Mabosi Yanga wakubali yaishe

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe.

KAMA ni kwenye mchezo wa ngumi unaweza kusema, Yanga imebanwa kwenye kona na sasa haina jinsi ila kukubali matokeo tu. Ndio, si mnajua kwa wiki kadhaa sasa kumekuwa na mzozo juu ya uchaguzi wa kuziba nafasi zilizo wazi Jangwani?

Kundi kubwa la wanachama wa klabu hiyo walitangaza kuugomea kwa madai ya kukiukwa katiba yao kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuendesha mchakato kibabe, huku wengine wakiunga mkono kuitishwa.

Lakini sasa jana Jumatatu, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe amekata mzizi wa fitina baada ya kusisitiza uchaguzi huo upo kama ulivyopangwa, huku akipangua hoja nne matata za viongozi wa klabu hiyo.

Yanga iliomba mchakato wa kuchukua na kurejea fomu kuanza upya, pia ilidai kwa Waziri wanaendelea kumtambua Yusuf Manji kama Mwenyekiti wao, kuhoji uhalali wa Barua ya TFF kumuondoa Clement Sanga ndani ya Bodi ya Ligi (TPLB) na ikataka Kamati ya Uchaguzi ya Yanga ipewe mamlaka ya kusimamia uchaguzi huo.

Hata hivyo, akitumia dakika 150, Waziri Mwakyembe alipangua hoja zote na kusisitiza uchaguzi wa Yanga ufanyike kama ulivyopangwa huku akiitaka Kamati ya Uchaguzi Yanga kushirikiana na ile ya TFF.

“Tutakuwa watu wa ajabu endapo tutafungua upya pazia la kuchukua na kurejea fomu, Yanga waliomba wakidai kuna wanachama wao walichelewa kupata taarifa, hivyo tuongeze muda, lakini haiwezekani,” alisisitiza.

Dk. Mwakyembe alisema, Yanga walikuja na hoja ya kumtambua Manji, lakini tangu wamesema yupo, hajawahi kujitokeza. “Amekuwa nje ya uongozi kwa miezi zaidi ya 18, hilo linatosha kumuondoa madarakani kwa mujibu wa Katiba ya Yanga, isitoshe Manji ni mtu mzima, hawezi kusemewa na watu, angejitokeza na kusema mwenyewe.

“Serikali hatutambui uwepo wake Yanga na niseme tu njia halali ya Yanga kumrejesha Manji ni uchaguzi, hawakumchukulia fomu ili agombee basi,” alisisiza.

Alisema hoja nyingine ilikuwa ya uhalali wa barua ya TFF kumuondoa aliyekuwa Kaimu Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga kwenye nafasi ya Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi kwa vile hakuwa na sifa tena baada ya kutambua kurejea kwa Manji Yanga kwani sifa ya Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi lazima uwe Mwenyekiti.

“Kwa hili sitaki kupepesa, TFF ilikosea na niseme hiyo barua ya TFF iliyomuondoa Sanga ilikuwa batili kwani Manji hakuwepo Yanga, tunafahamu hilo, ila licha ya kosa hilo, halizuii mchakato wa uchaguzi, zoezi liko pale pale,” alisema.

Alisema hoja ya Yanga kutaka kamati yao ya uchaguzi ipewe mamlaka ya kusimamia uchaguzi huo ilikuwa na mashiko, lakini ishirikiane na Kamati ya TFF kwa kuwa kamati ya Yanga ilikwishamaliza muda wake na uhalali wa kuteua kamati mpya huko chini ya Kamati ya Utendaji ya Yanga ambayo ina wajumbe wanne pekee kati ya saba wanaotakiwa ili kutimiza akidi.

Katika mkutano wa jana, Yanga iliwakilishwa Jaji John Mkwawa, Samwel Lukumay, Hussein Nyika, Thobias Lingalangala na Siza Lyimo walikubaliana na msimamo wa Serikali, huku Jaji Mkwawa akiomba utulivu kwa Wanayanga kuelekea uchaguzi wa Januari 13.

Wengine waliohudhuria kutoka TFF ni Rais Wallace Karia, Kaimu Makamu wa Rais, Athuman Nyamlani na Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya shirikisho hilo, Ally Mchungahela.