Magori : Bila MO Simba haiendi, mishahara tu ni 270 milioni

Muktasari:

Katika mfululizo wa maka ha haya bosi huyo amefunguka mambo mengi ndani ya klabu hiyo na katika soka la Tanzania kwa ujumla hasa ikizingatiwa amewahi pia kuwa Makamu wa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) katika utawala wa Rais, Leodgar Tenga.

BAADA ya Simba kuingia katika mchakato wa mabadiliko kwenye Ukumbi wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam Novemba 15, 2018 na wanachama kubariki mfumo huo unaokwenda kuipa sura mpya klabu yao aliyekuwa Kaimu Mwenyekiti, Salim Abdallah ‘Try Again’ hapohapo alimtangaza mtendaji mkuu wa klabu hiyo.

Try Again alimtangaza Crescentius Magori kuwa mtendaji mkuu wa klabu hiyo ambaye alidumu katia kiti hicho kwa takribani miezi minane kabla ya kumaliza muda wake na kupatikana mrithi wake, Senzo Mazingisa aliyetambulishwa Septemba 7, 2019.

Baada ya Magori kuachia ngazi Mwanaspoti lilimtafuta na kufanya mahojiano naye maalumu kutaka kujua miezi minane yake kama mtendaji ilikuaje.

Katika mfululizo wa maka ha haya bosi huyo amefunguka mambo mengi ndani ya klabu hiyo na katika soka la Tanzania kwa ujumla hasa ikizingatiwa amewahi pia kuwa Makamu wa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) katika utawala wa Rais, Leodgar Tenga.

Hali ya Simba kwasasa ikoje

Magori anasema Simba inaenda vizuri na baada ya muda itasimama kwenye mstari imara.

“Simba iko pazuri, hali ya Simba naiona iko sawa nafikiri kilichobaki ni kukamilisha mchakato wa mabadiliko, ndiyo changamoto pekee ambayo ipo sasa ndani ya klabu yetu kwa maana iwe ile kitu tunayoita Simba Sports Club Company Limited, lazima ikamilike kwa maana ya kwamba mali na madeni vihamishwe kuingia katika kampuni kutoka katika klabu na baada ya hapo sasa itakuwa kampuni halisi na mengine ambayo yanazungumzwa sasa kwa maana pesa haijawekwa sasa ndiyo utakuja wakati wake.

“Unajua kama haijakamilika ile ina maana haijawa kampuni kamili. Lakini mpaka sasa kampuni imeshasajiliwa serikalini (BRELA) lakini mchakato lazima ukamilike kwa kuhamisha hizo mali na madeni kutoka katika klabu

“Nafikiri mpaka sasa tupo katika asilimia 80% kuweza kukamilisha kwasababu jukumu kubwa lilikuwa wanachama kuridhia ambalo lilishafanyika na serikali kuridhia kwa maana ya kusajili katiba nalo limeshafanyika, sasa haya mengine ni michakato tu mfano ni kutafutwa kwa hati ile ya Bunju ilishapatikana, ile moja ya jengo nayo ilishapatikana na ile nyingine ilibidi itafutwe kwa kuwa ilikuwa haionekani, Mzee (Hamis Kolomoni) alikuwa anasema mara ipo mara haipo sasa ikabidi itafutwe kwa njia ya kiserikali na sasa imeshapatikana ingawa kuna taratibu nyingine za kiserikali zilikuwa lazima zifanyike ili kuweza kukamilisha mambo.

“Kuna kamati maalumu ambayo bodi iliiteua kwa ajili ya kufuatilia hilo naamini wakimaliza kila kitu kitakuwa sawa na Simba itabadilika. Naona hayo yote yakikamilika nafikiri klabu yetu itakuwa ya mfano kwa klabu nyingine kuiga kwasababu tatizo la klabu hizi kubwa kama Simba ni uimara ndiyo tatizo sana pamoja na mwendelezo. Ukiwa na klabu inayokosa hayo itayumba sana, leo unakuwa na Mwenyekiti Magori anatawala kwa miaka minne anafanya mambo A, B, C, D lakini kesho unakuja kufanyika uchaguzi anakuja kugombea mfano mtu kama Naheka anakuja na mtazamo tofauti kabisa na ule wa aliyemtangulia inaibuka migogoro vurugu kwahiyo hata kuweza kuvutia kipato na wadhamini inakuwa kazi ngumu.

“Leo Simba tunajua Mwenyekiti wa Bodi ya Simba ni Mohamed Dewji ‘MO’ kwasababu amewekeza hisa asilimia 49, mtafanya uchaguzi wa wajumbe wa bodi, kwahiyo mtu akifikiria kuja kufanya kazi na Simba ataanza kufikiri na kujiuliza uongozi wa Simba una maono ya mbali? Atamuona MO, hata wanachama wa kawaida kama huyu mfanyabiashara amefanikiwa katika biashara zake ni wazi akiwa mwenyekiti wa bodi ya Simba ambayo ndiye atakuwa anaiongoza Simba uwezekano mkubwa ni kwamba klabu itafanikiwa.”

Mo anapata wapi nguvu?

“Cha kwanza MO ataweka pesa zake katika hisa hizo, lakini cha pili kwa mfano sisi wanachama wengine tuko 7,000 sisi wenye hisa 51, swali ambalo watu wanatakiwa kujiuliza je, tukimteua mmoja wetu pale atakuwa na asilimia ngapi? Watu wanachotakiwa kutambua yale maumivu ya fedha. Mimi Magori ni mmoja wapo wa wanachama wa Simba leo ndio nakuwa mwenyekiti wa bodi ya Simba, hivi klabu ikiyumba nitakuwa nimepoteza nini? MO yeye mtu mmoja kampuni yake moja amewekeza hisa asilimia 49 lakini sisi wenye 51% tumeweka ngapi? Kwanza tumepewa bure hisa 10% hatujaweka chochote kisha tuangalie hizo zilizobaki 41 tutazitafuta vipi labda tunaweza kusema kila mwaka tuchangie sh 10, 000 kila mmoja ili tuwe tunaziendeleza sasa ule uchungu atausikia yule aliyeweka fedha zake sio mimi ambaye sijaweka chochote.

“Huko Mbele ya safari inaweza kutokea kwa mfano wanachama tukaamua labda katika hizo hisa 41 tuiuzie kampuni kama Vodacom hisa 10 labda tunaweza kuangalia pia tuiuzie Azam hisa 10, nafasi inakuwa hakuna atakayemkalibia kwa wingi wa hisa MO, kwahiyo ninachojaribu kusema ni kwamba MO iwe unapenda au hupendi yeye kama mtu mmoja anahisa nyingi na sisi kwa wingi wetu ndio tuna hizo hisa 51 na ilikuwa ni busara wakati wanachama wanapitisha ile huyu mwenye 49% ni bora awe mwenyekiti kwasababu yeye peke yake ana 49% uchungu atakaoupata ni tofauti na sisi wenye 51% za maneno na kati ya hizo 10% tumepewa bure hizi nyingine inabidi tutafute tutazijaziaje, kwahiyo kiuhalisia sasahivi MO ana 49 na sisi wanachama tuna 10 na hizo 41 zinazobaki ni zetu lakini hatujui tutakuja kuzijaza vipi lakini jambo zuri ni kwamba yule mwenye 49% hataweza kuja kumiliki zaidi mwingine yoyote atakayekuja atamiliki chini ya hapo na MO hawezi kutoka kule kuja huku.

Simba nikweli ina thamani ya 20 bilioni?

“Imezidi kwanza, Simba haina thamani ya 20 bilioni, hesabu hizo inamaana Simba ina thamani ya 40 bilioni kwasababu tunaposema Sh 20 bilioni kwa asilimia 49, Simba haina thamani hiyo, Simba sanasana sidhani kama inafika thamani ya bilioni saba. Kuna haja ya watu kusoma jinsi klabu inavyolinganishwa kithamani, ukiwa unapiga hesabu za namna hiyo utaangalia labda majengo ya pale ya Msimbazi, utaangalia eneo la Bunju, wachezaji na baada ya hapo labda utaangalia madeni ukimaliza hapo jumlisha vyote Simba haiwezi kufika hata bilioni saba.

“Hiki kiasi ambacho MO ameweka ni kikubwa sana halafu kuna watu wanapiga kelele hii ni pesa ndogo hakuna hiyo. Ukweli ni kwamba Simba kwanza inabahati sana hakuna mtu anayeweza kuja kuinunua Simba hii kwa kiasi cha Dola 18 milioni.

“Wako wengine wanasema Simba ina wanachama wengi na mashabiki wako wapi? Si maneno tu mfano halisi Yanga hapa wamechangisha wanachama wao hapa karibuni wamepata kiasi gani? Katika taarifa za idadi ya wanachama wako wangapi? Mpaka sasa katika leja yetu unaweza kukuta kuna wanachama sijui 7,000 na hapo unaweza kukuta wako wengine ni marehemu, mikutano yetu mikuu hakuna mkutano umewahi kuvuka wanachama 2,000 waliohudhuria hakuna, kwahiyo maneno yako mengi kuliko uhalisia.”

Nguvu ya Mwenyekiti

Magori anaendelea kuelezea mambo ya ndani ya klabu hiyo ambapo sasa anajibu madai ya kwamba kwasasa nguvu ya mwenyekiti wa klabu hiyo haipo. Bosi huyo mwenye msimamo anaelezea: “Sio kweli kwamba katiba imepoka nguvu ya mwenyekiti wa klabu kilichopo ni mwenyekiti wa klabu na wajumbe wakewaliochaguliwa ni wajumbe wa bodi. Kwa hiyo maamuzi yote makubwa ya klabu yanafanyika kwenye bodi na mwenyekiti anaingia na wajumbe wa kuchaguliwa na pia anachagua wengine wawili ili kuja kuiwakilisha katika asilimia 51 sasa hapo madaraka gani yamepokonywa.

“Unajua hapa tatizo ninaloliona bado kuna watu wana uchovu wa mfumo ule wa zamani kuwa mwenyekiti anatakiwa kukutana na kamati ya utendaji nadhani bado watu wako huko. Simba ilishatoka huko leo mimi nipo madarakani kama mtendaji zinaweza kupita hata wiki mbili tatu hatujaongea mambo ya Simba tunaongea mambo yetu mengine kabisa. Timu inakwenda na mimi naweza kufikisha hata siku tatu mambo yanaendeshwa na meneja wa timu. Nishampa fedha za wiki nzima ya mazoezi ya kila kitu posho zote, safari zinajulikana Simba itaondoka vipi itakaa wapi kuna mratibu Bwana Abbas (Ally) mambo yanakwenda. Kuna mpishi anajua majukumu yake mimi sihitaji kuwa huko sana na mambo yanakwenda. Muhimu ni ripoti kila baada ya muda kujua mambo yanavyokwenda kma kuna sababu ya kufanya malipo yanafanyika mapema kila kitu kinakwenda sasa hapo mwenyekiti wa klabu ana kazi gani?

Vikao vya bodi hali ya majadiliano huwa ikoje?

“Tunapokuwa katika vikao mambo mambo huwa yanakwenda vizuri sana. Majadiliano yote huwa yanafanyika kwa maslahi ya Simba na niseme wale wajumbe wa kutoka kwa wanachama na hata wale wa mwekezaji wote wanakuwa na ushiriki mzuri na pia niseme kuna zana kwamba wajumbe hawa wa bodi ya Simba wanaotoka upande wa wanachama hawaji pale kusema wanakuja kupambana na upande wa mwekezaji na ajenda ya Simba ni moja.

“Jambo zuri zaidi ni kama bahati huyu mwekezaji naye ni Simba damu kama ambavyo tenda ilihitaji kuwa kwa mwanachama wa Simba mwenye uwezo wa kuwekeza. Tatizo ninaloliona kuna watu wana mgongano binafsi na mtu mwingine sasa hilo ndiyo linalokuja kuletwa Simba.”

Vipi Mo hataweza kuja kuibeba Simba yote

Baada ya kueleza hilo Magori sasa anaondoa mashaka ya kwamba kupitia uwekezaji wa MO ndani ya Simba iko siku anaweza kuja kuichukua Simba na kuwa klabu yake binafsi hapa anaeleza: “Kwa jinsi muuondo ulivyotengenezwa hilo halitawezekana. Klabu ni ya wanachama, MO hawezi kufanya hivyo kwasababu kwa jinsi bodi ilivyoundwa hawezi kufanya maamuzi hayo, wanaweza kukubali wale wajumbe wake lakini wengine wa upande wa wanachama watakubali vipi?

Kuna wakati

MO alitaka kukata tamaa ya kuwekeza Simba?

“Unajua MO naye ni binadamu kwanza kitu kimoja ambacho watu wengi hawajakijua siku MO alivyotamka ile 20 bilioni aliitamka kama utani.

Baadaye akaona watu wameliweka lile vichwani mwaka akagundua kwamba alitamka kiasi kikubwa sana.

“Kwakuwa alishatamka hakuwa na namna, sasa kuna wakati anatoa fedha katika majukumu mbalimbali ya uendeshaji wa klabu alafu huku anasikia kama kuna watu wanampiga vita huwa anauliza hivi wanachama hawakumbuki hapa katikati tabu ambayo Simba ilipata?

“Hiki ninachofanya hawaoni chochote lakini cha ajabu watu ambao hawachangii chochote katika timu kwa kutoa fedha zao mfukoni wao ndio wanajifanya wana uchungu na hii timu.

“Hiki ndio kitu cha ajabu sana katika mpira wa Tanzania yaani ukiona mtu anapiga kelele sana muulize hivi huwa unachangia shilingi ngapi au mara ya mwisho amechangia lini na shilingi ngapi?

“Kuna wakati hapa nyuma tulikuwa tunachanga sh 3 milioni za usajili watu wanaona kama kitu rahisi. Unajua sisi tunaotoa fedha zetu kuna wakati tunajiuliza hivi MO akiondoka leo hali itakuaje? Tutaumiza vichwa kwa kiasi gani? Sisi tuotoa fedha zetu lakini pia tukiwa na ugonjwa na Simba tunajua tabu hiyo sasa yule asiyechangia chochote anaona kawaida tu. Hakuna anayetaka mafanikio ya Simba alafu akakataa uwekezaji huu ambao Simba imeingia.”

Utoaji wa pesa kwa MO ndani ya Simba ukoje

“MO amepunguza sana adha ndani ya Simba kwa kiasi kikubwa sana. Kuna fedha ambazo awali alikuwa anazikopesha lakini pia kuna fedha ambazo alikuwa anazitoa kama mchango wake. Mfano sasa hivi ameamua kwamba badala ya zile fedha ambazo alikuwan anazitoa kama deni ameachana na mambo ya kudai na amesamehe.

“Sasa bila kufanya hivyo lazima Simba ingekuwa na madeni angalia sasa mishahara tu ya klabu ni mikubwa ukiongelea mishahara tu Simba inahitaji kiasi cha Sh 270 milioni kwa mwezi. Kwa vyanzo vya mapato ya Simba hiyo pesa ingetoka wapi bila ya MO?

“Mwisho wa siku mtazunguka mtaweka bajeti lakini kuna wakati mnakwama inabidi mrudi kwa mwenyekiti wa bodi kujiuliza hapa tunafanyaje? Anaweka nguvu yake mambo yanaendelea.

Lakini sasa tunataka Simba itoke hapa na tuna mipango mingi tu tunachotaka ijiendeshe kama klabu. Tunataka kufanya kama Ulaya kwamba timu ijiendeshe na kile inachoingiza kimapato sio kila siku mwenye timu anaingiza fedha zake kutoka nje. Huku Afrika bado sheria ya financial fair play haikafika lakini huko mbele itafika maana Ulaya tayari sheria hii inatumika sasa,” anafafanua Magori.

Itaendelea Alhamisi ambapo Magori atafichua mambo mazito zaidi.