Maguire akamata dili la pesa ndefu

Sunday August 18 2019

 

MANCHESTER, ENGLAND. MWAKA wa Harry Maguire huu. Ndicho unachoweza kusema kuhusu beki huyo wa kati. Kwanza amenasa dili la maana la kwenda kukipiga huko Manchester United na kuweka rekodi ya kuwa beki ghali zaidi duniani.
Lakini, kwa sasa mezani kwake kuna bonge la dili la maana la kuhusu udhamini wa viatu ambao utamwongezea utajiri zaidi. Beki huyo, hakuwa na dili lolote la kuhusu viatu, lakini sasa baada ya kutua Man United tu mambo yameanza kumnyookea.
Kampuni za Nike, Adidas, Puma na Under Armour sasa zinachuana zikitaka kumpatia dili refu beki huyo ambalo litamwingizia mkwanja wa Pauni 700,000 kwa mwaka.
Adidas ndio wanaotengeza jezi za Man United, wamemnasa Dan James, ambaye pia alicheza mechi yake ya kwanza kwenye Ligi Kuu England dhidi ya Chelsea na kufunga kwenye ule ushindi wa 4-0 uwanjani Old Trafford.
Magurie ameripotiwa kugomea ofa ya mshahara wa Pauni 278,000 kwa wiki kutoka Manchester City na kuamua kwenda kukipiga huko Old Trafford, ambapo anacholipwa ni pungufu karibu Pauni 100,000 kwa wiki.
Lakini, beki huyo ametuliza daluga zake kwenye kikosi hicho cha kocha Ole Gunnar Solskjaer na taarifa za kutoka Man United zinafichua: “Ni kiongozi ambaye Man United ilikuwa ikimkosa kwa muda mrefu. Wachezaji wamefurahi sana kutokana na kuwasili kwake. Ameifanya beki kurudi kwenye makali yake, si tu kwa uwezo wake uwanjani, bali kwa maneno yake pia.”

Advertisement