Maguli kiroho safi FC Platinum

STRAIKA wa zamani wa Simba, Elius Maguli anayekipiga katika klabu ya FC Platinum iliyopo Ligi Kuu ya Zimbabwe, amesema amefurahishwa baada ya serikali ya nchini humo kuwaruhusu kuanza kufanya mazoezi ya pamoja.

Serikali ya Zimbabwe ilisimamisha shughuli zote za kimichezo tangu Machi kutokana na janga la covid 19, lakini kuanzia jana timu hiyo ilianza mazoezi ya pamoja baada ya kuruhusiwa.

Akizungumza na Mwanaspoti, Maguli alisema kuruhusiwa kufanya mazoezi ya pamoja kila mmoja wao alijikuta akiwa na furaha kwani ni jambo ambalo kila mmoja alikuwa analisubiria.

“Unajua tumekaa nje kwa muda mrefu sana bila mazoezi ya pamoja, tulikuwa tunafanya mazoezi lakini hatujui ni lini tutacheza soka kwa kweli tuna furaha kuruhusiwa kufanya mazoezi,” alisema Maguli aliyewahi kukipiga pia Prisons, Ruvu Shooting na Stand United.

Maguli alisema awali waliumia kuona miezi inakatika bila kufanya mazoezi ya pamoja, huku wakiwa na jukumu kubwa la kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika.