Mafundi wa mpira wanasubiri kuvaa buti za Hazard Chelsea

Saturday February 9 2019

 

LONDON, ENGLAND

KUNA asilimia ndogo sana ya kumshuhudia Eden Hazard akiendelea kubaki kwenye kikosi cha Chelsea baada ya msimu huu kumalizika. Hakika hilo haliwezi kuwa habari njema kabisa kwa mashabiki wa timu hiyo kwa sababu ni jambo la wazi, ndoto za Hazard kwa sasa ni kwenda Real Madrid.

Hakuna ubishi, Hazard akiondoka ataacha pengo kubwa sana huko Stamford Bridge ambalo bila ya shaka, The Blues watahitaji kutuliza akili katika kumsaka walau mtu mwenye uwezo wa kuliziba au kuwapunguzia makali ya kumpoteza mchezaji mkubwa kabisa kama itatokea hivyo.

Hawa hapa mastaa ambao wanaweza kuwafanya mashabiki wa Chelsea kumsahau Hazard kwa muda mfupi tu kama watawanasa baada ya supastaa huyo wa Kibelgiji kuondoka kwenye kikosi chao.

Nabil Fekir (Lyon)

Hili ni jina ambalo limekuwa likihusishwa mara kwa mara na Ligi Kuu England. Staa huyo wa Kifaransa, Nabil Fekir alishindwa kiduchu tu kujiunga na Liverpool katika dirisha la uhamisho wa majira ya kiangazi huko Ulaya mwaka jana kabla ya sasa jina lake kuendelea kuhusishwa na klabu za England. Chelsea kwa sasa inapiga hesabu za kumpata mtu atakayekuja kuwasahaulisha kuhusu Hazard kama ataondoka na Fekir anadaiwa kwamba anaweza kuwa ni mtu huyo wanayemsaka. Fekir ameendelea kuonyesha makali yake kwenye Ligi Kuu Ufaransa msimu huu akifunga mabao saba katika mechi 17 alizocheza. Uzuri wa Fekir ni kwamba ni kiraka, anaweza kucheza kwenye eneo lolote lile katika zile nafasi tatu za ushambuliaji, lakini pia anaweza kucheza kama kiungo wa kati jambo litakalomfanya kocha Maurizio Sarri kuwa ma machaguo mengi kwa kuwa na huduma yake kwenye kikosi. Shida ya Fekir pia ni majeruhi yake ya mara kwa mara na hivyo ndicho kilichowabadili mawazo Liverpool.

Marco Reus (Borussia Dortmund)

Marco Reus kwa sasa anafurahia kiwango chake bora kabisa kwenye kikosi cha Borussia Dortmund baada ya kuteswa sana na majeruhi yaliyotishia uwezekano wa staa huyo wa Kijerumani kustaafu soka mapema. Nyota huyo yupo kwenye kiwango cha ubora wake msimu huu ambapo kwenye Bundesliga ameshafunga mabao 13 na kuasisti mara sita kuifanya Dortmund kutamba kwenye kilele cha msimamo wa ligi ya Bundesliga. Uwezo wa Reus ni kucheza upande wowote ule wa pembeni iwe kushoto au kulia na pia anaweza kucheza kama mshambuliaji wa kati kitu ambacho atakuwa mrithi sahihi kabisa wa Hazard kwenye kikosi hicho cha Stamford Bridge. Shida pekee inayosumbua kwa mchezaji huyo ni kitendo cha kuwa majeruhi mara kwa mara huku umri wake pia akielekea kuikaribia miaka 30.

Lorenzo Insigne (Napoli)

Chaguo jingine ambalo linaweza kuwa mwafaka katika kupata mrithi wa Hazard basi linaweza kuwa Lorenzo Insigne. Staa huyo mwenye kimo cha futi 5 na inchi 4, siku za karibuni alihusishwa na mpango wa kwenda kujiunga na Liverpool huku kocha Jurgen Klopp akidai kwamba anavutiwa sana na kipaji cha mchezaji huyo. Hata hivyo, Chelsea hapo wanaweza kuwa na nafasi kubwa ya kumnasa mchezaji huyo kwa sababu ya kocha wao Maurizio Sarri kufahamiana vyema na Insigne baada ya kuwa pamoja huko Napoli kabla ya bosi huyo kwenda zake Stamford Bridge. Insigne amekuwa akicheza upande wa kushoto na Sarri alitamba naye sana msimu uliopita wakati alipofunga mabao manane na kuasisti mara 11. Kama Chelsea watamchukua moja kwa moja Gonzalo Higuain na kisha wakamsajili Insigne, basi ile ‘Sarri-Ball’ itakuwa imekamilika huko Stamford Bridge baada ya uwepo pia wa Jorginho.

Hirving Lozano (PSV Eindhoven)

Hirving Lozano ni jina jingine matata kabisa kwenye soka linalohusishwa na mpango wa kutua kwenye Ligi Kuu England, huku Chelsea wakionyesha dhamira ya dhati ya kunasa huduma ya staa huyo wa Mexico tangu Desemba mwaka jana. Fowadi huyo alionyesha kiwango bora kabisa kwenye fainali za Kombe la Dunia 2018 na ubora wake huo ameendelea kuuonyesha huko kwenye Ligi Kuu Uholanzi akiwa na kikosi cha PSV msimu huu. Nashika namba tatu katika chati ya wanaongoza kwa mabao kwenye ligi ya Uholanzi (Eredivisie) huku akiwa na asisti sita pia zinazomfanya awe kinara kwenye upande huo wa kupiga pasi matata za mabao. Lozano alishaweka wazi kwamba mpango wake ni kuhamia kwenye Ligi Kuu England.

Philippe Coutinho (Barcelona)

Mbrazili, Philippe Coutinho ni mchezaji mwingine ambaye mabosi wa Chelsea wanaweza kwenda kuisumbukia saini yake kuja kumrithi Hazard huko Stamford Bridge. Staa huyo mambo yake huko Barcelona kwa sasa si shwari, hivyo kama Chelsea watakuwa siriazi kwenye mipango yao ya kutaka huduma yake bila shaka wataipata. Tangu atue Barcelona, Coutinho ameshindwa kucheza kwa ubora ule aliokuwa nao Liverpool, hivyo jambo hilo limemfanya aanze kuripotiwa kwamba huenda maisha ya Nou Camp yamemshinda na ataondoke mwishoni mwa msimu. Ripoti za hivi karibuni zimedai kwamba Chelsea wameibukia kwenye mpango wa kumsajili Coutinho kama Hazard ataondoka zake.

Advertisement