Macho: Hayo yaliyotusibu Ulaya na Zubery Katwila acha tu - 4

Muktasari:

Anasema, kama ilivyo kawaida maisha ya likizo na yeye anamiliki kwa wakati huo, akaamua atumie usafiri wake huo kurudi Tanzania dereva akiwa mwenyewe.

KATIKA sehemu tatu za kwanza za makala haya na kiungo wa zamani wa Yanga, Simba, Mtibwa Sugar na Taifa Stars, Yusuph Macho ‘Musso’, tuliangazia nyota huyo alivyogeuka mganga wa kienyeji baada ya kustaafu soka na historia yake alivyokinukisha huko Jomo Cosmos, Afrika Kusini. Tuungane tena leo.

AENDESHA GARI SAUZI HADI BONGO

Anasema, gari aliyopewa na tajiri wa Jomo Cosmos ilikuwa ni Toyota Corolla Saloon. “Maisha yalikuwa mazuri kule Sauzi na hata baada ya msimu kuisha akaniomba nisaini msimu wa pili ili niendelee kuwepo pale, lakini nilimwambia nitafanya hivyo nitakaporudi.”

Anasema, kama ilivyo kawaida maisha ya likizo na yeye anamiliki kwa wakati huo, akaamua atumie usafiri wake huo kurudi Tanzania dereva akiwa mwenyewe.

“Nilitumia gari hiyo kwa ajili ya usafiri wangu lakini pia kwa sababu lilikuwa langu hivyo ilikuwa lazima lije nyumbani Tanzania.”

MAJARIBIO ULAYA

Anasema, aliporudi Bongo aliendelea na mazoezi na alikuwa anafanya na timu ya Tanzania Stars ambayo ilifanya vizuri katika mashindano mbalimbali na kuwakilisha nchini Kombe la Shirikisho.

Akiwa anaendelea kujifua huko, Macho akapata dili la kwenda kufanya majaribio katika nchi ya Ulaya ya Kati ya Austria ambako alifuatana na Zubery Katwila ambaye kwa sasa ni Kocha wa Mtibwa Sugar.

“Majaribio tulifanya katika Klabu ya Austria Klagenfurt. Baada ya hapo tulikwenda Ubelgiji na Uholanzi ambako mambo yalikuwa mazuri, lakini tatizo lilikuwa kwa wakala aliyetupeleka, ambaye alidai pesa walizotaka kutoa klabu hizo zilikuwa ndogo,” anasema Macho. “Binafsi sikupenda ile hali na kumtaka wakala aniachie nifanye kazi kwa sababu Ubelgiji na Uholanzi ilikuwa uhakika lakini yeye aligoma na kusisitiza twende England.”

DILI LA ENGLAND

“Baada ya majibizano, akafanya mpango niende England kwa sababu kuna timu alikuwa anafanya nao kazi na kwa kiwango changu aliamini nitafanikiwa. Katika safari hiyo nilikuwa na mchezaji mwenzangu kutoka Ureno,” anaeleza Macho. “Mipango ya safari ilifanywa tukafika uwanja wa ndege tayari kwa safari lakini kilichotokea kamwe sitakuja kusahau maishani mwangu. Baada ya kukabidhi pasipoti, mwenzangu huyo Mreno na wakala kwa sababu walikuwa ni mataifa ya huko walifanikiwa, lakini yangu kwa sababu ni Tanzania ikagomewa na nilitakiwa kutafuta Visa ya kutoka nyumbani na si kuunganisha kule kule.

“Nililia sana, nilikumbuka mengi kwa sababu awali nilitaka kubaki Ubelgiji lakini tukaondoka na dili la England ndiyo hivyo. Basi jamaa wale waliondoka na kuniacha mimi nirudi nilipofikia ili wanifanyie mpango wa Visa.” Anasema, alikaa pale yule Mreno alifanya majaribio kwenye timu tano tofauti ikiwemo Arsenal lakini hakufanikiwa wakarudi na kunikuta mimi Austria.

“Nilitamani sana lakini haikuwa bahati lakini yule wakala aliendelea kufanya mpango wa Visa kuhakikisha naenda England. Tulihangaika na mwisho wa siku, tulikubaliana nirudi nyumbani Tanzania kushughulikia Visa ya England, nikarudi,” anasema Macho na kuweka wazi wakala yule alimkatia tiketi ya Austria - Tanzania mpaka England na anakumbuka alirudi Septemba 15, 1998.

VISA IKAWA VIZA

“Nilipofika Tanzania tu, wakala wangu alinijulia hali na kunipa moyo. Nikaenda Ubalozi wa England na kupeleka vielelezo vyote lakini maofisa wa pale walimkatalia na kusisitiza wanachohitaji kuona kibali cha kufanyia kazi kwanza. Ilinichanganya kwa sababu mimi nilikuwa nakwenda kwa majaribio na si kufanya kazi kama wao walivyofikiri,” anasema Macho ambaye tiketi yake hiyo ilikuwa ya mwaka mzima.

“Nilimfahamisha yule wakala na yeye aliwasiliana moja kwa moja na Ubalozi wa England wanipe Visa lakini ilishindikana. Nilihangaika mwenyewe mpaka dakika za mwisho nakumbuka nilienda mpaka kwa Kassim Dewji anifanyie mpango na yeye aliambiwa haiwezekani mpaka kibali cha kazi na safari yangu ikaishia hapo.”

ATUA MTIBWA SUGAR

Baada ya kuwa katika hali hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Klabu ya Mtibwa Sugar, Jamal Baysel alimfuata na kumsajili.

“Nakumbuka Jamal alinipa kitu kama Sh. 1.5 milioni hivi ilikuwa 1999-2000, nikacheza mwaka mmoja na uliofuata 2001 nikajiunga na Moro United na kukutana na kina Mao Mkami, Juma Kaseja, Ali Bushiri si huyu kocha wa makipa yeye alikuwa kiungo na Mrisho Moshi,” anasema Macho.

Anasema, akiwa Moro United, Simba walimwomba yeye pamoja na Nteze John ‘Lungu’ wakawasajili na kucheza 2002, 2003 na 2004.

MAISHA YA SIMBA

“Kiujumla maisha ya Simba yalikuwa mazuri na niliyafurahia kama kawaida ya mchezaji wa mpira hivyo naweza kufanya kazi mahali popote mambo yakaenda,” anasema Macho.

Akiwa Simba, Macho alishiriki mashindano tofauti kama Ligi Kuu na Ligi ya Mabingwa Afrika 2003 msimu ambao waliingia hatua ya makundi kwa mara ya kwanza.

Anasema, katika mashindano hayo ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2003 wao walitisha sana. “Tulifanikiwa kwa sababu sehemu kubwa ya wachezaji wale tulikuwa tumezoeana. Tulikuwa tumekaa pamoja kwa kipindi kirefu.”

Akizungumzia utofauti wa Simba yao na Simba ya sasa, Macho anasema: “Simba ya sasa ina wachezaji wazuri lakini bado hawachezi kitimu wengi ni uwezo wa mmoja mmoja. Hii inawezekana kutokana na kutokuwa pamoja kwa kipindi kirefu.

“Timu yetu ilikuwa nzuri zaidi kwa sababu wachezaji tulikuwa tunajuana, tulikaa pamoja kwa kipindi kirefu hivyo hata mambo mengi tulifanya kwa kujuana,” anasema Macho akibainisha kuwa kipindi hicho walikuwa wanafundishwa na Mkenya James Siang’a.

Usikose Mwanaspoti kesho uone yaliyojiri katika safari yake ya Uarabuni.