Macho yote kwa Chama Uwanja wa Taifa

Muktasari:

Kiwango bora ambacho Chama amekuwa akikionyesha tangu alipojiunga na Simba, kinamfanya atazamwe kwa jicho na hisia tofauti na timu hizo mbili zinazotupa karata ya kwanza kwenye hatua ya makundi ya mashindano hayo.

Dar es Salaam. Hapana shaka kiungo Cletous Chama ameiteka zaidi mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, baina ya Simba na JS Saoura itakayochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam leo saa 10 jioni.

Kiwango bora ambacho Chama amekuwa akikionyesha tangu alipojiunga na Simba, kinamfanya atazamwe kwa jicho na hisia tofauti na timu hizo mbili zinazotupa karata ya kwanza kwenye hatua ya makundi ya mashindano hayo.

Upande wa Simba wanamtazama Chama kama mtu anayeweza kuwabeba dhidi ya JS Saoura kutokana na uwezo wake wa kutengeneza mashambulizi, kuichezesha timu, kupiga pasi za mwisho na kufunga mabao umekuwa chachu ya Simba kufanya vizuri kwenye mashindano hayo hadi kufanikiwa kutinga hatua hiyo ya makundi.

Katika kudhihirisha hilo, mchezaji huyo wa kimataifa wa Zambia amehusika moja kwa moja katika mabao sita kati ya 12 ambayo Simba imefunga katika mechi nne zilizopita za mashindano hayo ambazo ilicheza dhidi ya Mbabane Swallows na Nkana Red Devils.

Chama katika mabao sita aliyohusika nayo ambayo kitakwimu ni nusu ya mabao yote yaliyofungwa na Simba kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, amefunga manne huku akipiga pasi mbili zilizozaa mabao.

Na katika mabao hayo manne ambayo amefunga kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, mawili amepachika katika mechi mbili tofauti ambazo Simba ilicheza Uwanja wa Taifa dhidi ya Mbabane Swallows na Nkana Red Devils.

Pamoja na sifa za moja kwa moja kwa nahodha huyo msaidizi wa timu ya Taifa ya Zambia, Kocha wa Simba, Patrick Aussems alisema kila mchezaji katika kikosi chake ana kiwango bora.

“Yeyote kati ya hawa 18 nilionao kwa ajili ya mchezo wetu ujao naweza kumtumia na akatimiza vyema majukumu. Na wote nimewaandaa vizuri na wako tayari kwa mechi,” alisema Aussems.

Wakati Simba ikimtazama kama jemedari wao JS Saoura bila shaka watamtazama kiungo huyo kwa jicho la ziada na kumpa ulinzi wa kipekee ili asiweze kuwaumiza kutokana na ufanisi na kiwango chake bora ndani ya uwanja.

Timu hiyo ya Algeria huenda ikaweka ulinzi mkali kwa kiungo huyo ili asiweze kufurukuta vinginevyo inaweza ikajikuta ipo matatani kwani amekuwa hafanyi makosa anaposogea lango la timu pinzani.

Ndani ya uwanja, Simba inaonekana itaendelea na mbinu ya kucheza soka la kushambulia kama ambavyo imekuwa ikifanya katika mechi nyingine ambazo imekuwa ikicheza.

Hata hivyo, Aussems anaonekana kuongeza mbinu za ziada katika staili ya kushambulia ambapo mbali na kujaribu kupenya kwenye lango la adui kupitia katikati kwa mtindo wa kupiga pasi fupi, Simba pia itatumia mashambulizi kutokana na krosi kutokea pembeni mwa uwanja na upigaji wa mashuti ya mbali.

Pamoja na uimara wa safu ya ushambuliaji, Simba inapaswa kuwa na tahadhari na umakini wa hali ya juu kwenye safu yake ya ulinzi ili isiweze kufanya makosa ambayo pengine yatawanufaisha wapinzani wao.

Mabeki wa Simba hasa wale wa kati Paschal Wawa na Juuko Murshid wanapaswa kucheza kwa nidhamu dakika zote 90 za mechi hiyo ili kukwepa kuingia katika mtego wa washambuliaji wa JS Saoura wa kujiangusha ili wapatiwe penalti na mwamuzi kama ambavyo wamekuwa wakisifika kwa tabia hiyo.

Katika kudhihirisha kuwa JS Saoura wanajua kudanganya waamuzi, msimu huu timu hiyo imefunga mabao sita kutokana na mikwaju ya penalti wanayopewa baada ya washambuliaji wao kuangushwa ndani ya eneo la hatari la timu pinzani.

Mchezaji anayepaswa kutazamwa zaidi na Simba na kuchungwa kwa umakini ni mshambuliaji Mohammed Hammia ambaye penalti tatu zilizozaa mabao matatu kati ya manne waliyofunga kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, amesababisha.

Ukiiweka mechi hiyo kwenye mizani, Simba ina nafasi kubwa ya kuibuka na ushindi kwa kuwa wapinzani wao wamekuwa hawana rekodi nzuri wanapocheza ugenini kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika. Kwa kuthibitisha hilo, JS Saoura haijafunga bao ugenini msimu huu.

Akizungumzia mchezo huo, Aussems aliliambia gazeti hili kuwa vijana wake amewaandaa vizuri na haoni hatari au presha kuhusu mbinu zake za kushambulia.

“Tutakuwa nyumbani mpango wetu ni kushambulia, nina kundi kubwa la wachezaji ambao ni washambuliaji,” alidai Aussems.