Mafundi wa mpira waliotua Ligi Kuu England jioni kabisaa

Muktasari:

Lakini kuna baadhi ya wanasoka hao matata, walitua kwenye ligi hiyo tayari miaka ikiwa imewatupa mkono. Wametua kwenye Ligi Kuu England katika umri wa kizee kwenye soka.

LONDON, ENGLAND. MASHABIKI wa soka wa Ligi Kuu England wamekuwa na bahati ya kushuhudia wanasoka bora kabisa duniani wakikipiga kwenye ligi hiyo.

Lakini kuna baadhi ya wanasoka hao matata, walitua kwenye ligi hiyo tayari miaka ikiwa imewatupa mkono. Wametua kwenye Ligi Kuu England katika umri wa kizee kwenye soka.

Kutokana na hilo, mashabiki wa ligi hiyo wamekosa fursa nzuri ya kupata burudani matata kutoka kwa mastaa hao, ambako kwingine walikuwa bora na kucheza soka tamu la ujana wao kabla ya kutua England umri ukiwa umekwenda na kushindwa kuonyesha makali yao ya kibabe. Wametua Ligi Kuu England uzeeni.

Patrick Kluivert – Newcastle, miaka 28

Straika Patrick Kluivert alianza kutamba kwenye soka akiwa na umri mdogo, hadi wakati anafika miaka 28, tayari mwili ulishachoka. Staa huyo alijiunga na Newcastle United mwaka 2004 kipindi hicho akiwa na umri wa miaka 28, lakini alikuwa amechelewa. Mashabiki wengi wa Ligi Kuu England walitamani angetua kipindi cha miaka ya tisini angekuja kukutana na Alan Shearer huko kwenye kwenye kikosi cha Newcastle United na kutamba. Kwenye kikosi hicho cha Newcastle kwa msimu ambapo Kluivert alicheza hapo, timu iliishika nafasi ya 14 na msimu ulipomalizika, aliondoka zake.

Davor Suker – Arsenal, miaka 30

Straika Davor Suker ndiye kinara wa muda wote wa mabao kwenye Timu ya Taifa ya Croatia. Alikuwa staa wa taifa hilo kwenye Kombe la Dunia 1998, fainali zilizofanyika Ufaransa na wenyeji kubeba ubingwa. Suker aling’ara sana kwenye La Liga akiwa na kikosi cha Sevilla na Real Madrid kabla ya kwenda kujiunga na Arsenal mwaka 1999. Lakini wakati anatua kwenye Ligi Kuu England, tayari nyakati zilishaanza kumtupa Suker, kwani alikuwa na umri wa miaka 30. Fowadi huyo alidumu kwa msimu mmoja tu huko Highbury kabla ya kwenda kudumu kwa muda kama huo huko West Ham.

Jari Litmanen – Liverpool, miaka 30

Litmanen ni mmoja kati ya mastaa wa Ajax walikuwamo kwenye kikosi hicho wakati kilipobeba ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya katikati ya miaka ya tisa. Mwaka 2001, Litamanen alitua kwenye kikosi cha Liverpool kukipiga kwenye Ligi Kuu England, lakini kwa wakati huo tayari umri ulikuwa umekwenda, miaka 30. Majeruhi yalitibua maisha yake na hivyo kumfanya ashindwe kuwa na rekodi tamu huko Anfield. Alirudi England kujiunga na Fulham, lakini mahali hapo hakucheza mechi yoyote baada ya kukutwa na tatizo la moyo mazoezini.

Maicon – Man City, miaka 31

Mechi 76 kwenye kikosi cha Timu ya Taifa ya Brazil, hakika Maicon alikuwa beki matata wa kulia kwenye kikosi hicho cha Wacheza Samba kabla ya Dani Alves hajaja kuchukua mikoba. Kocha Jose Mourinho alikoshwa sana na huduma ya beki huyo wakati walipokuwa pamoja Inter Milan, mwaka 2010 walipobeba mataji matatu makubwa. Akapata nafasi ya kutua kwenye Ligi Kuu England, alipojiunga na Manchester City, lakini kwa bahati mbaya tayari umri ulikuwa umeenda, miaka 31. Majeraha yamemtibulia na kushindwa kumweka benchi Pablo Zabaleta.

Ruud Gullit – Chelsea, miaka 32

Staa Ruud Gullit aliwahi kusema kwamba mahali ambako alicheza na kufurahia zaidi mpira wake, kama sehemu ya kufurahia ni kipindi alichokuwa kwenye kikosi cha Chelsea. Hata hivyo, Gullit alitua Syamford Bridge, tayari umri ulikuwa umeshakwenda, miaka 32. Lakini, jambo hilo halikumzuia kuwa mmoja kati ya wanasoka bora kabisa kwenye Ligi Kuu England, akishinda namba mbili nyuma ya Eric Cantona katika tuzo ya mchezaji bora wa mwaka, huku akibeba Kombe la FA akiwa kocha mchezaji kwenye kikosi cha Chelsea.

Edgar Davids – tottenham, miaka 32

Mmoja kati ya wanasoka bora kabisa waliowahi kutokea huko Ulaya. Mdachi, Edgar Davids, kiungo wa mpira alitua kuichezea Tottenham Hotspur mwaka 2005 kipindi hicho akiwa na umri wa miaka 32. Edgar ametua kwenye Ligi Kuu England tayari akiwa kwenye nyakati zake za mwisho, ameshazeeka baada ya muongo mmoja wa kulitawala soka la Ulaya. aliisaidia Spurs kumaliza msimu wakiwa nafasi ya tano kwenye msimamo kabla ya kurudi zake Ajax, ambako pia hakuwa na maajabu, kwa sababu tayari umri ulikuwa ushamtupa mkono.

George Weah – Chelsea, miaka 33

Mmoja kati ya mastaa matata kabisa waliowahi kutokea kwenye soka la ulimwengu alikuwa George Weah. Staa huyo alifanya makubwa huko AC Milan, ambako mpira wake wa kiwango cha juu ulimfanya achaguliwe kuwa mwanasoka bora wa dunia. Mwaka 2000, Weah alijiunga na Chelsea kwa mkopo, lakini kipindi hicho tayari alikuwa na umri wa miaka 33. Alikwenda kukipiga pia kwenye kikosi cha Manchester City na ilikuwa ngumu kuamini kwamba staa huyo miaka mitano iliyopita alikuwa ameshinda tuzo ya Ballon d’Or.

Youri Djorkaeff – Bolton, miaka 33

Youri Djorkaeff alikuwa mmoja kati ya mastaa walioshinda Kombe la Dunia na ubingwa wa Ulaya wakiwa na kikosi cha Ufaransa. Alibeba Kombe la UEFA akiwa na kikosi cha Inter Milan. Ubora wake wa alichaguliwa kwenye kikosi bora cha mwaka cha Fifa. Akapata nafasi ya kutua kwenye Ligi Kuu England, alipokwenda kujiunga na Bolton Wanderers, lakini wakati huo fundi huyo wa mpira wa Ufaransa, tayari alikuwa na umri wa miaka 33. Hivyo, mashabiki wa England hawajamfaidi sana.

Zlatan Ibrahimovic – Man United, miaka 34

Straika mwenye tambo nyingi, Zlatan Ibrahimovic alitua kwenye Ligi Kuu England kuichezea Manchester United tayari akiwa na umri wa miaka 34. Hata hivyo, straika huyo wa Sweden, hakukwazwa na umri wake, ambapo alifunga mabao 28 katika kikosi hicho kabla ya kuanza kusumbuliwa na majeruhi yaliyomfanya aondoke zake Old Trafford kutimkia Marekani. Hivi karibuni mwenyewe alisema kwamba yupo tayari kurudi kukipiga Man United kama Kocha Ole Gunnar Solskjaer atahitaji huduma yake. Anakipiga LA Galaxy alikojiunga bure.

Esteban Cambiasso – Leicester City, miaka 35

Wakati kiungo Estaban Cambiasso ananaswa na Leicester City kwenye Ligi Kuu England, alikuwa na umri wa miaka 35, kwa sababu alitemwa na Inter Milan mwaka 2014. Ni jambo la wazi tu kukubali ukweli kwamba hata miguu yake ilikuwa imeshaanza kuwa na uchovu ndani ya uwanja. Cambiasso alicheza soka la kiwango cha juu kuchaguliwa kuwa mchezaji bora wa mwaka kwenye kikosi cha Leicester City kutokana na huduma yake, huku mashabiki wa England wakisikitika kwa mchezaji huyo alitua akiwa tayari umri umeshakwenda.

Henrik Larsson – Man United, miaka 35

Wakati anatua kwenye kikosi cha Manchester United, wengi walibeza usajili huo uliofanywa na Kocha Sir Alex Ferguson, kwa sababu Henrik Larsson alikuwa kwenye nyakati za mwisho za maisha yake ya soka. Staa huyo wa Sweden, alidumu kwenye kikosi cha Man United kwa wiki 10 tu, lakini shughuli yake haikuwa ya kitoto, alifunga kwa kadiri alivyotaka licha ya kwamba tayari alikuwa na umri wa miaka 35. Muda mfupi aliokuwa Old Trafford, Larsson alijitengenezea umaarufu mkubwa na kuonekana kama vile ni mchezaji wa siku nyingi mahali hapo.

Fernando Hierro– Bolton, miaka 36

Mhispaniola, Fernando Hierro alikuwa mmoja kati ya mabeki bora kwenye kufunga mabao huko Ulaya. Mwaka 2004, Hierro alikwenda kuungana na Youri Djorkaeff na Jay-Jay Okocha kwenye kikosi cha Bolton Wanderers kilichokuwa cha mastaa watupu, chini ya Kocha Sam Allardyce. Lakini, kwa bahati mbaya, beki huyo hakupata nafasi ya kutosha kuitumikia timu hiyo na kuonyesha uhodari wake kwenye Ligi Kuu England, huku sababu kubwa ya jambo hilo ikionekana kuwa ni umri wake.

Alitua Bolton akiwa na umri wa miaka 36. Umri ulishaenda.