Mahakama yatoa onyo la mwisho kwa Wema Sepetu

Muktasari:

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imemuonya msanii wa Filamu nchini, Wema Sepetu (30), kutokukiuka masharti ya dhamana, vinginevyo haitasita kufutia dhamana yake.

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imemuonya mchezafilamu, Wema Sepetu (30), kutokukiuka masharti ya dhamana, vinginevyo haitasita kufutia dhamana yake.
Kauli hiyo imetolewa leo, Juni 24, 2019 na Hakimu Mwandamizi wa mahakama hiyo, Maira Kasonde  wakati akitoa uamuzi kuhusiana na mshtakiwa kukiuka masharti ya dhamana.
Juni 17, 2019 mahakama hiyo iliamuru mshtakiwa huyo kupelekwa rumande hadi leo, ili iweze kutoa uamuzi baada ya mshtakiwa huyo kujisalimisha mahakamani hapo.
Wema alijisalimisha mahakamani hapo Juni 17, 2019 baada ya Mahakama hiyo kutoa hati ya kumkamata mshtakiwa huyo kutokana na kushindwa kufika mahakamani bila kutoa taarifa.
Mahakama ya Kisutu, ilitoa hati ya kumkamata Wema, Juni 11, 2019 baada ya mshtakiwa huyo kuruka dhamana.
"Mahakama inatoa onyo la mwisho kwa mshtakiwa, ikitokea mshtakiwa huyu amevuja sheria kwa kutokufika mahakamani bila taarifa, mahakama hii haitasita kumfutia dhamana, hivyo Mahakama imekurudishia dhamana yako na utakuwa nje kwa dhamana" Hakimu Kasonde wakati akisoma uamuzi wake dhidi ya mshtakiwa huyo.
Wema ambaye alishawahi kuwa Miss Tanzania mwaka 2006, Wema anakabiliwa na moja la kuchapisha video ya ngono na kusambaza katika mtandaoni wa Instagram kinyume cha sheria.
Hakimu Maira ameaihirisha kesi hiyo hadi Julai 4, 2019 itakapoanza kusikilizwa ushahidi.