Madrid yaanza kusaka ‘mbadala’ wa Pogba

Manchester, England. Matumaini ya kiungo Paul Pogba kwenda kujiunga na Real Madrid huenda yakashindwa kutimia baada ya miamba hiyo ya Satiago Bernabeu kuwafikiria wachezaji tofauti katika mpango wa kuunda Galacticos mpya.

Mabingwa hao wa La Liga wanatunza pesa zao kwa ajili ya kufanya usajili mkubwa kwenye dirisha la majira ya kiangazi la mwakani, huku wachezaji inaotaka kuwasajili ni Kylian Mbappe, Erling Haaland na kiungo kinda Eduardo Amavinga.

Pogba, 27, hakutaka kuweka siri kuhusu kuhusudi maisha ya kwenda kucheza Bernabeu.

Alhamisi iliyopita alisema: “Ndio, wachezaji wote wangependa kuichezea Real Madrid. Pengine ni ndoto. Ni ndoto kwangu, kwanini isiwe siku moja?”

Lakini, gazeti la AS linaandika kwamba Pogba anaweza kubaki kwenye huzuni kubwa. Mbappe anaendelea kubaki kwenye rada za Los Blancos baada ya kuonyesha dhamira ya kuachana na Paris Saint-Germain mwakani wakati huo mkataba wake ukiwa umebaki mwaka mmoja.

Ripoti kutoka Hispania zinadai kwamba PSG wanaweza kumuuza Mbappe kwa bei ndogo kati ya Pauni 111 milioni na Pauni 91 milioni wakati atakapoingia miezi yake 12 ya mwisho ya mkataba wake huko Paris.

Kiungo kinda Camavinga, 17, anasakwa kwa nguvu zote na Real Madrid huku wakipanga kutumia Pauni 25 milioni kumng’oa mchezaji huyo kutoka Rennes. Kocha, Zinedine Zidane atapiga hesabu pia za kumnasa Haaland kwenye majira yajayo ya kiangazi.

Straika, Karim Benzema, atakuwa bidhaa muhimu sokoni wakati atakapokuwa anapatikana kwa ada ya Pauni 70 milioni na timu kibao zinatajwa kwenye mpango wa kunasa saini yake.