Magori: Chama haondoki Simba

CRESCENTIUS Magori amewashangaa watu wanaomhusisha kiungo, Clatous Chama kuondoka kwenye timu hiyo akieleza kuwa wangeonekana wajinga kama wasingemuongezea mkataba mchezaji huyo raia wa Zambia.

Magori aliyewahi kuwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba (CEO) ambaye sasa ni mshauri wa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Simba, Mohammed Dewji 'Mo Dewji' ameiambia Mwanaspoti Online leo Jumanne, Agosti 11, 2020 kuwa uvumi wa kwamba Chama ataondoka si kweli.

"Tungeonekana wajinga kwamba tunahangaika kufanya usajili wa wachezaji wapya, halafu Chama hatujampa mkataba, yule ni mchezaji wetu bado tena kwa miaka mingi tu," amesema Magori bila kueleza wamemuongezea mchezaji huyo mkataba wa miaka mingapi.

Akizungumzia hatma ya kocha mkuu, Sven Vandenbroeck ambaye hivi karibuni alihusishwa kupewa mkono wa kwaheri, Magoro amesema kocha huyo ataendelea kukinoa kikosi cha Simba msimu ujao.

"Bado ni kocha wetu na hivi karibuni atarejea kuendelea na majukumu yake, ana mkataba wa miaka miwili na Simba," amesema.

Kuhusu mchakato wa kupata CEO mwingine kuziba nafasi ya Senzo Mazingisa aliyejiuzulu nafasi hiyo juzi Jumapili na kutua Yanga, Magori amesema kuondoka kwake hakujazuia kazi kufanyika.

"Wako wakuu wa vitengo mbalimbali, Simba sasa ni taasisi, hivyo majukumu yanaendelea kama kawaida wakati Bodi ikijipanga kuajili CEO mwingine," amesema.