Madogo 11 waliotisha makundi AFCON U17

Muktasari:

  • Makala hii inakuletea kikosi cha nyota 11 ambao wamefanya vizuri kwenye hatua ya makundi ya mashindano hayo ambao huenda hivi sasa majina yao yameshaandikwa kwenye vitabu vya mawakala na maskauti mbalimbali wa soka.

CAMEROON, Nigeria, Guinea na Angola zimekata tiketi ya kushiriki Fainali za Kombe la Dunia la vijana wenye umri chini ya miaka 17 baada ya kutinga hatua ya nusu fainali ya Fainali za Mataifa ya Afrika kwa vijana wa umri huo (AFCON U17) zinazoendelea hapa nchini zikipangwa kumalizika Jumapili Aprili 28.

Wenyeji Tanzania ‘Serengeti Boys’ wameaga mashindano hayo baada ya kushika mkia kwenye kundi A wakiwa timu pekee mwaka huu ambayo haikupata pointi hata moja, wakiungana na jirani zao Uganda huku kwenye kundi B timu za vijana wenye umri chini ya miaka 17 za Senegal na Morocco nazo zikifungasha virago.

Kuna mengi ya kufurahisha na kuhuzunishwa kwenye hatua ya makundi ambayo ilimalizika Jumapili iliyopita na sasa kinachongojewa ni hatua ya nusu fainali, mechi ya kuwania mshindi wa tatu na ile ya fainali ambayo itatoa mrithi wa taji lililo wazi kutokana na mabingwa watetezi Mali kutoshiriki fainali za mwaka huu.

Katika hatua hiyo ya makundi wapo wachezaji waliofanya vizuri ambao bila shaka wamevutia macho ya mawakala na maskauti mbalimbali waliopo nchini kusaka nyota wa kupeleka kwenye klabu mbalimbali Ulaya na kwingineko.

Makala hii inakuletea kikosi cha nyota 11 ambao wamefanya vizuri kwenye hatua ya makundi ya mashindano hayo ambao huenda hivi sasa majina yao yameshaandikwa kwenye vitabu vya mawakala na maskauti mbalimbali wa soka.

1. Sekou Camara - Guinea

Unaweza kupata wakati mgumu kumtaja kipa aliyefanya vizuri kwenye hatua ya makundi baina ya Sekou Camara wa Guinea pamoja na Taha Mourid wa Morocco kutokana na kiwango bora walichoonyesha kwenye mechi tatu walizochezea timu zao.

Wote wawili wamefanikiwa kuchukua tuzo ya mchezaji bora wa mechi mara moja lakini Camara anaweza kuwa chaguo la kwanza kwani ameweza kuibeba timu yake hadi ikafanikiwa kutinga hatua ya nusu fainali.

Ameonyesha uwezo mkubwa wa kuokoa mashambulizi ya ana kwa ana, mtulivu, mzuri wa kuzuia mipira itokanayo na krosi, kona na ‘frii-kiki’, anapanga vyema na kuikumbusha majukumu safu yake ya ulinzi, uwezo wa kusoma mchezo lakini pia anajua kuchezesha timu kuanzia nyuma.

2. Cheikh Diouf - Senegal

Mdogo kiumbo lakini ana akili na utulivu wa hali ya juu pindi anapomiliki mpira au kukabiliana na washambuliaji wa timu pinzani.

Ni mzuri katika kupandisha mashambulizi na amekuwa hana papara pale timu inaposhambuliwa na sifa yake nyingine ni uwezo wake wa kupiga pasi sahihi ambazo zimekuwa zikifikia walengwa.

3. Dabo Ibrahima - Guinea

Beki kisiki ambaye amekuwa hapitiki kirahisi na mawinga wa timu pinzani. Ana uwezo mkubwa wa kupandisha timu na kuzuia na kasi yake uwanjani imemuwezesha kutimiza vyema jukumu la kusadia mashambulizi na kuwahia haraka kuzuia pindi wanaposhambuliwa.

4. Fabrice Mezama - Cameroon

Ukuta wa Cameroon umeruhusu bao moja tu katika hatua ya makundi lakini pasipo shaka yoyote kazi nzuri ya nahodha wake Fabrice Mezama anayecheza kama beki wa kati imechangia hilo.

Ni mzuri katika kupanga timu, kucheza mipira ya juu na chini na amekuwa akitumia vyema umbo lake kuwadhibiti washambuliaji katika mapambano ya ana kwa ana.

5. Bere Francois - Cameroon

Anacheza kwa akili na hesabu za hali ya juu pindi anapokabiliana na washambuliaji wa timu pinzani, ni mtulivu na pia ni beki anayecheza kwa nidhamu kubwa na haishangazi kuona akimaliza hatua ya makundi pasipo kuonyeshwa kadi yoyote.

6. Fofana Ibrahima - Guinea

Ni mtaalamu wa kuvunja mashambulizi ya timu pinzani. Anajua kuilinda vyema safu ya ulinzi ya timu yake na anaweza kuichezesha vyema timu

7. Akunmi Amoo - Nigeria

Fundi wa kuuchezea mpira, kupiga pasi, kutengeneza nafasi za mabao pamoja na kumiliki mpira na ni mchezaji ambaye huwezi kuchoka kumtazama pindi anapokuwa ndani ya uwanja.

8. Osvaldo Capemba - Angola

Ni mchezaji anayeweza kuiunganisha vyema timu na kupiga pasi za mwisho sambamba na kufunga mabao. Ana uwezo mkubwa wa kuwasoma mabeki na viungo wa timu pinzani pamoja na uwezo wa kumiliki mpira.

Hadi sasa ndiye mchezaji anayeongoza kupachika mabao akiwa amefunga mara tatu.

9. Saidou Ismaila - Cameroon

Amepachika mabao matatu kwenye mashindano hayo na ni mchezaji ambaye ni tishio kwa mabeki wa timu pinzani kutokana na uwezo wake wa kukaa kwenye nafasi, kuisoma safu ya ulinzi ya timu pinzani kasi na utulivu wake pindi anapopokea mpira kwenye lango la timu pinzani.

10. Kelvin John ‘Mbappe’ - Tanzania

Amepachika bao moja tu kwenye mashindano hayo lakini amefanya kazi kubwa huku akiangushwa na kiwango duni kilichoonyeshwa na kikosi cha Serengeti Boys.

John ambaye anajulikana kwa jina la utani la Mbappe, ni mzuri katika kumiliki mpira, kuchezesha timu, kukaa kwenye nafasi na anajua kuvunja ukuta wa timu pinzani kutokana na chenga na kasi yake.

11. Tawfiq Bentayeb - Morocco

Ana akili ya kuuchezea mpira na ni vigumu kupokonywa au kudhibitiwa na mabeki wa timu pinzani pindi unapokuwa miguuni mwake.

Ni mchezaji anayecheza kitimu kwani pale mpira unapokuwa kwa wapinzani, huingia ndani na kuongeza idadi ya viungo na ana uwezo wa kufunga mabao kwa mashuti ya mbali.

Kocha - Pedro Goncalves (Angola)

Ni bingwa wa mbinu na anajua kuandaa mpango madhubuti wa kukabiliana na mpinzani kulingana na ubora wake.

Anabadilika haraka kulingana na aina ya mpinzani anayekabiliana naye lakini pia ni kocha anayeweza kuwajenga kisaikolojia wachezaji wake.