Madadi aitosa Simba, azuiwa getini Zanzibar

Saturday November 16 2019

 

WAZANZIBARI wana msemo wao ‘Ndio kwanza mkoko waalika maua’. Nami nasema ndio kwanza makala haya yanaanza kunoga.

Jana Ijumaa Mwanaspoti lilikuletea mazungumzo ya Mkurugenzi wa Mashindano wa Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF), Salum Madadi na Mwandishi Wetu,MOHAMMED KUYUNGA.

Katika maelezo hayo, Madadi alikumbushia mchezo wa fainali wa Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (sasa Kombe la Kagame), kati ya Simba na Yanga uliofanyika Zanzibar mwaka 1992.

Kocha huyo aliyekuwa akiinoa Simba kipindi hicho, alieleza jinsi mfadhili wa zamani wa Yanga, Abbas Gulamali alivyoivuruga kambi ya Simba kwa propaganda zake.

Gulamali alitengeneza maneno kuwa wachezaji sita muhimu wa Simba walikuwa wameshapewa pesa katika mpango wa kuihujumu timu hiyo dhidi ya Yanga.

Ilifikia hatua wafadhili wa Simba na uongozi wa klabu hiyo waliamini maneno hayo na kumtaka Kocha Madadi awafukuze wachezaji hao kambini.

Advertisement

Hata hivyo, kadiri mashindano yalivyokuwa yakiendelea, Simba ilifanya vizuri kwenye michuano hiyo na kufika fainali na kutakiwa kucheza dhidi ya Yanga, na hakukuwa na dalili za Madadi kuwafukuza wachezaji hao, ndipo wafadhili wa Simba walipofunga safari kutoka Dar es Salaam kwenda Zanzibar siku ya mchezo huo wa fainali.

Lengo la wafadhili hao lilikuwa ni kuhakikisha wachezaji wanaotuhumiwa kuchukua rushwa hawechezi dhidi ya Yanga. Je, walifanikiwa? Endelea kufuatilia maelezo haya…

Hadi siku hiyo ya mchezo wa fainali kati ya Simba na Yanga inafika, mtifuano ndani ya kambi ya Simba ulikuwa bado ni mkali na haikuonekana kama ungeweza kupata ufumbuzi.

Vikao vya hapa na pale vilikuwa vikifanyika ili kushinikiza wachezaji wanaodaiwa kupewa rushwa na mfadhili wa Yanga wasicheze mchezo huo.

Kwa upande wa pili ni Kocha Madadi tu ndiye aliyekuwa akiwaamini wachezaji wake kuwa hawakupokea mlungula huo kutoka kwa Gulamali huku akisapotiwa kwa mbali na aliyekuwa Mwenyekiti wa Simba, marehemu, Juma Salum.

“Niliwahakikishia (viongozi na wafadhili) kwamba iwe wachezaji wa Simba wamepewa pesa au hawajapewa wangecheza mchezo ule vizuri sana,” anasema Madadi.

MADADI AKAMATIWA GETINI

Kocha huyo anasema suala la Twaha (Hamidu) na Mohammed Mwameja kuitwa katika Hoteli ya Bwawani na wafadhili hao halikuisha salama.

“Pale ndipo palipozuka mzozo kati yangu na uongozi wa Simba. Kwa tukio lile la kumleta Twaha na Mwameja kutaka kuwahoji suala kuchukua pesa za Yanga.

“Kile kitu kilikuwa nje ya utaratibu wangu. Tukazozana sana. Nikaona isiwe tabu, nikaamua kuwaachia timu yao.

“Sikutaka kuwa sehemu ya jambo lile. Niliamua kuondoka zangu, hata hivyo hawakunipa nafasi hiyo, walinikamatia kwenye geti la kutokea la Hoteli ya Bwawani na kunirudisha chumbani.”

Madadi anasema hakutaka kuonyesha udhaifu wa kukubaliana na vitu vya hovyo. Alibaki na msimamo wake wachezaji walitakiwa kuheshimiwa na kuachwa wafanye kazi yao.

KIKAO KIZITO

Baada ya kuona hali imefikia hapo, ilibidi kuitishwa kikao kizito ambacho kilihusisha pande zote mbili ule wa wadhamini na viongozi na upande wa Kocha Madadi.

“Sasa uongozi na wadhamini (wafadhili) wa Simba nao wakapata nguvu kwa pamoja kikaitishwa kikao kuwajadili wachezaji waliopewa hongo ili wasitumike kwenye mchezo wa fainali wa siku hiyo.”

Madadi anasema kilikuwa kikao kizito kilichofanyika katika chumba chake, ndani ya Hoteli ya Bwawani lakini akawa anawazidi wapinzani wake kwa hoja baada ya wote kuamua kumkabiri moja kwa moja.

“Tukajidili, nikawaambia nyie viongozi nisikilizeni, tusizidiwe akili… Itanawezekanaje niwatoe wachezaji sita ‘key players’ halafu tuwafunge Yanga? All in all is the same… mi nikiwanao hawa kama mnavyoamini nyie nitafungwa. Na hata nikiwaondoka nitafungwa tena mabao mengi zaidi. Mi ninawahakikishieni hizi ni propaganda tu za kutuotoa mchezoni.”

JUMA SALUM AVISHWA KITANZI

Hali ilishakuwa mbaya ndani ya kambi ya klabu ya Simba. Maelewano yalikuwa mbali na muda ulikuwa ukitaradadi kuelekea kwenye mchezo huo wa wapinzani wa jadi.

Hatimaye, upande wa wafadhili uliamua kutumia kete yao ya mwisho kumaliza jambo hilo.

“Waliamua mwenyekiti wa Simba, Juma Salum ndiye atoe uamuzi wa mwisho kama wachezaji hao watumika au wasitumike kwenye mchezo huo.

“Katika fikra za kawaida nilijua Juma Salum atawaogopa wafadhili wale na kuungana nao. Nilikuwa na msimamo wangu, kama angeungana nao ningeondoka zangu. Na hata wao (wafadhili) walitarajia kwamba kiongozi huyo atakuwa upande wao. Lakini haikuwa hivyo, Juma Salum alisema: ‘mimi niko pamoja na kocha.’

“Basi, ukimya mzito ulitanda ndani ya chumba kile baada ya kauli ile ya Juma Salum. Watu walipigwa na bumbuwazi wakawa kama hawaamini vile kile walichokisikia kutoka kwa mwenyekiti.Wakagoma kuinuka katika makochi waliyokuwa wamekaa. Baadaye mmoja mmoja aliinuka na kuondoka chumbani mle bila ya kusema chochote.

“Wengine wakabadilisha kauli na kuanza kuungana na mimi…. Saa 10 nikaondoa Bwawani Hoteli na kwenda kambini kwenye Hoteli ya Kilimani.”

Madadi alikwenda kuungana na timu kwa ajili ya kuanza matayarisho ya mchezo huo ambao ulikuwa uchezwe siku hiyo saa 1:00 usiku.

Nini kilitokea zaidi? Tafadhali usikose Gazeti la Mwanaspoti kesho Jumapili.

Advertisement