Mabeki wa kumbeba Klopp hawa hapa

LIVERPOOL,ENGLAND. JURGEN Klopp kichwa kinampasuka huko. Usiku wa jana Jumatano, chama lake la Liverpool lilikuwa na shughuli ya kuwakabili Ajax kwenye mikikimikiki ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Lakini, shughuli pevu zaidi inayomkabili Klopp ni kucheza bila ya huduma ya beki wake wa kati, Virgil van Dijk abaye ameumia goti na huenda akawa nje ya uwanja kwa msimu wote.

Katika kuweka mambo sawa, Liverpool isiwe na shida kubwa, kocha Klopp ameambiwa mabeki ambao anapaswa kuhangaikia saini zao wakati dirisha la uhamisho wa Januari litakapofunguliwa ili kumaliza tatizo.

Kocha huyo Mjerumani, ameambiwa beki wa kuanza naye ni Kalidou Koulibaly wa Napoli. Staa huyo wa Senegal akitua Anfield atakuja kuunda kombinesheni matata kabisa wakati Van Dijk atakapopona.

Hayo ni maneno ya kiungo wa zamani wa miamba hiyo ya Anfield, Don Hutchison, ambaye anaamini ni Koulibaly pekee atakayeifanya Liverpool isihisi kuondokewa na beki wake muhimu kikosini.

Kiungo huyo anamtaka Klopp afanye usajili wa mabeki makini ili kuepuka aibu atakapokutana na washambuliaji hatari kwenye Ligi Kuu England na kuweka matumaini yao ya kubeba ubingwa huo na ule wa Ligi ya Mabingwa Ulaya.

“Unaweza kuvuta hisia jinsi timu itakavyocheza na hapo unakutana na Tottenham ya Harry Kane au Man United ya Bruno Fernandes au Man City ya Sergio Aguero,” alisema.

“Ingetokea kwa wachezaji kama Sadio Mane au Mohamed Salah au Roberto Firmino, kuna watu kama Takumi Minamino na Diogo Jota wanaweza kuziba mapengo na hata kwenye kiungo pia.

“Lakini, ukimwondoa Virgil van Dijk nje ya kikosi hiki cha Liverpool, akiwa mmoja wa mabeki bora kabisa Ulaya na kwenye Ligi Kuu England, unaweza kuona presha inayowakumba mashabiki wa Liverpool kwenye kusaka ubingwa.”

Mabeki wengine ambao Liverpool inaelezwa kwenda kunasa huduma zao kufanya mambo kuwa matamu huko Anfield itakapofika Januari ni Dayot Upamecano wa RB Leipzig, Milan Skriniar wa Inter Milan, Samuel Umtiti wa Barcelona na Conor Coady wa Wolves, ambao saini zao ni hadi dirisha la Januari litakapofunguliwa, huku huduma ambayo Klopp anaweza kuinasa kwa kipindi hiki kama atahitaji basi ni ya Ezequiel Garay.