Mahakama imetoa hati ya Wema kukamatwa

Tuesday June 11 2019

 

By Hadija Jumanne

Dar Es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imetoka hati ya kumkamata msanii wa Filamu nchini, Wema Sepetu (30), baada ya kuruka dhamana.

Wema aliyekuwa Miss Tanzania mwaka 2006, anakabiliwa na shtaka moja la kuchapisha video ya ngono na kusambaza katika mtandaoni ya kijamii wa Istagramu kinyume cha sheria.

Uamuzi huo umetolewa leo na Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama hiyo, Maira Kasonde, baada ya mshtakiwa kushindwa kufika mahakama kusikiliza kesi yake bila taarifa.

Kabla ya kutoa uamuzi huo, wakili wa Serikali, Silyia Mitanto alidia kuwa kesi hiyo ilikuja kwa ajili ya kusikiliza ushahidi lakini mshtakiwa hajamuona mahakamani wala mdhamini wake.

"Hatuna taarifa za mshtakiwa yuko wapi wala mdhamini wake, hivyo tunaomba mahakama itoe hati ya kumkamata mshtakiwa kwa kuruka dhamana" Alidai Mitanto.

Mitanto baada ya kueleza hayo, wakili wa Wema, Ruben Simwanza alidai kuwa mteja wake alikuwepo mahakamani hapo lakini aliugua ghafla tumbo na kuamua kuondoka.

Advertisement

"Mteja wangu alikuwepo mahakamani, lakini kwa bahati mbaya ameugua ghafla na kuamua kuondoka hapa Mahakamani" alidai wakili wa Wema, Simwanza.

Hakimu Kasonde, baada ya kusikiliza maelezo ya pande zote, alisema mahakama yake inatoa hati ya kumkamata mshtakiwa kwa sababu ameshindwa kufika mahakama bila kutoa taarifa.

"Kama amekuja mahakamani alafu akaondoka bila kutoa taarifa, mahakama itajuaje kama alikuja alafu akaondoka?  alishindwa nini kuja kutoa taarifa mahakamani ? Alihoji Hakimu Kasonde.

Baada ya kueleza hayo, Hakimu Kasonde aliahirisha kesi hiyo hadi Julai 4, 2019.itakapoanza kusikilizwa ushahidi.

Katika kesi ya msingi, Wema anadaiwa Oktoba 15, 2018 katika maeneo mbali mbali ya jiji la Dar es Salaam alichapisha video ya ngono na kuisambaza katika mtandaoni wake wa kijamii wa Instagram.

Hata hivyo, siku alivyosomewa maelezo ya awali( PH), Wema alikubali kuwa  yeye anakaa Mbezi Salasala na anamiliki mtandao wa kijamii wa Istagramu wenye jina la Wemasepetu.

Katika maelezo hayo ya awali, Wema alikana kurekodi na kusambaza video ya ngono ambayo haina maudhui kupitia simu yake ya kiganjani.

Alikiri kukamatwa Oktoba 29, 2018 na kupelekwa Kituo Kikuu cha Polisi (Central) kwa ajili ya kuhojiwa.

Pia alikubali kuwa alifikishwa Mahakama ya Kisutu, Novemba Mosi, 2018, kujibu shtaka linalomkabili.

Advertisement