Maguire mjadala mzito Man Utd

MANCHESTER, ENGLAND. BEKI wa zamani wa Manchester United, Rio Ferdinand amemwambia kocha Ole Gunnar Solskjaer: “Mpumzishe Harry Maguire.”

Ferdinand anaamini kwamba Maguire anahitaji kuondoshwa kwenye kikosi kwa ajili ya faida yake baada ya mchezaji huyo kuonekana kuchoka sana kiasi cha kufanya makosa mengi kwenye timu na kuonyeshwa kadi nyekundu alipoitumikia England dhidi ya Denmark.

Ferdinand, 41, alisema: “Ni wazi anapita kwenye nyakati mbaya sana. Hakuna ambaye hawezi kushuka kiwango na kupoteza kujiamini.

“Kama unahitaji kumwona akicheza vizuri, awe mwenye kujiamini basi jambo hilo ni muhimu. Kupumzishwa.”

Ferdinand alisisitiza kwamba kuendelea kucheza soka la kiwango cha hovyo, suala la nahodha huyo wa Man United kulaumiwa halitakwisha, hadi hapo atakapotuliza daruga zake na kurudi kwenye ubora.

“Ishu ya Manchester United, haimhusu tu Harry Maguire. Kuna mambo mengine makubwa,” alisema Rio.

Wakati Rio akitaka Maguire apumzishwe, beki huyo wa kati mwenyewe amemtaka kocha Solskjaer aendelee kumpanga na kila kitu kitakwenda sawa, haya ya sasa ni mapito tu.

Kumekuwa na wito kutoka pande zote zikidai mchezaji huyo awekwe benchi baada ya kuonyesha kiwango cha hovyo kwenye mechi za kimataifa na kuonyeshwa kadi nyekundu.

Man United itasafiri kuwafuata Newcastle United kwenye Ligi Kuu England leo Jumamosi na baada ya hapo watakuwa na shughuli ya kuwafuata Paris Saint-Germain kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Na Maguire anaamini atakwepa vizingiti na kuendelea kukipiga kwenye kikosi hicho cha kocha Solskjaer. Maguire amekiri kwamba hayupo kwenye kiwango bora cha soka, lakini anaamini jambo hilo halitamfanya awekwe benchi.

Beki wa kati Eric Bailly naye alicheza hovyo kwenye kipigo cha mabao 6-1 kutoka kwa Tottenham, huku Victor Lindelof naye akiwa ovyo.