Magori : Sababu hizi zilitung'oa mabingwa

Muktasari:

Ilikuwa ni kama bahati mbaya kutolewa hatua ya kwanza, najua wanachama wetu na mashabiki iliwasikitisha sana mmoja wapo ni MO. Aliumia sana kwasababu ni kitu ambacho hakukitarajia Simba ingetolewa mapema kiasi kile.

KATIKA toleo la jana Alhamisi tuliona jinsi Crescentius Magori akielezea jinsi ya mfumo wa usajili ulivyofanyika na sasa anajibu jinsi ulivyofanikiwa au ulifeli.

“Binafsi naamini mwaka huu Simba katika Ligi ya Mabingwa Afrika ilikuwa bahati mbaya kutolewa na hii ni kwasababu ratiba ya msimu huu ilianza mapema sana timu haikuwa imecheza.

“Hadi tunakutana na UD Songo wenzetu walishacheza mechi saba za ligi, sisi hatucheza hata moja bahati mbaya washambuliaji wetu wengine watatu walikuwa wameumia.

“Bocco (John), Wilker (Da Silva) na Ajibu (Ibrahim) walikuwa wameumia, tukabakia na Kagere (Meddie) katika mchezo wa hapa nyumbani. Bocco aliumia katika mchezo wa Msumbiji. Nafikiri hapo ndipo tulipokwama, kama tungekuwa na mshambuliaji mwingine katika eneo lao la hatari tungewafunga tu.

“Hili lilitugharimu, kubaki na Kagere na presha ile kwasababu mpira ulikuwa hautoki kwao hasa ule muda wa mwisho hali ilivyokuwa kina Deo Kanda wanavyoingiza mipira kila wakati sasa kama tungekuwa na Bocco na Kagere tu kwenye kupishana pale wangefungwa tu, kwahiyo kuna mambo yakitokea unakubali ukweli wenyewe.

Ilikuwa ni kama bahati mbaya kutolewa hatua ya kwanza, najua wanachama wetu na mashabiki iliwasikitisha sana mmoja wapo ni MO. Aliumia sana kwasababu ni kitu ambacho hakukitarajia Simba ingetolewa mapema kiasi kile.

“Hakuna mtu aliyetarajia. Unajua Simba haifuatiliwi na watu wa hapa nyumbani pekee, kuna watu wa nje huko walishtushwa na hilo lakini inatokea katika soka na sio kwa Simba tu. Tutajipanga kutoka hapa tulipo na pengine watu wanasema ni mbaya lakini ina faida ndani yake, nafikiri ni vizuri kwa Simba kujipanga zaidi kwa msimu ujao.

Kipi kifanyike

“Ushauri wangu kama kuna usajili Simba inataka ufanyike kulingana na ratiba ya sasa hivi ya Caf ni bo ra wa ngesajiliwa katika Desemba hii wakati wa usajili wa dirisha dogo na sio wakati wa dirisha kubwa. Mpaka kufika Desemba wakati dirisha linafunguliwa uchambuzi wa timu uwe umeshafanyika kama kuna mwanya kama kuna mabadiliko, kama kuna wachezaji wapya wanatakiwa kuingizwa lifanyike wakati huu.”

MO alikwama vipi Caf?

Wakati Simba ilipopata vipigo vikubwa katika mechi za ugenini msimu uliopita wa Ligi ya Mabingwa Afrika MO alitoa ahadi ya kikosi chake kusajili wachezaji waliotoka katika Ligi ya Mabingwa Afrika na hata Kombe la Shirikisho ili kushindana na klabu kubwa za Afrika hapa Magori anaeleza kilichokwamisha usajili huo.

“Kuna wachezaji tuliwataka, tatizo walikuwa na mikataba mirefu na klabu zao. Ilikuwa ukimfuata mchezaji mwenye mkataba ambaye tulidhani ni sahihi kuja Simba klabu yake inakwambia ada ya usajili tu Dola 30,0000(Sh 684 ml) hiyo ni klabu yake yeye anakwambia anataka Dola 150,000 (Sh 342 ml).

“Tulilikataa hilo, unajua hii klabu haiwezi kuruka hatua za kukua kwake, yaani Simba hata kama mwekezaji anataka kufanya hilo hatuwezi kukubaliana nalo.

Simba haiwezi kusajili mchezaji wa Dola 450,000 (Sh 1.02 bil) kisha ukishamsajilihapa nyumbani kuna mchezaji unamlipa Sh 3 milioni huyo mchezaji wa Dola 450,000 atakwambia anataka mshahara wa Dola 12000 (Sh 27.3 ml), unawezaje kutengeneza timu kwa akili hiyo?

“Hait awezekana kwasababu klabu kama Simba lazima ijiendeshe kama klabu. Nilikuwa nasema kila siku isifikie hatua Simba ikawa inasimama kwasababu ya MO.

“Ukishaleta bei za wachezaji za namna hiyo inawezekana ukawa unafanya kwasababu MO yupo. Unajua Simba haiwezi kuruka katika hatua za maendeleo, yale mafanikio ya kufika hatua ya robo fainali mwaka jana katika Ligi ya Mabingwa Afrika ni kama Simba iliruka. “Hata sisi tulijua pale atavuka Al Ahly na AS Vita. Vita ilitoka kucheza fainali ya Afrika msimu uliotangulia na Ahly nayo ilikuwa kama hivyo lakini Simba ilipenya, lakini haiondoi ukweli kwamba Simba inatakiwa kukua katika mfumo sahihi. Vitu vyote lazima viende sambamba na ndiyo maana ule mkataba wa kadi mpya na idadi ya mashabiki niliupigania sana na katika mambo ambayo naongea na MO kila wakati ni hilo huwa namsumbua kwa kumuuliza limefikia wapi hili?

“Simba lazima iwe na matawi, kuwe na uongozi wa wilaya, uongozi wa mkoa, Simba iwe na msingi wa mashabiki wake, huko ndiko kuna pesa,huwezi kufanya hivyo bila kuwa na taasisi. Tukiwapata watu wa Equit hili litasaidia hata akija mdhamini tunamwambia tuna mashabiki 1.2 milioni atauliza wako wapi unamuonyesha hilo la kwanza. La pili hili litasaidia hata katika biashara ya vifaa kama jezi unauliza tu nani anataka jezi kila kitu kinaonekana yuko mkoa fulani tawi fulani, anaweka pesa unafanya biashara.

“Kwahiyo tangu Aprili unajua labda una watu laki sita wameshalipa 20,000 kila mmoja ya kununua jezi, unaokuja hiyo ni kama 1.2 bilioni hapo kuna kofia kuna kila kitu unatumiwa moja kwa moja huko ulipo hiyo ndio njia ya kutengeneza pesa kwa klabu. Hata akija mdhamini unamuonyesa tu mashabiki ninao, unafanikiwa kumbana vizuri kwahiyo hili ni lazima lifanyike na hapo ndio sasa Simba itaanza kupiga hatua. Itaendelea Jumamosi.