Maftah: Luhende ni bonge la staa

BEKI wa zamani wa Simba na Yanga, Amir Maftah amesema licha ya mastaa wa klabu kongwe kuonekana kutikisa mbele ya mashabiki, mlinzi wa Kagera Sugar, David Luhende ni hatari zaidi.

Maftah alisema anaamini Luhende angekuwa anacheza Simba na Yanga kipindi hiki, basi angekuwa staa anayetajwa kila kona kutokana na uwezo anaouonyesha akiwa uwanjani.

Alisema Luhende ni beki mtulivu na anayejua kazi huku akisisitiza kwamba Simba na Yanga zikienda kucheza mechi na Kagera Sugar zinajua uwepo wake na ni kati ya wachezaji wanaoogopwa kuwaharibia mipango yao.

“Ukiwa nje ya Simba na Yanga ni ngumu kuongelewa na mashabiki, hata kama unafanya makuu huwezi kuongelewa kama wanavyoongelewa mastaa wao, labda itokee uwasumbue kwenye mechi zao ndipo unatupiwa jicho na ndicho ninachokiona kwa Luhende ambaye haangaliwi kiundani,” alisema Maftah na aliongeza kuwa:

“Mfano Prince Dube wa Azam FC, naona anatajwa tajwa kwa sababu tayari ndiye aliyeshika usukani wa mabao matano akiwaacha mastaa wa Simba na Yanga kwa nafasi hiyo, hawana namna ya kumtaja kila kona, ila angekuwa beki basi ngumu kusikia sifa zake.”

Maftah alisema anapenda aina ya uchezaji wa Luhende kwa sababu ndivyo alivyokuwa anacheza wakati anatikisa kwa kiwango akiwa na Simba na Yanga alizozichezea kwa nafasi tofauti.

“Luhende ni beki anayeweza akafanya mambo mengi, mfano anajua kutengeneza mashambulizi, mtaalamu wa kufunga na kupiga mashuti, yaani ana vitu vingi vyenye kupendezesha macho ya mtazamaji,” alisema.