Madrid yanusa ubingwa, Zidane ataka heshima

Muktasari:

  • Real Madrid ndio bingwa wa kihistoria wa taji la Ligi Kuu ya Hispania wakiwa wametwaa ubingwa mara 33

Ushindi wa bao 1-0 ugenini dhidi ya Athletic Bilbao jana, umezidi kuiweka Real Madrid katika mazingira mazuri ya kutwaa Ubingwa wa Ligi Kuu ya Hispania 'La Liga' msimu huu.
Bao la Sergio Ramos lililotokana na penati iliyotolewa na mwamuzi Jose Gonzalez katika dakika ya 72 lilitosha kuifanya Real Madrid kujikita kileleni ikifikisha pointi 77 ambazo ni nne dhidi ya washindani wao wakuu, Barcelona wenye pointi 73.
Penati hiyo iliamriwa kwa msaada wa teknolojia ya video (VAR) baada ya Dani Garcia kumfanyia madhambi Marcelo katika dakika ya 70
Zikiwa zimebaki raundi nne kabla ya msimu kumalizika, Real Madrid inahitaji pointi nane tu katika mechi zake nne zilizobakia ili ijihakikishie ubingwa wa ligi hiyo msimu huu.
Hata hivyo ushindi huo umeonekana kuzua mjadala na kuibua hisia kuwa Real Madrid inabebwa kwani kabla ya kupatikana kwa penati iliyozaa bao hilo, Ramos alimfanyia madhambi Garcia ndani ya eneo la hatari la Real Madrid lakini Bilbao hawakupata penati.
Ushindi huo umeonekana kuwakosha Real Madrid ingawa tuhuma za kubebwa zimeonekana kumkera kocha wao mkuu, Zinedine Zidane ambaye amepingana nazo na kudai kuwa wanashinda kwa uwezo wao.
"Ni rahisi kuongea kuhusiana na kile ambacho kimetokea, lakini mimi nafikiri kuwa tunacheza vizuri kiwanjani na ndio maana tunapata kile ambacho tunachostahili
Sihitaji kuwa mmoja kati ya watu wanao jihusisha kwenye maongezi yao, lakini jambo ambalo siwezi kukubali kuendelea kusikia ni watu kusema  kuwa tupo kileleni, kwa sababu ya marefa
Tunahitaji heshima kubwa kwa kile ambacho tunafanya, na nimechoshwa na kauli za watu wanaodai kuwa tunashinda kwa sababu ya marefa," alisema Zidane.
Katika mechi nyingine, washindani wakuu wa Real Madrid katika mbio za ubingwa, Barcelona waliibuka na ushindi wa mabao 4-1 ugenini dhidi ya Villareal 'Nyambizi'
Bao la kujifunga la mchezaji wa Villareal, Pau Torres na mengi ya Luis Suarez, Antoine Griezman na Ansu Fati yalitosha kuipa ushindi mnono Barcelona huku lile la wapinzani wao likipachikwa na Gerard Moreno.
Katika mchezo huo, Lionel Messi alipachika bao moja ambalo lilikataliwa.
Ukiondoa mechi hizo, Espanyol ilifungwa bao 1-0 na Leganes wakati Osasuna ilitoka sare ya bila kufungana na Getafe.
Ligi hiyo itaendelea tena leo kwa uwepo wa mechi mbili ambapo Levante watacheza na Real Sociedad wakati Sevilla wataumana na Eibar.