Maganga, Kibaya ndio wanaotamba

Muktasari:

Wachezaji wawili Fully Maganga (Ruvu) na Jaffar Kibaya (Mtibwa Sugar), walibadili upepo wa hali ya hewa kwa mashabiki wa Simba na Azam, kuwa wanyonge baada ya timu hizo kufungwa na nyota hao.

NI wachezaji wawili wa timu tofauti Jafari Kibaya (Mtibwa Sugar), aliyepunguza kasi ya Azam FC na Fully Maganga (Ruvu Shooting) aliyezima kelele za mashabiki wa Simba jijini Dar es Salaam.

Kibaya ndiye aliyeifunga Azam FC, Uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro, hivyo aliipunguza kasi ya kuendelea kujiimalisha zaidi kileleni, ambapo imebaki na pointi zile zile 21, huku Yanga ikiwa na pointi 19, imecheza mechi saba ikishinda mchezo wa nane itapanda kileleni.

Huu ni ushindi wa pili mfululizo kwa Mtibwa Sugar tangu aondoke aliyekuwa kocha wao, Zuber Katwila anayeinoa Ihefu kwasasa, kwani katika mechi nane wameshinda tatu, sare mbili, walifungwa michezo mitatu hivyo ipo nafasi ya 10 na pointi 11.  

Kibaya ameliambia Mwanaspoti Online, jana Jumanne Oktoba 27, 2020 kwamba  amejisikia faraja kufunga bao lililoiongezea timu yake pointi kutoka  ane mpaka 11, ambazo zinawasaidia kuendelea kupanda nafasi za juu kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara.

"Ushindi huo ni ushirikiano wetu wote, kwani tunahitaji kupambana zaidi ili kuhakikisha tunasonga mbele, ligi ni ngumu bila jitihada tunaweza tukajikuta pabaya,"amesema.

Beki wa timu hiyo, Dickson Job amesema ushindi huo umewapa ari ya kuendelea kupambana kupata pointi tatu katika mechi zinazoendelea, ili msimu huu waweze kuumaliza kishujaa, tofauti na uliopita ambao walikuwa wanapambana kujikwamua na kushuka daraja.

"Azam FC sio timu mbaya, ina wachezaji ambao wanajua kupambana, lakini tunashukuru Mungu bahati ilikuwa kwetu kupata ushindi ambao umetusogeza hatua moja mbele," amesema.

Bao la Maganga wa Ruvu, limewanyima raha mashabiki wa Simba kukaa kimya, baada ya jana kuzitikisa nyavu alizokuwa amesimama kipa Beno Kakolanya.

Maganga amelizungumzia bao hilo kwamba, limetokana  na umakini wa hali ya juu, ambao waliambiwa na kocha wao Boniface Mkwasa kabla ya mechi, jambo lililowazalia  matunda.

"Kocha Mkwasa alitupa mbinu kwamba Simba ingetuchukulia poa, hivyo alitutaka tuingie na ari ya kupambana na kutojiona wanyonge licha ya timu yao kuwa nzuri, hiyo ndio siri ya mafanikio yetu ya kuwafunga,"


"Kipindi cha kwanza tuliamua kumaliza mchezo, hivyo kipindi cha pili Simba ikawa na wakati mgumu wa kupambana kukomboa bao, ingawa shukrani zimuendee kocha wetu Mkwasa ambaye alitupa mbinu hizo," amesema Maganga.