Madrid, Man City acha nyasi ziteseke

Muktasari:

Viwango vya timu hizo katika mechi zao tatu za mwisho za michuano mingine, Real Madrid imeshinda moja, sare moja na kichapo kimoja kwenye mchezo wao wa mwisho walipocheza na Levante kwenye La Liga, lakini Man City wao kwenye mechi zao, wameshinda mbili na kupoteza moja, walipochapwa na Tottenham Hotspur ya Jose Mourinho.

MADRID, HISPANIA . MANCHESTER City itakuwa na kete muhimu ya kucheza kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya leo Jumatano wakati watakaposhuka uwanjani Bernabeu kuwakabili mabingwa wa kihistoria wa michuano hiyo, Real Madrid.

Kocha Pep Guardiola anafahamu wazi kikosi chake kinapaswa kufanya kitu cha ziada msimu huu kunyakua ubingwa huo kabla ya kuingia kwenye adhabu ya kukosa michuano hiyo kwa misimu miwili baada ya kufungiwa na Uefa.

Staa wa Man City, Kevin De Bruyne amewaambia wachezaji wenzake wanahitaji kushinda ubingwa wa michuano hiyo msimu huu ili wasionekane kuwa wamefeli.

Man City itakwenda kukwaana na Los Blancos katika mchezo wa kwanza wa hatua ya mtoano ya raundi ya 16 bora.

Viwango vya timu hizo katika mechi zao tatu za mwisho za michuano mingine, Real Madrid imeshinda moja, sare moja na kichapo kimoja kwenye mchezo wao wa mwisho walipocheza na Levante kwenye La Liga, lakini Man City wao kwenye mechi zao, wameshinda mbili na kupoteza moja, walipochapwa na Tottenham Hotspur ya Jose Mourinho.

Hata hivyo, mchezo wa leo kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya inatarajia kuwa kali kwelikweli kutokana na Man City kupania kufanya kitu tofauti katika mchezo huo.

Mechi nyingine ya Ligi ya Mabingwa Ulaya itakayopigwa leo, Lyon itakuwa nyumbani kuikaribisha Juventus ya Cristiano Ronaldo. Usiku wa jana Jumanne kulikuwa na mechi mbili, Napoli walikipiga na Barcelona na Chelsea walijimwaga uwanjani Stamford Bridge kuwakabili Bayern Munich.