Mabosi ngumi wapewa somo

Muktasari:

  • Nahodha wa zamani wa timu ya Taifa, Mzonge Hassani alisema lazima OBFT ikubali kuanza moja kwa kuboresha mfumo wa ufundi wa ngumi.

Dar es Salaam. Viongozi wapya wa Shirikisho la Ngumi za wazi (OBFT), wametakiwa kufuata misingi ya utawala bora endapo wanahitaji kufufua mchezo huo ulioporomoka kimataifa.

Kwa nyakati tofauti baadhi ya wadau wa ngumi za wazi nchini wametoa angalizo kwa uongozi huo uliochaguliwa hivi karibuni katika uchaguzi mkuu uliomrejesha aliyekuwa rais, Mutta Lwakatare huku Andrew Mhoja akichaguliwa kuwa makamu wa rais.

“Ngumi za ridhaa (sasa za wazi) zilipoteza dira, lakini tunaimani viongozi tuliowapa dhamana wataitumia kama changamoto ya kurejesha hadhi ya ngumi nchini,” alisema Mwenyekiti wa Chama cha Ngumi Dar es Salaam (Daba), Godfrey Akarory.

Alisema OBFT inapaswa kuwa na programu inayoeleweka na kutekelezeka, kuwaandaa vijana na kuhakikisha wanafanya kazi katika misingi ya utawala bora.

Nahodha wa zamani wa timu ya Taifa, Mzonge Hassani alisema lazima OBFT ikubali kuanza moja kwa kuboresha mfumo wa ufundi wa ngumi.

“Tunahitaji maandalizi ya muda mrefu, tuwe na mashindano ya mara kwa mara lazima tutafanya vizuri, lakini tukiwa na maandalizi ya zimamoto, tusijidanganye tutakwama,” alisema Mzonge.

Aliyekuwa kocha msaidizi wa timu ya Taifa David Yombayomba alisema viongozi wapya wajipambanue kuhakikisha mabondia wenye uwezo kutoka mkoa wowote nchini wanakuwa katika kikosi cha timu ya Taifa