Maguli : Nachukulia changamoto kama mtaji

Muktasari:

Elias Maguli anaamini changamoto katika soka zinamkomaza kifikra na kufanya anapopata nafasi ya kutumikia timu kazi zake kuwa makini zaidi.

Dar es Salaam. Mshambuliaji Elias Maguli amesema kila msimu aliowahi kucheza umeacha fundisho la maisha yake ya soka akidai changamoto zinakomaza fikra na kubadili mitazamo.

Maguli hakuwa na msimu mzuri ndani ya kikosi cha KMC ambacho hakumaliza nacho mpaka mwisho wa ligi kutokana na kutofautiana na kocha wake Ettien Ndayiragije.

Alisema kwa sasa amepevuka na amejifunza kutokukata tamaa hasa kupambania ndoto ya kile anachokiamini kipo ndani ya uwezo wake katika soka na maisha mengine nje ya hapo.

"Soka haliwezi kukosa changamoto nipo tofauti sana na vile ambavyo nilikuwa naanza kucheza Ligi Kuu Bara mpaka sasa nina uwezo wa kupokea mambo magumu kwa ujasiri na kuendelea na mambo mengine.

"Tangu nilipotoka Oman nimekuwa katika vipindi vya changamoto za hapa na pale ambazo zimejaa mafunzo makubwa ya maisha ya mpira na isitoshe nazichukulia kama mtaji wa kuweka umakini kila ninapokuwa uwanjani.

"Msimu huu umeisha na changamoto zake najiandaa na ujao, najipanga na kufanya maandalizi ya kuhakikisha nafanya kitu bora zaidi," alisema Maguli.