Mabingwa RBA waanza kwa kipigo

Tuesday July 7 2020

By Imani Makongoro

Dar es Salaam. Wakati mashabiki wa mpira wa kikapu wakisubiri kwa hamu mechi ya watani wa jadi, Vijana City Bulls (VCB) dhidi ya Pazi itakayochezwa leo Jumanne jioni, 'dada' zao ambao ni mabingwa wa Ligi ya mpira wa kikapu mkoa wa Dar es Salaam kwa wanawake, Vijana Bulls Queens (VBQ) wameanza kwa kipigo.

VBQ ambaye ni bingwa mtetezi wa RBA kwa wanawake imeanza vibaya Ligi hiyo kwa kuruhusu kipigo cha pointi 47-43 dhidi ya Ukonga Queens.

Mkurugenzi wa Ufundi wa timu hizo na nahodha wa zamani wa timu ya taifa ya mpira wa kikapu, Bahati Mgunda amesema robo ya kwanza ndiyo iliwagharimu VBQ.

"Tulicheza vibaya robo ya kwanza, lakini robo ya pili hadi ya nne tulibadilika, japo hatukufanikiwa kurudisha pointi," amesema Mgunda.

VBQ ni ya tatu katika msimamo ikiwa na pointi moja, nyuma ya DB Lioness inayoongoza kwa pointi mbili na Ukonga Queens yenye pointi mbili zikitofautiana idadi ya vikapu vya kufunga na kufungwa.

Ukonga Princess ni ya nne huku mechi ya wapinzani wa jadi ya Jeshi Stars na JKT Stars ikisubiriwa kwa hamu upande wa wanawake.

Advertisement

Mechi nyingine ya watani wa jadi ni ile ya Vijana City Bulls (VCB) dhidi ya Pazi ambayo itachezwa leo Jumanne jioni kwenye uwanja wa Bandari, Kurasini.

VCB ambaye ni bingwa mtetezi wa RBA kwa wanaume itacheza mechi hiyo ikiwa na kumbukumbu ya kuifunga Pazi msimu uliopita.Mechi nyingine za leo, Chui itacheza na DTB, Young Stars na UDSM, Mgulani JKT na Kurasini Heat na Mabibo Bullet itacheza na Magnet.

Advertisement