Magori afichua usajili Simba

Muktasari:

Simba inajiandaa kwa mechi ngumu dhidi ya TP Mazembe ya DR Congo hapo Aprili 6, mwaka huu, Uwanja wa Taifa ukiwa ni mchezo wa kwanza hatua ya robo fainali kabla ya kumalizana kule Lubumbashi wiki mbili baadaye.

WAKATI Yanga wakianza harakati za kusuka upya safu yake ya uongozi ili kwenda sambamba na watani zao Wekundu wa Msimbazi, Simba wenyewe wako kwenye mikakati mingine kabisa.

Simba ambao kikosi chake kinaondoka jijini Dar es Salaam leo kwenda Morogoro kwa mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Mbao FC, utakaopigwa keshokutwa Jumapili Uwanjani Jamhuri, wako pia kwenye robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Simba inajiandaa kwa mechi ngumu dhidi ya TP Mazembe ya DR Congo hapo Aprili 6, mwaka huu, Uwanja wa Taifa ukiwa ni mchezo wa kwanza hatua ya robo fainali kabla ya kumalizana kule Lubumbashi wiki mbili baadaye.

Hata hivyo, Simba ambayo inataka kuhakikisha inafanya kweli mwenye michuano yote ikiwa ni pamoja na kutetea ubingwa wake wa Ligi Kuu Bara, ambapo kwa sasa ina pointi 54 ikishika nafasi ya tatu kwenye msimamo huku ikiwa na mechi za viporo mkononi.

Lakini, wakati hayo yakiendelea mabosi wa klabu hiyo wako kwenye harakati za kuimarisha kikosi chake kwa ajili ya msimu ujao wa ligi na michuano ya kimataifa.

Kwa sasa Simba inahusishwa na wachezaji mastaa wa ndani ya nje ya nchi akiwemo Naodha wa Yanga, Ibrahim Ajibu ambaye mkataba wake na wababe hao wa Jangwani ndio inaelekea ukingoni.

Mbali na Ajibu, ambaye aliwahi kuichezea Simba kabla ya kutua Yanga, pia yumo kipa wa Yanga Beno Kakolanya ambaye kwa sasa hayuko kwenye maelewano na viongozi wake na yuko nje ya uwanja kwa miezi kadhaa akisugua benchi.

Habari ambazo Mwanaspoti linazo ni kwamba, Kakolanya anakwenda kuchukua nafasi ya Deogratius Munishi ‘Dida’, ambaye anamaliza mkataba wake mwishoni mwa msimu na huenda asiwe kwenye mipango ya Simba kwa msimu ujao.

Wachezaji wengine ambao inaaminika wanahusishwa na usajili wa Simba ni straika matata wa Zesco ya Zambia, Lazarous Kambole, Jacques Tuyisenge wa Gor Mahia na Obrey Chirwa, ambaye anakipiga Azam FC huku mazungumzo ya kuongeza mkataba mpya yakishindwa kufikia mwafaka.

Tuyisenge, ambaye kwa sasa anaibeba Gor Mahia kweye hatua ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho ndiye alikuwa pacha wa straika wa Simba, Meddie Kagere.

Msikieni Magori

Mwanaspoti limezungumza na Mtendaji Mkuu wa Simba, Crescetius Magori ambaye alisema kwa sasa akili wameielekeza kwenye mambo mawili kwa ajili ya timu.

“Suala la usajili halina mjadala kwa sababu ni lazima tutaimarisha kikosi chetu, lakini kwa sasa tunataka kuhakikisha tunatetea ubingwa wetu wa Ligi Kuu Bara ili kupata tiketi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao.

“Pia, tunakabiliwa na mechi ya robo fainali na TP Mazembe, ambao ni mchezo mgumu na muhimu kwetu kwa sababu, tunataka kufika mbele zaidi na ndio sababu ya tumeegemea hapo zaidi.

“Usajili tutaufanya kulingana na mahitaji baada ya kufanya tathimini ya kikosi chetu kwa sababu mipango ni kufanya vizuri zaidi ya msimu huu,” alisema Magori.

Wakala huyo

Mupenzi Eto ameliambia Mwanaspoti kwa simu kutoka Ubelgiji jana kuwa Tuyisenge hakuja nchini lakini kama Simba wanahitaji huduma ya mshambuliaji huyo wahakikishe mkononi wameshika Dola 150,000 (Sh 345 milioni).

Eto ambaye kwasasa anaishi nchini Ubelgiji alisema kiasi hicho kitatumika kumalizana na klabu yake ya Gor Mahia pamoja na kumlipa mchezaji kutokana na kuwa yupo ndani ya mkataba unaomalizika Februari mwakani.

Hata hivyo Eto alikiri Tuyisenge kuhitaji kuja nchini kuungana na rafiki zake Meddie Kagere na Haruna Niyonzima ingawa klabu ya AS Vita Club kupitia kocha wao, Florent Ibenge anahitaji huduma yake.

Alisema Simba inatakiwa kujiandaa vyema kutokana na kama AS Vita wakimaliza biashara ya kumuuza mshambuliaji wao Makusu Mundele watakuwa na urahisi kulipa kiasi cha Dola 200,000 (Sh 460 milioni).

Bunju Arena kufumuliwa

Simba ilianza ujenzi wa uwanja wa mazoezi uliopo Bunju B nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam, lakini kwa sasa umeanza kuwa pori jipya baada ya ujenzi wake kusimama kwa muda kutokana na nyasi zake kuzuiwa bandarini.Awali, uwanja huo uliokuwa unajengwa na Kampuni ya Masasi Construction Limited, ulitakiwa kukabidhiwa kwa viongozi wa Simba, Februari 15, mwaka huu.

Mwanaspoti hivi karibuni lilitembelea uwanja huo ambao ulifikia hatua ya mwisho ili uwekwe nyasi bandia ndipo taratibu zingine ujenzi ziendelee.

“Ni kweli nyasi zimeruhusiwa na kazi ya ujenzi itaendelea kwa haraka na sasa mkandarasi ndiye anajua itachukuwa muda gani hadi kukamilika japo ni lazima ufumuliwe na kujengwa upya,” alisema.