Madrid, Man City zafanya mauaji Ulaya

Muktasari:

  • Miamba ya soka duniani, Real Madrid na Manchester City zimefanya mauaji katika mechi za Ligi ya Mabingwa Ulaya zilizocheza kwenye viwanja tofauti jana usiku.
  • Wakati Real Madrid ikipata ushindi mnono wa mabao 5-0 dhidi ya Viktoria Plzen, Man City iliibugiza Shakhtar Donetsk 6-0.

 

London, England. Real Madrid ikiwa ugenini imepata ushindi wa kishindo baada ya kuilaza Viktoria Plzen mabao 5-0.

Mabao mawili ya mshambuliaji nguli wa Ufaransa Karim Benzema, Gareth Bale, Casemiro na Toni Kroos yalitosha kumpa raha kocha wa muda Santiago Solari.

Mbali na miamba hiyo ya Makao Makuu Santiago Bernabeu, Manchester City ikiwa nyumbani kwenye Uwanja wa Etihad ilitoa dozi kwa wapinzani wao Shakhtar Donetsk kwa kuilaza mabao 6-0.

Mabao ya Man City yalifungwa na David Silva, Gabriel Jesus (matatu), Raheem Sterling na Riyad Mahrez.

Real Madrid ilipata ushindi zikiwa zimepita siku tisa tangu klabu hiyo ilipomtimua aliyekuwa kocha wa timu hiyo Julen Lopetegui.

Matokeo hayo ni mwanzo mzuri kwa kocha huyo wa kikosi cha pili ambaye amepewa jukumu la kuongoza timu hiyo huku klabu hiyo ikiendelea na mchakato wa kusaka kocha mpya.

Tayari majina makubwa yanatajwa akiwemo kocha wa zamani wa Chelsesa Antonio Conte na Roberto Martinez anayeinoa Ubelgiji.

Nahodha wa Real Madrid Sergoi Ramos alimpiga kiwiko beki Milan Havel puani na kusababisha mchezaji huyo kupatiwa huduma ya kwanza kutokana na kuvuja damu nyingi.

Hata hivyo, beki huyo wa kati anayependa kucheza ubabe, hakuonyesha kadi nyekundu na mwamuzi. Real Madrid na AS Roma zinakabana koo zikiwa na pointi tisa kila moja, CSKA Moscow nne na Viktoria Plzen moja katika Kundi G.