Madrid wapiga dili la kijanja kwa Pogba

Muktasari:

Real Madrid ambao ndio hasa wanaonekana kwamba watakwenda kunasa saini ya kiungo huyo wameripotiwa kutenga mkwanja wa Pauni 73 milioni pamoja na wachezaji wawili, James Rodriguez na Mariano Diaz kwenye ofa yao ya kumchukua supastaa huyo wa kimataifa wa Ufaransa.

MADRID, HISPANIA . HABARI ndio hiyo. Real Madrid wameripotiwa kupania kumnasa kiungo wa Manchester United, Paul Pogba na wameshaweka mkakati wa kunasa saini ya staa huyo kwenye usajili ujao wa dirisha la Januari.
Kulikuwa na taarifa hivi karibuni kwamba Pogba amekuwa akijifanyisha kuwa hajapona vizuri ili kukwepa kuichezea Man United ili asipate majeruhi yatakayotibua dili lake la kutaka kuachana na wababe hao wa Old Trafford kwenye dirisha la Januari.
Real Madrid ambao ndio hasa wanaonekana kwamba watakwenda kunasa saini ya kiungo huyo wameripotiwa kutenga mkwanja wa Pauni 73 milioni pamoja na wachezaji wawili, James Rodriguez na Mariano Diaz kwenye ofa yao ya kumchukua supastaa huyo wa kimataifa wa Ufaransa.
Ripoti zinadai kwamba kocha Ole Gunnar Solskjaer atakabiliwa na wakati mgumu wa kufanya uamuzi kwenye dirisha hilo la Januari juu ya kufahamu hatima ya mchezaji huyo, ambaye anaonekana kama vile ameshapoteza uchu na kiu ya kuitumikia Man United. Pogba amecheza mechi tano tu kwenye Ligi Kuu England msimu huu na amekuwa nje ya uwanja kutokana na kuugua enka tangu Septemba.
Pogba anatarajia kurudi mazoezini wiki moja kutoka sasa, lakini madai hayo ya kwamba hataki kuichezea Man United yanaweza kumfanya mchezaji huyo akapigwa tu bei kwenye dirisha la Januari. Man United walimnasa Pogba kwa ad ya Pauni 89 milioni, lakini rais wa Los Blancos, Florentino Perez amepanga kutumia Pauni 73 milioni pamoja na wachezaji Rodriguez na Mariano ili kuwalainisha Man United wafanye biashara. Taarifa zinadai kwamba hata Rodriguez baada ya kusikia anahusishwa na Man United ameamua kuweka kando mpango wa kwenda kujiunga na Arsenal ili tu akakipige Old Trafford. Man United wamekuwa hawan maajabu kwenye fowadi yao baada ya kuwaruhusu washambuliaji wenye uzoefu, Romelu Lukaku na Alexis Sanchez kwenda Inter Milan kwenye dirisha lililopita la uhamisho wa majira ya kiangazi huko Ulaya.