Madrid ilipanga kuwakomoa Barca kupitia Eden Hazard

Muktasari:

  • Kawaida ya Real Madrid inaposajili mchezaji wake mkubwa ni lazima iende kumtambulisha mbele ya mashabiki wake huko Bernabeu.

MADRID,HISPANIA.REAL Madrid sio watu wazuri kabisa. Kumbe dili lao la kumsajili Eden Hazard limepangwa kwa ajili ya kufanya roho mbaya tu.

Hata hivyo, Liverpool wametibua kila kitu kuhusu mpango huo wa Real Madrid kwa supastaa huyo wa Stamford Bridge.

Taarifa za kutoka Ufaransa zinafichua dili zima la kumshuhudia Hazard akitoka Stamford Bridge na kutua Bernabeu limepangwa kwa ajili ya kufanya robo mbaya tu.

Supastaa huyo wa kimataifa wa Ubelgiji anajiandaa kwenda kujiunga na Los Blancos kwa ada inayotajwa huenda ikazidi Pauni 100 milioni.

Kawaida ya Real Madrid inaposajili mchezaji wake mkubwa ni lazima iende kumtambulisha mbele ya mashabiki wake huko Bernabeu.

Hicho ndicho kitu maarufu zaidi ambazo kimekuwa kikifanywa na wababe hao wa La Liga kutambulisha mastaa wao wa maana mbele ya mashabiki wao huko Bernabeu na Hazard usajili wake utakuwa mkubwa tangu alipoondoka Cristiano Ronaldo kutimkia Juventus mwaka jana.

Kwa mujibu wa L’Equipe, Los Blancos walipanga kumtambulisha staa wao Hazard, Juni 2, siku ya pili baada ya fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Wazo la kumtambulisha Hazard siku hiyo lilipangwa kwa ajili ya robo mbaya tu.

Madrid ilitaka kuwatibulia mahasimu wao Barcelona kwa sababu waliamini wangefika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu.

Ilipangwa utambulisho wa Hazard ufanyike siku hiyo bila ya kujali kama Barca watachukua ubingwa au watakosa, ili mradi tu waizime siku hiyo na stori kubwa iwe ya supastaa huyo wa Kibelgiji kutambulishwa huko Bernabeu na si ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Ilitaka kama Barcelona ingechukua ubingwa, basi siku ambayo wangetembeza kombe hilo mtaani, huko Bernabeu kufanyike utambulisho wa mchezaji mkubwa kama Hazard ili kuwazima wapinzani wao hao. Roho mbaya.

Lakini sasa Barcelona imetupwa nje ya michuano hiyo baada ya kufungwa kwenye mechi ya pili ya nusu fainali na kusukumwa nje kwa jumla ya mabao 4-3, hivyo mpango mzima umevurugwa na Liverpool.

Kutokana na hilo, Real Madrid sasa imeamua kubadilisha mpango wake huo na sasa bado haijafahamika itamtambulisha lini Hazard itakapokamilisha usajili wake.

Staa huyo wa Chelsea ni kipenzi kikubwa cha Kocha Zinedine Zidane na anamhitaji kwa nguvu zote atue kwenye kikosi chake kwa ajili ya mchakamchaka wa msimu ujao kwenye La Liga na Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Real Madrid inafahamu wazi wapinzani wao Barcelona wapo bize kufanya usajili wa maana kujiandaa na msimu ujao, hivyo na wao ni lazima waingie sokoni na kushusha vyuma vya maana huku kwenye orodha ya wachezaji inaowasaka wapo pia Neymar, Kylian Mbappe, Christian Eriksen na Pierre-Emerick Aubameyang.

Imekuwa ni kawaida kwa Madrid kusajili mastaa wenye majina makubwa na kwa orodha walionayo ni wazi msimu ujao chini ya Kocha Zinedine Zidane klabu hiyo itakuwa moto.

Barcelona wenyewe wanafanya usajili wao kimya na moto wao huonekana pale ligi inapoanza na msimu ujao watakuwa katika harakati za kutetea ubingwa wao na kufanya vyema michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.