Majaliwa: Tumetolewa Afcon ila kuna kitu tumejifunza

Thursday April 25 2019

 

By Fidelis Butahe

Dodoma. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema licha ya Tanzania kutolewa katika Fainali za Afrika (Afcon) kwa vijana chini ya miaka 17 zinazoendelea nchini, kuna mambo mengi tumejifunza.

Majaliwa alisema kitendo cha fainali hizo kufanyika nchini kimetoa fursa katika nyanja mbalimbali, kwamba sasa Tanzania imeanza kuaminika katika mashirikisho mbalimbali ya soka duniani na Afrika, kutokana na sasa kujiandaa kuanda mashindano ya watu wenye ulemavu Afrika Mashariki.

Majaliwa ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Aprili 25, 2019 bungeni jijini Dodoma katika kipindi cha maswali ya hapo kwa papo kwa Waziri Mkuu wakati akijibu swali la mbunge wa Kilolo (CCM), Venance Mwamoto.

Katika swali lake Mwamoto amesema licha ya Tanzania kutolewa katika michuano hiyo ya vijana, sasa inajiandaa kwa mashindano ya watu wenye ulemavu huku akitaka kujua mkakati wa Serikali kuhakikisha Tanzania haitoki kapa katika mashindano hayo kama ilivyokuwa kwa yale ya vijana.

“Tumeanza kuona mwamko wa Watanzania kushiriki michezo mbalimbali, mashirikisho mbalimbali duniani na Afrika wanaendelea kututambua Tanzania na kutupa heshima ya kuendesha mashindano mbalimbali,” amesema Majaliwa.

“Leo nchini yanaendeea mashindano ya vijana chini ya miaka 17 na sisi tumepeleka timu yetu hatujafanya vizuri lakini tumejifunza mambo mengi kupitia mashindano hayo.”

Advertisement

Ameongeza, “Nchi yetu imepata heshima ya kuendesha mashindano ya walemavu ya Afrika Mashariki. Jambo hili ni tunu maana tunaanza kuona mashirikisho ya soka yanatupa hadhi ya kusimamia mashindano yetu maana yake nchi yetu inatambulika au kwa kiusalama na uwezo wa kusimamia mashindano.”

Amesema kuandaa mashindano hayo kumetengeneza fursa ya kuyatumia kwa ajili ya shughuli za uchumi.

“Hii itatufanya tuondoke tulipo na kufikia hatua nzuri ya kuweza kushindana mpaka ngazi ya dunia. Mashindano haya yanayoendelea na haya yanayokuja tutaendelea kujifunza na kuandaa vizuri timu za ndani ili zinaposhindana ziweze kupata kombe,” amesema.

“Serikali tumeanza kusimamia michezo kuanzia shuleni ili tuunde timu za bora za kitaifa na ndio maana tuliruhusu vijana na watanzania kuingia bure uwanjani (michuano ya Afcon) kwa lengo la kujifunza zaidi katika michezo.”

Amewataka Watanzania kupitia mashindano hayo kuongeza fursa za uchumi, kuboresha sekta za utalii sambamba na watoa huduma kupata fursa ya kutoa huduma zao.

Advertisement