Mabondia Bongo mzuka tupo Senegal

Muktasari:

Mabondia hao wameambatana na kocha wao, David Yombayomba na mkuu wa msafara ni Samwel Mwera.

MABONDIA wa timu ya Taifa ya ngumi za ridhaa wametamba kufanya vyema katika michuano ya kutafuta tiketi ya kufuzu mashindano ya Olimpiki mjini Dakar, Senegal.

Mashindano hayo yamepangwa kuanza kesho na Tanzania itawakilishwa na mabondia wanne ambao ni Boniface Mligwa ambaye anachezea uzito wa Bantam, Yusuph Changarawe (light heavy), Haruna Swanga (super heavy) and Alex Isendi wa uzito wa Light.

Mabondia hao wameambatana na kocha wao, David Yombayomba na mkuu wa msafara ni Samwel Mwera.

Bondia maarufu wa mchezo huo, Swanga alisema kuwa wamekwenda kuiwakilisha nchi kwa kushinda na si kutembelea mji wa Dakar.

Alisema kuwa wamedhamiria kushinda medali katika mashindano hayo ambayo yanashirikisha mabondia kutoka nchi mbalimblai barani Afrika.

“Tunajua nini Watanzania wanataka kutoka kwetu, sisi hatuja kushangaa huku, tuna usongo wa kufanya vyema na kuleta medali za Olimpiki nyumbani. Kwa hiyo lazima tushinde hapa Dakar ili tuweze kwenda kushiriki Tokyo,” alisema Swanga.

Alisema kuwa hali ya hewa siyo tatizo na kwamba, wanaendelea kujifua vilivyo kabla ya kuanza mashindano hayo.

“Bondia yeyote atakayekuja mbele yetu tutampa kipigo, tupo hapa hakuna kuchagua bondia zaidi ya kuwa tayari kupambana na yeyote,” alisema.