Maeneo hatari kwa vibaka unapotinga Uwanja wa Taifa

Muktasari:

Mechi kama za Simba, Yanga na Taifa Stars, ni kati ya ambazo zimekuwa zikijaza watu kwenye uwanja huo wenye uwezo wa kubeba mashabiki 60,000.

BAADA ya Uwanja wa Taifa kuzinduliwa mwaka 2007, ilikuwa ni faraja kubwa kwa wapenda soka nchini.

Klabu za soka zilitambua kuwa sasa zitacheza kwenye uwanja wenye hadhi ya kimataifa na mashabiki walifurahi kuona wamepata kivutio kingine cha kwenda uwanjani kuangalia soka ukiacha nyota wanaowavutia na klabu zao.

Hamasa zinazofanywa kuvutia mashabiki uwanjani, zimechangia maelfu ya watu kufurika katika mechi zenye ushindani mkubwa.

Mechi kama za Simba, Yanga na Taifa Stars, ni kati ya ambazo zimekuwa zikijaza watu kwenye uwanja huo wenye uwezo wa kubeba mashabiki 60,000.

Muamko wa mashabiki umefanya hata mgeni kustuka anapokuja nchini na kukutana na wingi wa watu wanaofurika katika mechi zenye mvuto zaidi nchini.

Lakini mashabiki hawa huwa wanakutana na changamoto kubwa ya kukosa usalama hasa pindi mechi hizo zinapochezwa nyakati ya usiku. Mechi inapomalizika baadhi hukumbana na kadhia mbalimbali wakati wakielekea kupanda vyombo vyao vya usafiri kurejea makwao.

Kati ya kadhia hizo ni kukabwa na kuporwa baadhi ya vitu vyao vya thamani kama vile simu, pesa, mikufu, pochi, saa na vinginevyo.

Mwanaspoti linakuletea maeneo ambayo mechi ikichezwa usiku mashabiki wanalazimika kuwa katika tahadhari kuepuka kukwapuliwa, lakini pia kuvikumbusha vyombo vya usalama kuweka mikakati ya kumaliza suala hili.

UPANDE WA CHUO CHA DUCE

Mashabiki wengi wakiwa wanatoka huwa wanapenda kutembea kwa miguu kuanzia katika uwanja mkubwa wa Taifa wakielekea upande wa Chuo cha Duce kwaajili ya kwenda kupata magari yanayoelekea, Ilala, Magomeni na Kawe.

Vijana ambao wanakuwa wanawavizia huwa wanaanza kusimama pembezoni mwa nyumba za hapo. Wakiwa katika vikundi huwa wanakufuatilia kwa nyuma na usiombe ukawa peke yako katika eneo hili.

Vibaka hawa huwafuatilia mashabiki kuanzia geti la Duce lilopo upande wa Uwanja wa Taifa na huwa wanahakikisha wanamaliza kazi yao kabla hawajafika karibu na njia panda ya kwenda Keko na Mgulani kwani katikati huwa kuna giza kali ambalo linawaruhusu wao kufanya lolote lile.

KITUO CHA KWENDA MBAGALA KARIBU NA MATAA

Katika eneo hili huwa kuna changamoto ndogo lakini pia inaweza dhahiri ikawa kubwa pia, hii inatokana na vibaka hao kuwa wanakaa pembezoni ya ukuta wa Uwanja wa Uhuru wakiwa vikundi vikundi.

Eneo hilo huwa wanaonewa sana kinadada, kwani huvutwa pochi zao na wanapogeuka nyuma wanakutana na sura nyingi za vidume.

Katika kituo chenyewe pia huwa wanakaa na kutegea kuona namna ambavyo wanaweza kuwapora pochi na vitu vingine kinadada hao.

Wanawake wanaonekana kuwa waathirika wakubwa wa eneo hasa kwa wale ambao hutembea kwa mguu hadi Uhasibu.

KITUO CHA KWENDA BUGURUNI KARIBU NA ‘SHELI’

Kituo hiki mwanzoni mwa mwaka huu hadi waandishi wa habari wa chombo kimoja nchini waliwahi kukumbwa na vibaka waliowapora simu zao.

Eneo hili huwa na idadi kubwa ya vijana, miongoni mwao wakijifanya kama abiria, hivyo kwa mtu wa kawaida anakuwa anaona amani na kwenda katika kituoni.

Anapofika katika kituo hicho basi vibaka hao huwa wanawazunguka kama ni watu wawili na kuwachukulia simu zao, hilo huwa wanafanya kutokana na wingi wao.

Kitu kingine ukiwa eneo hilo wakiona tu umetoa simu wapo ambao anakufuata na kukuomba simu na unapotaka kuleta utata wengine wanaongezeka. Kutokana na giza lililopo eneo hilo ni ngumu kujitetea.

Kwenye mchezo uliochezwa Novemba 15 kati ya Tanzania na Guinea ya Ikweta wa kuwania kufuzu kwa fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) 2021, wengine waliibiwa mali zao katika eneo hilo hasa kwa upande wa jinsia ya kike.

BODABODA WATUMIKA KWENYE WIZI

Ukiwa unatoka uwanjani usiku huwa kuna foleni, matrafiki huwa wanajitahidi kuita gari zinazotokea Taifa ziende njia ya Buguruni pamoja na Mbagala.

Katika barabara ya inayoelekea Buguruni mara kwa mara huwa kuna foleni ndogo. Hapo vibaka hutumia pikipiki kupora simu na vitu vingine.

Vibaka hao hushuka na huwa wanatembea kwa miguu, wakiwa wanatembea wanaangalia watu wanaotumia simu huku wakiwa hawajafunga vioo vya magari katika foleni na kupora.

Wakati wakifanya hivyo bodaboda zinazoendeshwa na wenzao huwa zinakuwa zipo mbele kidogo tu zikiendeshwa mdogomdogo. Wakipora tu wanadandia pikipiki zao na kutimka.

POLISI WAFUNGUKA

Mwanaspoti lilimtafuta Ofisa Usalama Viwanjani, Inspekta Hashim Abdallah ambaye alisema suala hilo bado halijaripotiwa kwake lakini ataanza kulifanyia kazi.

“Taarifa kama hizo zinakuwa zinaripotiwa katika kituo cha Chang’ombe, mimi binafsi sijaripotiwa taarifa hiyo lakini mnaweza mkatusaidia kutujulisha kina nani wanafanya matukio hayo,” alisema.

Hashim aliongeza kama matukio hayo yatakuwa yanaripotiwa basi RPC wa Temeke atakuwa anayajua, lakini kama hayaripotiwi ni changamoto nyingine.