Madadi : Abbas Gulamali alichafua hali ya hewa Simba 1992

Muktasari:

Kocha wa Yanga wakati huo, alikuwa Syllersaid Mziray ambaye kwa sasa ni marehemu. Upande wa Simba ulikuwa chini ya Kocha Salum Madadi.

MWAKA 1992 kulipigwa bonge la mechi katika Uwanja wa Amaan mjini Unguja, pale Zanzibar.

Illikuwa ni fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (sasa Kombe la Kagame) kati ya Simba na Yanga.

Mechi hiyo ilitawaliwa na mambo mengi sana ya ndani na nje ya uwanja. Ilikuwa na msisimko wa aina yake huku vituko vya hapa na pale vikichukua nafasi.

Kocha wa Yanga wakati huo, alikuwa Syllersaid Mziray ambaye kwa sasa ni marehemu. Upande wa Simba ulikuwa chini ya Kocha Salum Madadi.

Ili kupata baadhi ya vimbwanga vya mechi hiyo, Mwandishi wa Mwanaspoti, MOHAMMMED KUYUNGA amefanya mazungumza na Madadi ambaye kwa sasa ni Mkurugenzi wa Mashindano wa Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF) hebu ungana naye…

Kabla ya Madadi kupewa jukumu la kuinoa Simba, awali timu hiyo ilikuwa chini ya makocha Abdallah Kibadeni, Hassan Haffif na marehemu, Omary Mahadhi.

Kipindi alichopewa mikoba ya kuinoa Simba, mbele yake kulikuwa na mashindano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati yalikuwa yakifanyika Zanzibar katika makundi na timu mbili kufikia fainali.

“Nakumbuka ndio kwanza nilikuwa nimerudi freshi nikitokea Ujerumani kuchukua kozi ya ukocha, nilikaa kule kwa miezi sita. Niliporudi nikapewa jukumu la kuiongoza Simba kwenye mashindano hayo,” Madadi anaanza kusimulia katika mahojiano haya yaliyofanyika ofisini kwake, Karume, Ilala jijini Dar es Salaam.

KAMBI MBILI

Madadi anafafanua wiki mbili kabla ya mashindano hayo, aliona baadhi ya mambo hayaendi sawa ndani ya kambi iliyokuwa imewekwa jijini Dar es Salaam, akawaomba viongozi wake kuhamisha kambi kuelekea Arusha.

“Niliona mambo hayaendi vizuri kulingana na ukubwa wa mashindano yenyewe tuliyokuwa tunaenda kushiriki. Kwanza nilitaka nipate sehemu yenye utulivu mkubwa zaidi kuliko Dar es Salaam. Pili, nilitaka kuweka kambi sehemu ambao ina ‘high attitude’ (ukanda wa juu, kwenye hali ya hewa nzito) na timu itokee hapo kwenda Zanzibar kwenye mashindano.

Madadi anasema katika kumbukumbu zake mashindano hayo yalikuwa magumu kati ya yote aliyowahi kuyasimamia katika taaluma yake ya ukocha.

“Timu zilikuwa zimejiandaa kwelikweli na upinzani ulikuwa mkali kiasi cha kutosha,” anakumbuka na kutoa mfano wa mchezo wa kwanza ambao Simba ilicheza dhidi ya Jamhuri ya Pemba na kuambulia sare.

Kikubwa zaidi ambacho, Madadi anakikumbuka zaidi ni mchezo wa fainali dhidi ya timu yake na Yanga ambayo ulimpa wakati mgumu sana.

“Mechi ile ilikuwa na mambo mengi ndani na nje ya uwanja. Ilikuwa na misukosuko. Sitasahau tukio la wachezaji sita wa Simba kudaiwa kuhongwa na Yanga na wote key players (wachezaji muhimu).”

TAARIFA ZA SIMBA KUHONGWA

Madadi anasema katika mashindano hayo, ghafla zikazuka taarifa za kuwa kuna baadhi ya wachezaji nyota wa Simba wamehongwa na wapinzani wa wa jadi, Yanga.

Anasema taarifa hizo zilitoka kwa wafadhili wa Simba waliokuwa jijini Dar es Salaam. Wafadhili hao ndio walikuwa kila kitu katika kuiendesha klabu hiyo.

Anafafanua taarifa hizo zilimfikia hata kabla timu haijafika fainali kucheza na Yanga kwenye mashindano hayo.

Wafadhili waliokuwa wakitoa fedha zao kuihudumia Simba walimtaka Madadi awafukuze baadhi ya wachezaji kutokana na tuhuma hizo za kupewa pesa na mfadhili wa zamani wa Yanga, Abbas Gulamali (marehemu).

“Ilidaiwa wachezaji sita au zaidi walishahongwa na Gulamali tangu timu ikiwa Dar es Salaam, hivyo niwafukuze kambini kitu ambacho sikukukiafiki kabisa.

“Walinitumia ujumbe kwamba hali ni mbaya na kwenye maandalizi yangu niwaangalie zaidi wachezaji hao.

“Mtu aliyekuwa akiniambia taarifa hizo alikuwa anatumia lugha ya kidemokrasia sana. Nikajua huko Dar es Salaam moto umeshawaka na hali ya hewa imeshachafuka,” anakumbuka Madadi.

UNAMFAHAMU GULAMALI?

Madadi anasema alisita kuchukua uamuzi wa kuwatimua wachezaji hao kwa kuwa alikuwa akimfahamu vizuri Mfadhili wa Yanga, Gulamali katika masuala ya propaganda.

“Kwa bahati nzuri nilikuwa namfahamu Gulamali, niliamini alilizusha hilo jambo ili kuidhohofisha Simba. Zilikuwa ni propaganda zake tu na bahati mbaya, viongozi wa Simba waliyaamini maneno yale mia kwa mia na kutaka niwatimue wacheza hao.

“Nilipokuwa nikiwaangalia wale wachezaji kisaikolojia sikuona dalili zozote kama wamehongwa, ili tufungwe. Sikuwa tayari kukubaliana na uvumi huo, nilipuuza.”

Madadi ambaye pia alishawahi kuinoa Kariakoo Lindi katika Ligi Kuu anasema aliamini Gulamali alifanya hila akijua Simba ikipoteza wachezaji sita, itakuwa ni mteremko kwa Yanga katika mashindano hayo katika kubeba taji hilo.

“Wafadhili walipoona hadi tunafika fainali na tunacheza na Yanga sijawatimua wale wachezaji, watoa fedha wote wa Simba walikuja Zanzibar kwa nia ya kutaka kuwazuia wachezaji hao wasipate nafasi kwenye kikosi cha kwanza dhidi ya Yanga.”

MASTAA WALIOHONGWA

Madadi anawataja baadhi ya wachezaji wa Simba ambao walituhumiwa kuhongwa na Gulamali ni aliyekuwa kipa namba moja, Mohammed Mwameja ‘Tanzania One’, beki wa kushoto, Twaha Hamidu ‘Noriega’, kiungo, Hussein Marsha na beki wa kati, George Masatu.

Hata hivyo, mtaalamu huyo wa ufundi wa soka hakuweza kuwakumbuka wachezaji wengine wawili waliohusishwa na sakata hilo.

JANJA NYINGINE YA GULAMALI

Madadi anasema alijiridhisha hiyo ilikuwa ni janja ya Gulamali kwa sababu mfadhili huyo alishawahi kutaka kupiga naye picha katika Hoteli ya Bwawani.

“Nilikuwa nakaa Bwawani na timu ilikuwa inakaa Hoteli ya Kilimani, Gulamali alikuwa akija pale kwa ajili ya kuangalia mechi za Yanga. Siku moja alitaka tupige picha nikamtakalia.

“Nilimshtukia nikasema no, kwa kuwa nilijua picha ile angeitumia katika kutafuta chochote cha kuikorofisha Simba. Kipindi hicho timu zote za Simba na Yanga zilikuwa zinaingia nusu fainali ya michuano hiyo.”

WACHEZAJI WAFUKUZWE

Madadi anawataja wafadhili wa Simba waliokuwa wakishinikiza jambo hilo kuwa ni Jamal Motorways, Ramesh, Azim Dewji na wengine wengi waliokuwa wakitoa pesa kwa Simba wakati huo.

“Siku ya fainali walifika mapema asubuhi Zanzibar (wakitokea Dar)… wakambana Mwenyekiti wa Simba, Juma Salumu, wale wachezaji sita wasionekane kambini na wafuzwe.

“Juma Salum naye alikuwa na busara sana. Alikuwa hataki kuonyesha kama ananiingilia moja kwa moja.”

AWAZUI WAFADHILI KAMBINI

Kabla ya wafadhili hao kufika Zanzibar, Madadi alishajua mapema kama siku ya mchezo wa fainali viongozi na wadhamini wa Simba wengefika na kutaka kwenda kwenye kambi ya timu hiyo, hivyo alishapiga marufuku mtu yeyote kwenda kuzungumza na wachezaji.

“Siku hiyo nikapiga marufuku viongozi na wadhamini kwenda Kilimani. Nilimwambia mwenyekiti, leo kisayansi wachezaji hawatakiwi kuwa over motivated (kushawishiwa zaidi). Kama ahadi mlishatupa, zinatosha asiende mtu kwa nia ya kwenda kuzungumza na wachezaji kwa nia ya kuhamasisha ama vipi.

“Juma Salumu akaniunga mkono. Waliotoka Dar es Salaam wote hawakuruhusiwa kwenda Kilimani. Sasa vita, mvutano uliozuka pale Bwawani (walipofikia) ulikuwa sio wa kawaida.

“Baada ya Juma Salum kuwazidi nguvu wakaamua kuwaita wachezaji, kutoka Kilimani na kuja Bwawani. Walimwita Twaha Hamidu na Mwameja nafikiri. Sijui walimwambia kitu gani, nilimshtukia Twaha (Hamidu) akiwa pale saa nne asubuhi anatoka pale analia. Walimwambia kitu gani, sijui… Nikamuuliza wewe nani kakwambia uje huku wakati nilishapiga marufuku mchezaji kutoka pale kambini, ,” alisema Madadi.

Je, wafadhili walifanikiwa kuwafukuza wachezaji hao? Nini kilitokea? Usikose kusoma Mwanaspoti kesho Jumamosi ufahamu zaidi.