Mabeki hatari kwa kumwaga maji VPL

Muktasari:

Bila kujali kwamba krosi walizopiga zilizaa matunda ama kusababisha kupatikana kwa kona na hata nafasi za kusababisha kupatikana kwa mabao, hawa hapa ni baadhi ya mabeki ambao wamekuwa na mwendelezo bora

LIGI Kuu Bara hatimaye baada ya safari ndefu yenye vikwazo kufuatia kusimamishwa kwa miezi mitatu kutokana na janga la covid-19, imemalizika kwa timu ya Simba SC kuendeleza ubabe wakitwaa taji kwa msimu wa tatu mfululizo.

Kumekuwepo na matukio mbalimbali yaliyojitokeza wakati ligi hiyo ikiendelea, lakini leo hawa ni baadhi ya mabeki wa timu zilizoshiriki kati ya 20 - kuna wale ambao wamekuwa na kazi nzuri ya kusaidia mashambulizi ya timu kutokana na krosi zao dhidi ya timu pinzani.

Bila kujali kwamba krosi walizopiga zilizaa matunda ama kusababisha kupatikana kwa kona na hata nafasi za kusababisha kupatikana kwa mabao, hawa hapa ni baadhi ya mabeki ambao wamekuwa na mwendelezo bora wa ‘kumimina maji’ kwenda milango ya wapinzani msimu huu.

NICHOLAUS WADADA - AZAM FC

Mganda huyu ni beki wa kulia katika klabu ya ‘Wanalambalamba’ Azam FC. Timu hii imewahi kufanya usajili wa wachezaji wengi wa kigeni na kuachana nao kutokana na kutoridhishwa na viwango vyao pamoja na sababu mbalimbali, lakini kwa beki huyu iliyemsajili kutokea Vipers ya Uganda mwaka 2018, hajawahi kuwaangusha kwani ameendelea kufanya kazi nzuri ya kumimina maji kwa timu pinzani.

Alisajiliwa na kocha Hans Pluijm aliyekuwa amekabidhiwa timu hiyo akitokea Singida United.

SHOMARY KAPOMBE - SIMBA

Ukitaka kujua umuhimu wa nyota huyu matata kabisa wa Simba, kumbuka matukio mawili kuanzia la kuombwa sana kutengua uamuzi wa kuamua kutojiunga na mazoezi ya timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ kwa sababu ambazo hakuziweka wazi, licha ya ukweli kwamba alikuwa na umuhimu mkubwa wa kuichezea timu hiyo.

Tukio lingine ni lile la mashabiki wa Simba ambao walipaza sauti zao juu ya kiungo wa Azam, Frank Domayo aliyemchezea rafu mbaya kwenye mchezo uliopita wa robo fainali ya Kombe la Shirikisho (FA), ambalo hata hivyo tukio hilo halikuonekana na mwamuzi.

Kapombe amekuwa na msaada mkubwa kwa timu ya Simba kwa muda mrefu sasa akichangia mabao tofauti pamoja na kusababisha hekaheka kwa timu pinzani zilizokuwa na shughuli pevu ya kujilinda dhidi ya krosi zake hatari pindi anapopanda kushambulia.

JUMA ABDUL - YANGA

Achana na msimu mmoja nyuma ambao beki huyu hakuwa na nafasi kwenye kikosi chini ya kocha Mwinyi Zahera ambaye alimtumia zaidi Paul Godfrey ‘Boxer’ kucheza kama beki wa kulia na kumfanya Juma Abdul kusahaulika kwa muda mrefu.

Abdul huyu wa sasa chini ya makocha Luc Eymael na Charles Mkwasa ndiye yuleyule wa kabla ya Zahera ambaye alishinda Tuzo ya Mchezaji Bora wa Ligi Kuu kutokana na kasi yake na zaidi kazi nzuri ya kumimina krosi za hatari kwa timu pinzani. Hakuna shaka kuwa Abdul ni mkali wa krosi ambazo mara zote hugeuka kuwa hatari kwa ukuta wa wapinzani.

DAVID LUHENDE - KAGERA SUGAR

Mkongwe huyu aliyedumu kwa muda mrefu kwenye soka la ushindani, bado ana makali yake anayoendelea kuyaonyesha hususani kwenye kupiga krosi za maana tu na zenye hatari kwa timu pinzani.Achana na wakati anaichezea Yanga, krosi zake zikitumiwa vyema na washambuliaji nyota wa timu hiyo wakati huo, Luhende ambaye amecheza mechi zote za timu ya Kagera Sugar msimu huu chini ya Mecky Mexime.

Krosi zake ni za hatari kwa timu pinzani akiendelea kuthibitisha hilo msimu huu na kuwa mmoja wa wachezaji walioing’arisha timu hiyo.

MOHAMMED HUSSEIN - SIMBA

Kama ilivyowahi kuwa kwa Abdul wa Yanga aliyebeba Tuzo ya Mchezaji Bora wa Ligi Kuu licha ya kuwa ni beki, ndivyo ilivyo kwa Mohammed Hussein ‘Zimbwe Jr’ ambaye naye kutokana na kazi yake nzuri ya kumimina krosi tamu kwa timu pinzani, ni sababu iliyowahi kumpa tuzo ya mchezaji bora wa msimu.

Zimbwe Jr ameendelea kuwa mkali wa kushambulia kupitia upande wa kushoto ambapo ubora wake wa kupanda na kupiga krosi kwa timu pinzani, umemfanya aendelee kutawala kikosi cha kwanza na kumpoteza kabisa Gadiel Michael.

MICHAEL AIDAN - JKT TANZANIA

Moja ya krosi yake mujarabu kabisa aliyothibitisha kwamba yeye ni mkali wa kumimina maji, ni ile aliyoipiga kwenye uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma kwenye mchezo dhidi ya Yanga ambapo Aidan ‘Maicon’ alimimina vema mpira kutokea upande wake wa kushoto akilenga kuwa krosi lakini mpira wake ulienda kuzama kwenye nyavu za juu za goli na kuipa bao timu yake akimuachana kipa Metacha Mnata akiutazama mpira ukitikisa nyavu.

ISSA RASHID - MTIBWA SUGAR

Kazi nzuri ya Issa Rashid ‘Baba Ubaya’ ni ile ya kupiga mipira ya kona na kwenda moja kwa moja nyavuni kwenye mchezo dhidi ya Azam kwenye Uwanja wa CCM-Gairo, lakini pia aliwahi kufanya hivyo kwenye mchezo wa fainali ya FA jijini Arusha. Rashid naye amedumu kwenye kusakata soka kwa muda mrefu ikiwemo kuitumikia Simba,ambapo krosi zake siyo za mchezo pindi anapopanda kushambulia, kwani huwapa wakati mgumu mabeki na makipa kutokana na krosi zake.

Hawa ni baadhi tu ya mabeki wakali wa kumimina krosi kwenda kwenye lango la timu pinzani, wengine ambao nao sio haba ni Mwaita Ngereza wa Kagera Sugar, Mwinyi Hajji wa Singida United, Kelvin Kijiri wa KMC, Charles Manyanya wa Namungo, Bruce Kangwa wa Azam, Adeyun Saleh Yanga, Kibwana Shomary wa Mtibwa Sugar.