Majanga yamuandama Eymael

Muktasari:

Luc alijiunga Yanga Januari 9, 2020 akitokea Black Leopards ambayo aliachana nayo Desemba, 2019, licha ya Yanga kutangaza kutoa taarifa ya kuachana naye, yeye mwenyewe amesema kuwa bado hajapokea barua rasmi inayoeleza kuwa amefutwa kazi.

SIKU moja baada ya Shirikisho la Soka nchini (TFF) kutamka kumchukulia hatua kali kocha wa Yanga, Luc Eymael kwa kauli zake za kibaguzi huku uongozi wake ukimfuta kazi, Chama cha Soka Afrika Kusini (SAFA) nacho kimetoa msimamo mkali juu yake.

Jana Julai 28, 2020, SAFA imetoa taarifa ya kutomruhusu Eymael raia wa Ubelgiji kufundisha timu yeyote katika ligi ambazo zinaendeshwa na shirikisho hilo kwa kumuandikia barua Waziri wa Michezo nchini humo kwa sababu ya kauli zake za kibaguzi alizotoa kwa mashabiki na wapenzi wa mpira wa Tanzania.

Katika taarifa huyo SAFA imesisitiza na kushauri klabu za Bara la Afrika kuhakikisha kuwa zinafanya uchunguzi wa kina kabla ya kuwachagua makocha wa kufundisha kwenye timu zao.

SAFA imesema kuwa inaungana na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na haitatoa kibali kwa klabu yeyote ambayo itamsajili kocha huyo na kuhakikisha watapeleka taarifa zake FIFA na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

"Vitendo vya kibaguzi kama hivyo ni vya kupingwa na kukemewa vikali, kocha kuwa na leseni ya FIFA haimfanyi kupata kazi kwenye Bara letu, lazima timu za Afrika zijitafakari mara mbili mbili," imeeleza taarifa hiyo.

SAFA imesema kuwa Luc hapaswi kufungiwa Afrika tu, bali ni Dunia nzima kwa kuwa hakuna mahali ambapo ubaguzi wa rangi unakubalika.

Baada ya kusambaa kwa kipande cha sauti cha Luc ambacho kilikuwa inalenga ubaguzi wa rangi kwa mashabiki wa soka hapa nchini, Yanga ilitoa taarifa ya kumfuta kazi na kuahidi kuchukua hatua stahiki kwa tukio hilo.

TFF nayo ilikitoa taarifa ya kuwasilisha suala hilo kwa mamlaka husika ikiwemo kumshitaki FIFA.

Luc alijiunga Yanga Januari 9, 2020 akitokea Black Leopards ambayo aliachana nayo Desemba, 2019, licha ya Yanga kutangaza kutoa taarifa ya kuachana naye, yeye mwenyewe amesema kuwa bado hajapokea barua rasmi inayoeleza kuwa amefutwa kazi.