Machalii wa Kagera wanogewa

Muktasari:

  • Nahodha Msaidizi wa Kagera, Paul Ngwai alisema wanahitaji ushindi zaidi katika michezo yao, hivyo timu zilizobaki zijipange kwani hawatafanya mzaha kwenye kusaka pointi tatu.

KAGERA. USHINDI mtamu buana asikuambie mtu. Baada ya Kagera Sugar kupata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Simba nyota wa timu ni kama wamenogewa kwani mzuka wao umepanda maradufu na sasa wanapiga hesabu kuendeleza kugawa dozi ili kumaliza nafasi nzuri kwenye Ligi Kuu Bara msimu huu.

Simba inayotetea taji ilikumbana na kipigo hicho mwishoni mwa wiki kwenye Uwanja wa Kaitaba na kuwapa wenyeji nafasi ya kufikisha alama 39 na kuchupa kutoka nafasi ya 17 hadi ya 12, huku mfungaji wa bao la ushindi Ramadhan Kapera akisema matokeo hayo yamewaongezea nguvu na matumaini.

“Timu haiwezi kushuka daraja, haya matokeo yametuongezea morari na nguvu kubwa, kiafya nimeimarika, hivyo lolote linaweza kutokea ina maana nikifunga kila mchezo naweza kuwafikia walionitangulia” alisema Kapera mwenye mabao manne sasa.

Nahodha Msaidizi wa Kagera, Paul Ngwai alisema wanahitaji ushindi zaidi katika michezo yao, hivyo timu zilizobaki zijipange kwani hawatafanya mzaha kwenye kusaka pointi tatu.