fulham itaikaribisha Arsenal, Crystal Palace itacheza na Southampton, Liverpool itakuwa nyumbani kupambana na Leeds United na West Ham watakuwa na kibarua mbele ya Newcastle United.

Hapana shaka kwamba kiu ya mashabiki wengi ni kutaka kuona ufanisi wa wachezaji wapya ambao timu mbalimbali zimewasajili kutoka kwingine na kwa namna gani wanaweza kutoa mchango mkubwa kwa timu zao.

Miongoni mwa wachezaji waliosajiliwa wapo wale ambao kabla hata hawajaanza kucheza, kile walichokifanya kule walikotoka kinawapa imani mashabiki na timu zao kwamba, watatoa mchango mkubwa katika vikosi vyao kwenye msimu ujao.

Ifuatayo ni orodha ya majembe mapya ambayo yanawafanya mashabiki wa EPL wakae mkao wa kula kusubiri kwa hamu.

James Rodriguez - Everton

Advertisement

Hakuna aliyetegemea kama kiungo huyo mshambuliaji angeweza kuachana na Real Madrid na kujiunga na Everton lakini uwepo wa kocha Carlo Ancelotti na dau la Pauni 12 milioni vimechangia kwa kiasi kikubwa kufanikisha usajili wa nyota huyo raia wa Colombia, mwenye umri wa miaka 29

Hakuna mwenye shaka na ubora wa Rodriguez ambaye ameshinda mataji mawili ya Ligi ya Mabingwa Ulaya akiwa na Real Madrid na katika ligi za ushindani amecheza mechi 388, akifunga mabao 104 huku akipiga pasi za mwisho 125

Hakim Ziyech - Chelsea

Mashabiki wengi wa Chelsea wanaamini kuwa Ziyech ambaye ni raia wa Morroco ataziba vyema pengo lililoachwa na Eden Hazard kutokana na kasi, chenga, krosi, pasi za mwisho na uwezo wa kufumania nyavu.

Winga huyo mwenye umri wa 27 alionyesha kiwango bora katika kikosi cha Ajax ambacho alikichezea michezo 112 na kukifungia mabao 38.

Donny van de Beek - Manchester United

Anawekwa katika kundi la viungo bora wa kati duniani kwa sasa kutokana na uwezo wake wa kuunganisha na kuchezesha timu, lakini pia anaweza kucheza vyema katika nafasi ya kiungo mshambuliaji na kiungo wa ulinzi.

Mchezaji huyo ana umri wa miaka 23 tu, lakini amekuwa nyota tegemeo katika kikosi cha timu ya taifa ya Uholanzi ambacho amekichezea mechi 12 akipiga pasi moja iliyozaa bao na hivyo kumuweka katika orodha ya wakali.

Gabriel Magalhaes - Arsenal

Safu ya ulinzi ya Arsenal ilifanya vibaya msimu uliopita na katika kuhakikisha wanatibu tatizo hilo, timu hiyo imeamua kumsajili beki wa kati raia wa Brazil, Gabriel Magalhaes kutoka Lille ya Ufaransa kwa ada ya Euro 26 milioni.

Huyu ni beki mwenye uwezo wa hali ya juu wa kutibua mashambulizi ya timu pinzani, ujanja wa kudhibiti washambuliaji na ana utulivu na matumizi ya akili pindi awapo uwanjani

Kai Harvetz - Chelsea

Kiwango bora alichoonyesha nyota huyo wa Ujerumani mwenye umri wa miaka 21 akiwa na kikosi cha Bayer Leverkusen msimu uliopita akicheza mechi 45 na kufunga mabao 18 huku akipiga pasi tisa za mwisho ndicho kinachombeba. Hapana shaka ndicho kimewashawishi Chelsea kutumia kitita cha Euro 80 milioni ili kumnasa kiungo huyo mshambuliaji.

Uwezo wake wa kufunga, kupiga pasi za mwisho, kasi na chenga ni vitu vinavyowapa jeuri Chelsea kuwa huenda wakatikisa msimu huu.

TImo Werner - Chelsea

Nyota huyo mwenye umri wa miaka 24 aliitumikia RB Leipzig kwa misimu minne akiicheza mechi 159 na kupachika mabao 95, huku akipiga pasi za mwisho 40 ambazo bila shaka zimeishawishi Chelsea kutumia kitita cha Euro 64 milioni ili kumsajili kuongeza nguvu katika safu yao ya ushambuliaji kwenye msimu ujao wa Ligi Kuu ya England.

MAJEMBE MENGINE

Wakali wengi waliotua EPL ni Alphonce Areola atakayecheza kwa mkopo Fulham akitokea PSG, Rodrigo Moreno atakiwasha Leeds akitokea Valencia.

Advertisement