Mabil, Deng waitosa Kenya waamua kuichezea Australia

Muktasari:

Awer Mabil (23), anayekipiga katika klabu ya FC Midtjylland, alizaliwa katika kambi ya wakimbizi ya Kakuma, kabla ya kuhamia nchini Australia (2006). Thomas Deng (21), anayekipiga katika klabu ya Melbourne Victory, alizaliwa na kukulia Jijini Nairobi, Wazazi wake wakiwa na asili ya Sudan Kusini.

Nairobi, Kenya. Siku ya Jumapili, Oktoba 14, Kikosi cha Harambee Stars, kilichosheheni mapro kibao kilishuka Uwanja wa Moi Kasarani, kuumana na Ethiopia, katika mchezo wa marudiano, kusaka tiketi ya kufuzu, mashindano ya Kombe la Mataifa Afrika, yatakayofanyika nchini Cameroon, mwakani.

Katika kikosi chake, Kocha wa Stars, Sebastien Migne, alikuwa na jumla ya maproo 12, saba kati yao wakiwa ni wa kikosi cha kwanza, huku watano wakisubiri kwenye benchi. Maproo hao ni pamoja wauaji walioiongoza Stars kuitandika Ethiopia 3-0. Ni mshambuliaji Michael Olunga (Kashiwa Reysol), Eric Johanna (IF Bromma) na nahodha Victor Wanyama (Tottenham).

Mbali na mastaa hao 12, Kenya bado inajivunia kuwa na nyota kibao wanaokipiga huko katika mataifa ya mbali, ambao kama wakiitwa wanaweza kutengeza vikosi vitano vya timu ya taifa, huamini?

Baadhi ya nyota hao, ambao wengi wao wana umri kati ya miaka 15-20, ni pamoja dogo anayefahamika kwa jina la Linton Maina, mzaliwa wa Berlin, Ujerumani, ambaye anaendelea kutesa kwenye Bundesliga. Anakipiga katika klabu ya Hannover 96.

Wengine ni Handwalla Bwana (Seattle Sounders), Vincent Harper (Bristol City), Daniel Anyembe (Esbjerg FB, Denmark) na Philip Mwene (Mainz 05). Hata hivyo, habari mbaya ni kwamba, Siku moja baada ya Stars, kuitandika Ethiopia pale Kasarani, Kenya ilikosa nafasi ya kuwatumia mastaa wawili, walioamua kuitumikia timu ya taifa ya Australia.

Nyota hao ni Awer Mabil na Thomas Deng. Oktoba 15 (Jumatatu), waliikana rasmi bendera ya Kenya, walipoamua kuipeperusha bendera ya Australia, katika ulimwengu wa soka. Ndio, Mabil na Deng walikuwa miongoni mwa wachezaji wa akiba katika kikosi cha Kocha wa Australia, Graham Arnold.

Nyota hao wawili waliingia dimbani katika kipindi cha pili na kufuta ndoto ya Shirikisho la soka nchini (FKF), kuwatumia katika shughuli za kitaifa. Mabil aliingia dimbani katika dakika ya 73, kuchukua nafasi ya Mathew Leckie na kutupia bao la nne wavuni katika ushindi walioupata wa 4-0.

Dakika mbili baada mbili baada ya Mabil, kufunga bao, Kocha Graham Arnold, alimuingiza Thomas Deng, kuchukua Joshua Risdon. Mabil (23), anayekipiga katika klabu ya FC Midtjylland, alizaliwa katika kambi ya wakimbizi ya Kakuma, kabla ya kuhamia nchini Australia (2006). Amewahi kuzichezea timu za U20 na U23, mara 15.

Naye Deng (21), anayekipiga katika klabu ya Melbourne Victory, inayoshiriki ligi kuu ya Australia, alizaliwa na kukulia Jijini Nairobi, Wazazi wake wakiwa na asili ya Sudan Kusini. Baadae alihamia Nchini Australia. Amezichezea timu za vijana za taifa hilo mara 14.