Magari, mamilioni ya pesa kwa Serengeti Boys hatihati

Muktasari:

  • Hii ni baada ya kupoteza mechi zao mbili kwenye fainali za AFCON zinazoendelea jijini Dar es Salaam

Dar es Salaam. Ahadi ya magari na mamilioni ya pesa kwa Serengeti Boys, kutoka kwa mlezi wa Serengeti Boys, Reginald Mengi vinaelekea kufutika kwa vijana kutokana na kutofanya vyema mechi zake mbili walizocheza.

Hii ni baada ya kupoteza mechi zao mbili kwenye fainali za AFCON zinazoendelea jijini Dar es Salaam.

Timu hiyo ya vijana hadi sasa wamefungwa na Nigeria 5-4 na Uganda 3-0.

Mengi alionyesha uzalendo kwa timu hiyo na kuwaahidi wachezaji wa Serengeti Boys magari pamoja na pesa kwa wachezaji iwapo watafanya vizuri kwenye fainali hizo.

Mengi aliahidi gari kwa kila mchezaji wa Serengeti Boys kama watafuzu fainali za dunia ambazo zitafanyika nchini Brazil mwishoni mwa mwaka huu.

Mbali na magari hayo, vijana hao waliahidiwa kupewa shilingi milioni 20.

Kabla ya mchezo wao wa jana dhidi ya Uganda wachezaji wa Segerengeti Boys walisikika wakisikitikia magari hayo na pesa.

 "Kweli hatuna bahati yaani tunakosa magari na pesa zote hizo inauma sana. Sijui ngoja tuombe Mungu," alisikika mmoja wa wachezaji hao.

Mashindano hayo ya vijana chini ya miaka 17 AFCON yanayoendelea nchini Tanzania katika viwanja viwili jijini Dar es Salaam vya Chamazi na Taifa.