Madogo janja wanaolipwa pesa ndefu barani Ulaya

Muktasari:

Kwa mshahara huo mpya, Sancho anaingia kwenye 10 bora ya makinda wanaolipwa pesa ndefu. Lakini, unawafahamu wengine na anayeshika namba moja? Hapa hapa na umri wao.

LONDON, ENGLAND. STAA wa Kingereza, Jadon Sancho amesaini dili jipya kwenye kikosi cha Borussia Dortmund ambalo linamshuhudia akipokea karibu Pauni 200,000 kwenye mshahara wake kila wiki.

Mshahara huo mpya unamfanya winga huyo kuingia kwenye orodha ya wanasoka makinda wanaolipwa mishahara ya kibosi huko Ulaya kwa sasa, wakiweka majina yao kwenye ubao wa matajiri.

Umri wa Sancho ndio kwanza miaka 19, hivyo kulipwa mshahara unaokaribia Pauni 200,000 kwa wiki si pesa ndogo.

Hata hivyo, dili hilo jipya halina maana kwamba Sancho hatafikiria kuachana na timu hiyo, bali walichokifanya Dortmund ni kuweka mazingira ya kumpiga bei kwa pesa nyingi staa wao huyo pindi itakapotokea timu ikahitaji huduma yake.

Lengo la Dortmund ni kumuuza mchezaji huyo wa zamani wa Watford na Manchester City kwa pesa inayozidi Pauni 100 milioni, huku Man City chini ya Kocha Pep Guardiola ikitaka kumrudisha Etihad staa wake huyo wa zamani, kwenye vita ambayo watapambana jino kwa jino na mahasimu wao Manchester United, ambao wameweka wazi ikifika Januari mwakani wataanza kumfungia kazi Sancho ili akakipige Old Trafford.

Kwa mshahara huo mpya, Sancho anaingia kwenye 10 bora ya makinda wanaolipwa pesa ndefu. Lakini, unawafahamu wengine na anayeshika namba moja? Hapa hapa na umri wao.

Jadon Sancho – miaka 19, Pauni 190,000

Ripoti zinadai Manchester United imemtaja staa Jadon Sancho kuwa namba moja kwenye orodha ya wachezaji itakaowasajili kwenye dirisha la Januari mwakani. Zaidi ya Pauni 100 milioni zimedaiwa kutengwa kwa ajili ya kumng’oa Mwingereza huyo kutoka Borussia Dortmund. Sancho sasa akiwa na umri wa miaka 19, ni miongoni mwa makinda wanaolipwa mishahara mikubwa kwenye soka, akiwa anapokea Pauni 190,000 kwa wiki.

Gianluigi Donnarumma – miaka 20, Pauni 195,000

Kipa, Muitaliano Gianluigi Donnarumma ni mmoja kati ya makinda walionasa mikataba ya kibabe inayowafanya waingie kwenye orodha ya wachezaji wenye umri mdogo wanaolipwa pesa ndefu, akipokea Pauni 195,000 kwa wiki. Kipa huyo wa AC Milan amekuwa akihusishwa na mpango wa kuachana na timu hiyo huku PSG ikidaiwa kutaka huduma yake, ambapo bila ya shaka atakwenda kulipwa mshahara mkubwa zaidi kama atakwenda kujiunga na mabingwa hao wa Ufaransa.

Callum Hudson-Odoi – miaka 18, Pauni 200,000

Tangu dirisha la uhamisho wa Januari mwaka huu, winga Callum Hudson-Odoi alikuwa akitajwa kuwa kwenye mpango wa Bayern Munich wakisaka saini yake akakipige kwenye kikosi kuchukua mikoba ya Franck Ribery na Arjen Robben waliokuwa wanamaliza mikataba yao. Lakini, Chelsea iliweka ngumu na kumbakiza staa huyo huko Stamford Bridge, ambako wameripotiwa kumlipa pesa ndefu sana, Pauni 200,000 kwa wiki kumwingiza kwenye orodha ya makinda wenye pesa ndefu.

Marcus Rashford – miaka 21, Pauni 200,000

Straika Marcus Rashford amefanywa kuwa chaguo la kwanza la Kocha Ole Gunnar Solskjaer kwenye safu ya ushambuliaji ya timu hiyo ya Old Trafford kwa msimu huu. Hivi karibuni, fowadi huyo Mwingereza aliripotiwa kuwa kwenye mpango wa kusaini mkataba utakaomfanya alipwe kibosi zaidi katika kikosi hicho cha Man United, huku ikielezwa mshahara wake wa sasa ni Pauni 200,000 kwa wiki na hivyo kuwa mmoja kati ya wachezaji wenye umri mdogo wanaolipwa mishahara mikubwa huko kwenye soka la Ulaya.

Ousmane Dembele – miaka 21, Pauni 210,000

Staa wa Kifaransa, Ousmane Dembele amekuwa akihusishwa na mambo mengi katika dirisha hilo la uhamisho wa majira ya kiangazi huko Ulaya, kwamba huenda akatumika kwenye dili la Barcelona la kutaka kumrudisha Mbrazili, Neymar kwenye kikosi chao. Huduma ya Dembele huko Nou Camp si ya thamani mbaya, kutokana na kulipwa mshahara wa Pauni 210,000 kwa wiki. Dembele alitua kwenye kikosi hicho akitokea Borussia Dortmund kwenda kurithi mikoba ya Neymar, aliyekuwa akitimkia PSG, lakini sasa huenda akatumika kwenye dili la kumrudisha Mbrazili huyo huko Catalan.

Christian Pulisic – miaka 20, Pauni 230,000

Chelsea ilinasa huduma ya winga Christian Pulisic kutoka Borussia Dortmund kwenye dirisha la Januari mwaka huu, lakini alibaki huko kwenye Bundesliga hadi mwishoni mwa msimu na sasa ametua huko Stamford Bridge. Lakini, dili la staa huyo wa Marekani huko Chelsea si la mchezo, analipwa Pauni 230,000 kwa wiki na hivyo kuwa miongoni mwa wachezaji wenye umri mdogo wanaolipwa mishahara mikubwa kwa sasa huko Ulaya. Pulisic umri wake ni miaka 20 tu, lakini mshahara wake ni mzito.

Matthijs de Ligt – miaka 20, Pauni 245,000

Huduma ya beki huyo wa kati wa Kidachi ilisakwa sana kwenye dirisha hili la uhamisho majira ya kiangazi, wakati klabu vigogo wa Ulaya walipopambana kusaka saini yake hadi hapo aliponaswa na Juventus akitokea Ajax. Kubwa lililomfanya De Ligt afukuziwe sana ni kutokana na kiwango chake alichokionyesha Ajax msimu uliopita, hasa kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya. Dili lililompeleka De Ligt huko Turin si mchezo na anaripotiwa mshahara wake ni Pauni 245,000 kwa wiki na kuwa mmoja kati ya wachezaji makinda wanaolipwa mishahara ya kibosi.

Joao Felix – miaka 19, Pauni 255,000

Kinda wa Kireno, Joao Felix alitua kwenye kikosi cha Atletico Madrid kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi akienda kuchukua mikoba iliyoachwa na Antoine Griezmann aliyetimkia zake Barcelona. Kama ilivyo pesa ndefu kwenye uhamisho wake, Joao Felix hata akaunti yake ya beki imetuna kiasi cha kutosha kutokana na mshahara anaolipwa, ambapo anapokea Pauni 255,000 kwa wiki. Umri wa mshambuliaji huyo ni miaka 19 tu, lakini tayari anapokea mshahara unaomfanya kuwa miongoni mwa wanasoka wenye pesa huko Ulaya.

Kylian Mbappe – miaka 20, Pauni 325,000

Staa Kylian Mbappe ni mmoja kati ya washambuliaji matata kabisa wanaotamba duniani kwa sasa. Fowadi huyo wa kimataifa wa Ufaransa, huduma yake kwa sasa anaitoa huko kwenye kikosi cha PSG, ambako analipwa Pauni 325,000 kwa wiki ikiwa ni malipo ya mshahara wake.

Mbappe ni mmoja kati ya wanasoka wanaosakwa sana na klabu vigogo huko Ulaya, huku Real Madrid ikiweka wazi kwamba litakuwa chaguo lao la kwanza kwenye usajili wa majira ya kiangazi ya mwakani. Mbappe ni wa gharama.

Luka Jovic – miaka 21, Pauni 365,000

Pesa sabuni ya roho. Staa Luka Jovic kilikuwa kitu kidogo sana kwake kuondoka kwenye timu iliyomfanya kuwa staa mkubwa huko Ulaya, Eintracht Frankfurt na kujiunga na Real Madrid ambako hakujali kama atapangwa au atakaa benchi baada ya kuwekewa mshahara mnono mezani.

Fowadi huyo wa Kiserbia, ameripotiwa kulipwa mshahara wa Pauni 365,000 kwa wiki huyo Santiago Bernabeu na hivyo kuwa kinda anayelipwa mshahara mkubwa zaidi Ulaya kwa sasa.

Jovic alitua Real Madrid bila ya kujali wababe hao mpango wao ni kusajili wachezaji mastaa jambo ambalo linaweza kumfanya akaishia tu kusugua benchi.