Mabondia wa Tanzania mguu sawa Olimpiki

Muktasari:

Mabondia 221 kutoka mataifa 39 wanachuana kusaka ubingwa wa Afrika na kuliwakilisha bara la Afrika kwenye michezo ya Olimpiki 2020 itakayoanza Julai 26 mjini Dakar.

Dar es Salaam.Kesho Ijumaa mabondia wa Tanzania wataanza kampeni ya kusaka ubingwa wa Afrika na tiketi ya kufuzu kushiriki michezo ya Olimpiki ya 2020.

Kikosi cha mabondia wanne wako nchini Senegal tayari kwa mashindano ya Afrika ambapo Nahodha wa timu hiyo, Alex Isendi atafungua dimba kesho dhidi ya Rarhat Mohamed Almnsori wa Libya.

Isendi atamkabiri Almnsori kwenye uzani wa light kilogramu 57, pambano la mkondo wa kwanza.

Keshokutwa Jumamosi, Boniphace Mlingwa atacheza na Manuel Pedro Gomes wa Angola katika uzani wa feather kilogramu 52.

Bondia wa uzani wa juu mwepesi, Haruna Swanga atazichapa na Kutsuke Anani wa Ghana Jumamosi na Yusuph Changalawe atacheza na Mauricio Martins wa Guinea Bissau katika uzani wa light heavy.